Shairi
Shairi (kwa Kiingereza: poem) ni aina ya fasihi. Mashairi ni tungo zenye kutumia mapigo ya silabi kwa utaratibu maalumu wa kimuziki kwa kutumia lugha ya mkato, lugha ya picha na tamathali za semi.
Mashairi ndiyo fasihi pekee duniani ambayo huingizwa katika fasihi andishi na fasihi simulizi.
Mashairi huweza kuandikwa au kutungwa kulingana na jinsi yanavyoonekana. Hii ina maana kuwa, mashairi huweza kutofautishwa kwa idadi ya mishororo, jinsi maneno yalivyopangwa, urari wa vina na kadhalika. Mtu anayetunga shairi huitwa malenga. Mtu anayekariri au kuimba shairi huitwa manju.
Kuna mashairi yanayofuata taratibu za kimapokeo, yaani yanazingatia taratibu za urari na vina, mizani, idadi sawa ya mistari, vituo na beti. Mashairi hayo huwa na mizani 14 au 16 katika kila mstari, yaani mizani 7 au 8 kwa kila kipande cha mstari.
Pia kuna mashairi yasiyofuata utaratibu huo wa kimapokeo na huitwa mashairi ya kimamboleo. Mashairi hayo mara nyingi ni nyimbo.
- Mfano
- Tulopeleka bungeni, wamegeuka nyang'au,
- Mafisadi kama nini, baladhuli mabahau,
- Wanavunja mpini, konde wamelisahau,
- Zamani na siku hizi, mambo sivyo yavyokuwa.
- Mwalimu mwana elimu, asiyekujua ni nani?
- Kwake ilete elimu, liyopewa na Maanani,
- Watu wote wafahamu, hapingiki hasilani,
- Adharauye mwalimu, kapungua akilini.
Aina za mashairi
Kuna aina kuu mbili za mashairi, nazo ni kama ifuatavyo:
(i) Mashairi ya kimapokeo
Haya ni mashairi yanayozingatia kanuni za muwala/urari (ulinganifu) wa mizani, vina, idadi ya mistari katika kila ubeti na kituo katika shairi. Vilevile huitwa mashairi funge.
Aina ya mashairi kulingana na mtindo huu wa mapokeo,hupatikana kwa kuangalia idadi ya mishororo katika kila ubeti.
(ii) Mashairi huru
Haya ni mashairi yasiyozingatia kanuni za kimapokeo, yaani, hayazingatii kanuni za muwala/urari (ulinganifu) wa mizani, vina, idadi ya mistari katika kila ubeti na kituo katika shairi. Mashairi haya huitwa pia mashairi ghuni/mashairi ya kisasa/masivina/mapingiti.
Mizani
Mizani ni ulinganifu wa idadi ya silabi katika kila kipande au mistari ya ubeti wa shairi. Mara nyingi mashairi ya kimapokeo huwa na mizani nane (8) kwa kila kipande na mizani kumi na sita (16) kwa kila mstari (mshororo). Vile vile katika mashairi mengine, mizani huwa saba (7) kwa kila kipande huku kila mshororo ukiwa na mizani kumi na minne (14).
Vina
Vina ni silabi zenye sauti ya namna moja zinazotokea katikati au mwishoni mwa kila mshororo wa kila ubeti wa shairi. Hivyo basi kuna vina vya kati na vina vya mwisho.
Ili shairi lako lihesabike kama limetimia vina, ni lazima herufi za mwisho na za kati za ubeti wako ziwe zinafanana.
Vina vya kati katika kila ubeti lazima vifanane, navyo vina vya mwisho pia ni lazima vifanane kwenye ubeti.
- Mfano katika shairi
Baba tumekosa nini, wanao kutukimbia. Umetuachia nani, mwengine kukimbilia.
Vina vya kati ni "ni" navyo vya mwisho ni "ia" katika kila mshororo.
Ubeti
Ubeti ni fungu la mistari lenye maana kamili. Ubeti unaweza kulinganishwa na aya katika maandiko ya kinathari. Mara nyingi ubeti huishia katika kituo. Ubeti mmoja unaweza kuwa na:
- Mstari mmoja (tamonitha)
- Mistari miwili (tathiniya/tathinia/uwili): shairi hili huwa na mishororo miwili katika kila ubeti. vina vyake vyaweza kuwa na mtiririko.
- Mistari mitatu (tathilitha): shairi hili huwa na mishororo mitatu katika kila ubeti. vina vyake huenda vikawa na urari.
- Mistari mine (tarbia): shairi la aina hii huwa na mishororo minne katika kila ubeti. mara nyingi shairi hili hugawanywa katika sehemu mbili, ukwapi na utao. Mshororo wa kwanza wa shairi hili huitwa kipokeo, wa pili huitwa mloto,wa tatu huitwa mleo, wa nne huitwa kibwagizo. kibwagizo huwa kinarudiwarudiwa katika kila ubeti.
- Mistari mitano (takhmisa): hili ni shairi lenye mishororo mitano katika kila ubeti
- Mistari zaidi ya mitano (sabilia), kwa mfano: tasdisa huwa na mishororo sita katika kila ubeti, tathmina huwa na mishororo minane katika kila ubeti, ukumi huna na mishororo kumi katika kila ubeti.
Aina za mashairi jinsi yanavyojitokeza
- Kikwamba ni aina ya shairi lililo na kibwagizo ambacho ni kifupi ukilinganisha na ile mishororo mingine. hili huweza kuuchukuwa mfumo wa mashairi yale mengine.
- Ngonjera: shairi hili huhusisha waimbaji zaidi ya mmoja ambao uimbaji wao huwa katika mfumo wa majibizano.
Kituo
Ni mstari (mshororo) wa mwisho katika kila ubeti wa shairi ambao huonesha msisitizo wa ubeti mzima au shairi zima. Wakati mwingine kituo huitwa kibwagizo/korasi/mkarara/kiitikio.
Kibwagizo ni mshororo wa mwisho katika ubeti ambao unajirudiarudia.
Tazama pia
Makala hii kuhusu mambo ya lugha bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Shairi kama historia yake, uenezi au maendeleo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |