Gertrudi wa Thuringia
Mtakatifu Gertrudi (pia: Getrudi Mkuu; 1256 – 17 Novemba 1301) alikuwa mmonaki wa kike wa monasteri ya Helfta nchini Ujerumani.
Ametambuliwa na Kanisa Katoliki kuwa mtakatifu kama bikira.
Sikukuu yake ni tarehe 16 Novemba[1].
Maisha
[hariri | hariri chanzo]Gertrudi alizaliwa katika mji wa Eisleben, mkoa wa Thuringia, nchini Ujerumani mwaka 1256.
Katika utoto wake alilelewa na watawa wa kike Wabenedikto wa urekebisho wa Citeaux huko Helfta, ambako alifaulu vizuri katika masomo yake, hasa falsafa, historia na fasihi.
Alijiweka kabisa mikononi mwa Mungu, akasonga mbele haraka sana katika utakatifu, akitumia muda wake katika kusali na kufanya fikara.
Alifariki tarehe 17 Novemba 1301.
Sala yake
[hariri | hariri chanzo]Mungu, unayestahili upendo usio na mipaka, sina chochote cha kupimia vema ukuu wako, lakini hamu yangu kwako ni hivi kwamba, kama ningekuwa na yale yote uliyonayo wewe, ningekupa yote kwa furaha na shukrani.
Kwa ajili ya uongofu nakutolea, Baba mpenzi sana, mateso yote ya Mwanao mpendwa sana tangu wakati ule ambapo, akilazwa horini juu ya nyasi, alianza kulia, halafu akavumilia mahitaji ya utoto, mapungufu ya ubalehe, mateso ya ujana, hadi alipoinamisha kichwa akafa msalabani kwa mlio mkubwa.
Vilevile, kwa kufidia makosa yangu ya uzembe, nakutolea, Baba mpenzi sana, mwendo wote wa maisha matakatifu sana ambayo Mwanao pekee aliyaishi kikamilifu kabisa katika mawazo, maneno na matendo yake tangu atumwe kutoka ukuu wa kiti chako cha enzi kuja katika dunia yetu, hadi alipouonyesha mtazamo wako wa Kibaba utukufu wa mwili wake mshindi.
Kama shukrani nazama katika kilindi kirefu sana cha unyenyekevu, na pamoja na huruma yako isiyolipika, nasifu na kuabudu wema wako mtamu sana.
Wewe, Baba wa huruma, nilipokuwa ninapoteza maisha yangu hivyo, ulikuza kwangu mawazo ya amani, si ya mabaya, ukaamua kuniinua kwa wingi na ukuu wa fadhili zako.
Kati ya mengine, ulitaka kunijalia ujirani usiothaminika wa urafiki wako kwa kunifungulia kwa namna mbalimbali hazina ile azizi sana ya umungu, ambayo ni moyo wako wa Kimungu, na kwa kunitolea kwa wingi mkubwa kila utajiri wa furaha ndani yake.
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]- Watakatifu wa Agano la Kale
- Orodha ya Watakatifu Wakristo
- Orodha ya Watakatifu wa Afrika
- Orodha ya Watakatifu Wafransisko
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- Patron Saints Index: "Saint Gertrude the Great" Archived 19 Machi 2012 at the Wayback Machine.
- The Life and Revelations of Saint Gertrude the Great - the full text online. Archived 26 Machi 2012 at the Wayback Machine.
- "St. Gertrude the Great". Catholic Encyclopedia. New York: Robert Appleton Company. 1913. http://www.newadvent.org/cathen/06534a.htm.
Makala hii bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari. |