Nenda kwa yaliyomo

Koloseo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Koloseo mwaka 2020.

Koloseo (kwa Kiitalia: Colosseo; jina la Kilatini: Amphitheatrum Flavium) ni uwanja wa michezo[1] cha kale mjini Roma kilicho katika hali ya maghofu kutokana na umri wake wa karibu miaka 2000. Ni kati ya majengo mashuhuri zaidi mjini Roma na duniani kwa ujumla. Wakati wa Dola la Roma ilikuwa jengo kubwa kabisa lililojengwa na Waroma wa Kale.

Inahesabiwa kati ya maajabu mapya ya dunia na kati ya urithi wa dunia.

Historia[hariri | hariri chanzo]

Koloseo ilijengwa kuanzia mwaka 72 hadi 90 BK. Kaisari Vespasiano alianzisha ujenzi kwa kutumia mapato ya windo la vita ya Waroma dhidi ya Uyahudi na hasa hazina ya hekalu la Yerusalemu. Ilikamilishwa na Kaisari Titus.

Kiwanja kilikuwa na nafasi kwa watu 50,000 hadi 75,000. Watazamaji waliangalia maonyesho ambako watu au wanyama waliuawa. Michezo hii iligharamiwa na serikali kwa ajili ya wakazi wa mji kama burudani. Falsafa ya kisiasa ya Roma ilisema ya kwamba watu wanatulia wakipewa "panem et circenses" yaani "chakula na michezo".

Baada ya ushindi wa Ukristo dhidi ya dhuluma za kidini, mashindano ya kuua watu yalipingwa na Kanisa. Shindano la mwisho lilitokea mwaka 434/435. Mapigano dhidi ya wanyama yaliendelea hadi mwaka 523. Lakini baada ya mwisho wa Dola la Roma idadi ya wakazi wa Roma ilipungua na Koloseo haikutumiwa tena kwa michezo.

Katika karne zilizofuata wakazi wa Roma walitumia Koloseo kama windo la mawe kwa ajili ya ujenzi. Hivyo sehemu kubwa ya jengo imepotea.

Sehemu za ndani za Koloseo

Uharibifu ulisimamishwa na Papa Benedikto XIV aliyetangaza Koloseo kuwa ukumbusho wa mashahidi Wakristo waliouawa hapa na tangu 1744 imehifadhiwa.

Michezo katika Koloseo[hariri | hariri chanzo]

Michezo katika Koloseo ilikuwa hasa ya aina mbili:

  • mashindano ya wapiganaji walioshindana kwa silaha za kweli hadi kifo. Wapiganaji waliitwa na Waroma kwa jina la "gladiator" yaani "mwenye upanga". Wengi wao walikuwa watumwa lakini wengine walikuwa watu huru. Walijifunza mapigano kwa silaha kwa ajili ya maonyesho na kuitumia kwenye kiwanja mbele wa watazamaji. Walioshinda walipata tuzo na zawadi nyingi. Wegine walikufa na kusahauliwa.
  • mashindano kati ya watu na wanyamapori. Waroma wa Kale walikamata wanyamapori kutoka Ulaya na Afrika ya Kaskazini kwa ajili ya maonyesho hayo. Wanyama waliuawa na magladiator kwenye kiwanja mbele ya watazamaji, lakini ilitokea pia ya kwamba wawindaji waliuawa na wanyama.

Waroma wa Kale walipenda maonyesho hayo.

Wakristo jinsi waliowekwa mbele ya simba.

Palikuwa pia na michezo ya pekee:

  • kiwanja kilijazwa maji na jahazi, pia manowari ndogo, ziliwekwa humo ili zishindane. Michezo hii ilikuwa ghali sana na ni makaisari tu walioweza kugharamia michezo ya aina hii.
  • Tangu karne ya 3 Wakristo waliuawa kiwanjani kama sehemu ya maonyesho. Ukristo ulikuwa dini marufuku katika Roma ya Kale hadi mwaka 313. Wakati mwingine Wakristo walikamatwa kwa wingi na kupewa adhabu ya kifo. Walionekana walifaa kwa maonyesho ambako walisimamishwa mbele ya wanyamapori kama simba, chui au dubu.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. "Wikiwand - Koloseo". Wikiwand. Iliwekwa mnamo 2023-02-26.
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Koloseo kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.