John Bosco
Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
John Bosco (16 Agosti, 1815 – 31 Januari, 1888) alikuwa padri wa Kanisa Katoliki na mwanzilishi wa Shirika la Mt. Fransisko wa Sales (kwa Kiingereza Salesian Congregation).
Alijitahidi hasa kuwaelimisha watoto na vijana wa kiume.
Mbinu zake za malezi ni kwa pamoja: akili, dini, hisani. Hakutaka kurekebisha vijana kwa ukali, bali kuwakinga dhidi ya maovu kwa wema. Upendo wake wa ajabu kwa vijana ndio siri ya mafanikio yake ya ajabu katika malezi.
Yaliyomo |
[hariri] Utoto
Giovanni Bosco alizaliwa na Francesco Bosco na Margherita Occhiena tarehe 16 Agosti 1815 karibu na Castelnuovo d'Asti, leo Castelnuovo Don Bosco. Baba yake alifariki mwaka 1917 akimuachia mke wake watoto watatu. Ilikuwa miaka migumu kwa maradhi na njaa, lakini mama yake alijitahidi kuwatunza na kuwalea vizuri.
Alipokuwa na miaka 9 Yohane alipata ndoto ya kinabii iliyomtabiria utume wake kwa vijana. Baadaye Mungu alizidi kumjalia karama nyingi za pekee.
Kufuatana na ndoto hiyo, Yohane aliamua kuwa padri, ingawa hakuweza kusoma hata shule ya msingi, kwa sababu ilikuwa mbali. Lakini taratibu mama alimfanyia mpango dhidi ya upinzani wa kaka yake. Wakati huohuo alianza utume wake akitumia vipawa vyake vyaajabu.
Tarehe 26 Machi 1826, siku ya Pasaka, alikubaliwa kupokea ekaristi ya kwanza kabla ya wakati.
[hariri] Seminarini
Alipokwenda Chieri, pamoja na kuendelea vizuri na masomo, alifunga urafiki na Luigi Comollo, kijana mwema aliyemsaidia kuthamini wokovu wa milele kama jambo muhimu pekee, hata Yohane alifanya kauli mbiu ya maisha yake maneno: "Da mihi animas, caetera tolle" ("Unipe roho za watu, uniondolee mengine yote").
Kwa shauri la Yosefu Cafasso tarehe 30 Oktoba 1835 aliingia seminari ya Chieri. Tarehe 3 Novemba 1837 alianza masomo ya teolojia, na tarehe 29 Machi 1841 akapewa daraja takatifu ya ushemasi, na tarehe 5 Juni 1841 upadri huko Torino.
Badala ya kuitikia mialiko ya kufanya utume wenye malipo mazuri, mnamo Novemba 1841 alijiunga na Bweni la Torino, ambapo padri Luigi Guala, akisaidiwa na Cafasso, alikuwa anakamilisha malezi ya mapadri vijana 45 waweze kukabili ulimwengu wa wakati huo.
[hariri] Kukutana na vijana wenye shida
Huko Torino kulikuwa na watoto 7184 chini ya umri wa miaka 10 waliofanya kazi viwandani. Yohane Bosco aliwatafuta ili kuwasaidia kijamii na kidini.
Pamoja na Cafasso alitembelea magereza akashtuka kuona hali ya wafungwa vijana. Kwa wema wake aliwavuta kumuahidia wamuendee mara baada ya kutoka.
Tarehe 8 Desemba 1841 Bartolomeo Garelli alikuwa wa kwanza kujiunga na kundi lake (Oratorio). Muda mfupi baadaye vijana walikuwa wengi hivi hata akahitaji msaada wa mapadri watatu na vijana wakubwa kadhaa.
Hatimaye tarehe 12 Aprili 1846 alipata nafasi kwa vijana wake: kibanda na kiwanja huko Valdocco.
[hariri] Kueneza utume kwa vijana
Mwaka 1854 alianzisha shirika la mapadri kwa utume wa vijana (kifupisho chake ni SDB).
Miaka 10 baadaye alianza ujenzi wa patakatifu pa Bikira Maria Msaada wa Wakristo (ndivyo alivyopendelea kumuitamama wa Yesu).
Mwaka 1872, pamoja na Maria Domenica Mazzarello, alianzisha shirika la Mabinti wa Bikira Maria Msaidizi, ili walee wasichana kwa roho ileile.
Mwaka 1875 alianza kutuma Wasalesiani wa kwanza huko Argentina, na wakati huohuo alianzisha kundi la watawa wasaidizi aliowaona kama «Wasalesiani wa nje».
Yohane Bosco alifariki tarehe 31 Januari1888.
Papa Pius XI alimtangaza mwenye heri tarehe 2 Juni 1929 na mtakatifu tarehe 1 Aprili 1934. Sikukuu yake ni tarehe 31 Januari.
]]