Wasia wa Fransisko wa Asizi
Wasia wa Fransisko wa Asizi ni maandishi ambayo Fransisko wa Asizi aliwaachia wafuasi wake muda mfupi kabla ya kufariki dunia jioni ya tarehe 3 Oktoba 1226.
Huo wasia wa Kiroho ni mbinu mojawapo aliyotumia kuhakikisha hawatalegea. Pamoja na kwamba aliandika wasia zaidi ya mara moja, muhimu zaidi ni ule mrefu aliouandika katika wiki za mwisho za maisha yake. Haukukusudiwa kuwa kanuni mpya, ila kusaidia ile iliyoahidiwa kwa Bwana: ni kumbukumbu, onyo na shauri.
Kwanza ni kumbukumbu za uongofu wa Fransisko na za maisha asili ya shirika ambayo ndugu wote wafananishe nayo maisha yao. Katika kumbukumbu hizo hakutaja mateso yote aliyojaliwa na Mungu, bali alifafanua chaguo lake la kumfuata Yesu fukara kama utajiri pekee anaowaachia watoto wake. Hivyo wasia, ukiunganisha maagizo ya kanuni na mang’amuzi ya mwanzilishi, ukabaki katika shirika kama mwiba mwilini mwa wanaopenda kulegeza kamba, na kama changamoto kwa wote kadiri walivyompenda Fransisko, kwa kuwa ndiyo maneno yake ya mwisho aliyoyatoa kwa upendo mkuu akiwa amefanana na Yesu msulubiwa hata mwilini mwake. Ndiyo sababu toka mwanzo wasia ulisababisha shirikani mabishano yaliyohitaji kuingiliwa kati na Mapapa. Upande wa wasia walisimama ndugu waaminifu, ingawa kipindi fulani baadhi yao (Fraticelli) walipita kiasi hata kujitenga na Kanisa ili kupigania ufukara; baada yao kosa hilo halijarudiwa tena. Baadhi ya marekebisho ya shirika (k. mf. Wakapuchini) yalijifunga kushika wasia pamoja na kanuni, na hivyo wakafaulu kurudia maisha asili.
Pamoja na kumbukumbu, katika wasia tunakuta maonyo ya mwisho ya Fransisko kuhusu kuheshimu mapadri, kufanya kazi za mikono, kuishi kama wakimbizi katika nyumba duni, na kutoomba fadhili yoyote kutoka ofisi za Papa.
Polepole maonyo yakawa mashauri, na hasa shauri kuu lililo lengo la yote yaliyotangulia, kiasi kwamba ni katazo kali. Linahusu ujanja wa wanasheria katika kupotosha maana halisi ya maneno ya kanuni na wasia. Kuyaelewa kunahitaji unyofu uleule wa Fransisko pamoja na nia ya kuyatekeleza. Watakaofanya hivyo watapata baraka pana kabisa ya Mungu na ya kwake. Kivutio hicho kimejaa upendo wa mzee kwa watoto wake ambao ulijitokeza mara nyingi miaka ya mwisho katika maneno, maandishi na matendo.
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Wasia wa Fransisko wa Asizi kama historia yake, matokeo au athari zake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |