Kisiwa cha Chole
Kisiwa cha Chole ni kisiwa kidogo kwenye funguvisiwa la Mafia ambayo ni sehemu ya mkoa wa Pwani, nchini Tanzania, ambacho kinapatikana katika Bahari ya Hindi.
Kisiwa kina eneo la takriban kilomita ya mraba 1. Kuna kijiji kimoja cha Chole chenye vitongoji vya Mwapepo, Mnyange na Kilimani ambacho ni sehemu ya kata ya Jibondo.
Historia
[hariri | hariri chanzo]Kufuatana na taarifa ya Oskar Baumann mji wa Chole ulianzishwa baada ya mashambulio ya Wasakalava kutoka Madagaska walioangamiza mji wa Kua kwenye kisiwa jirani cha Juani mnamo mwaka 1829. Bauman aliandika katika taarifa yake ya 1895 kwamba kila mwezi nazi milioni moja zilitolewa nje kutoka Mafia yote kupitia Chole, pamoja na kamba na mikeka[1]. Hadi sehemu ya kwanza ya karne ya 20 Chole ilikuwa mji muhimu zaidi wa Mafia yote. Kamusi ya Koloni za Kijerumani (1920) iliita Chole "mahali pakuu pa biashara pa visiwa vya Mafia"[2] na mwaka 1913 kulikuwa na makampuni ya biashara 13 ya Waarabu, Waswahili na Wahindi pamoja na makampuni 3 ya Wazungu.
Wakati ule wa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani Chole ilikuwa pia na vituo vya forodha na posta. Lakini meli kubwa za Kizungu zilishindwa kuingia katika bandari yake kutokana na uhaba wa kina cha kutosha zilifika Kilindoni kwenye kisiwa kikuu. Hivyo Wajerumani walihamisha makao makuu ya serikali kwenda Kilindoni kwenye mwaka 1913.
Baadaye umuhimu wa Chole ulipungua haraka; Waingereza walitwaa visiwa vya Mafia kwenye mwaka 1915; mashambulio yao dhidi ya koloni la Kijerumani yaliwahi hapa kwa sababu walitafuta njia ya kushambulia manowari ya SMS Koenigsberg iliyojificha kwenye delta ya mto Rufiji. Waingereza waliendelea kutumia Kilindoni kwenye kisiwa kikuu kama makao makuu ya utawala wao.
Leo hii kuna maghofu mengi ya majengo makubwa katika sehemu ya kisiwa inayoitwa "Chole mjini" iliyopo upande wa kaskazini wa kisiwa, karibu na kituo cha kivuko kwenda Mafia. Jengo la kituo cha forodha cha Wajerumani limekarabatiwa, kuna pia jengo la gereza la zamani linalotambuliwa kwa urahisi.
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]- Orodha ya visiwa vya Tanzania
- Orodha ya miji ya kale ya Waswahili
- Maeneo ya Kihistoria ya Kitaifa ya Tanzania
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Barua ya Baumann ya 7 Novemba 1895
- ↑ lingainsha makala Mafia kwenye [Koloniallexikon] (matini ya Kijerumani)
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- Chole Island kwa Geonames.org
- Oskar Baumann, Barua ya 7 Novemba 1895 kutoka Chole, Barua tano za Baumann (jer.) kuhusu safari yake kwenye visiwa kati ya Pemba na Kilwa, katika jarida ya Shirika la Jiografia ya Leipzig, nakala ya dijitali katika maktaba ya Chuo Kikuu cha Dresden, Ujerumani
Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Pwani bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Kisiwa cha Chole kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno. |