Nenda kwa yaliyomo

Sikomi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
“Sikomi”
“Sikomi” cover
Kasha la Sikomi
Single ya Diamond Platnumz
Imetolewa 5 Disemba, 2017
Muundo Upakuzi wa mtandaoni
Imerekodiwa 2017
Aina Bongo Flava
Urefu 4:02
Studio Wasafi Records
Mtunzi Diamond Platnumz
Mtayarishaji Laizer Classic
Mwenendo wa single za Diamond Platnumz
Hallelujah
(2017)
"Sikomi"
(2017)
"Waka"
(2017)

"Sikomi" ni wimbo uliotoka tarehe 5 Disemba, 2017 kwa msanii wa muziki wa kizazi kipya wa Tanzania, Diamond Platnumz. Wimbo ulitambulishwa kwa mara ya kwanza mnamo tarehe 27 Novemba 2017 ambapo alitoa nyimbo mbili kwa pamoja katika muundo wa audio kama utangulizi tu - wimbo mwingine ni "Niache". Alitaka watu wachague wimbo gani utoke rasmi mwanzo kati ya hizo mbili. Hatimaye ukatoka rasmi Sikomi na wimbo ulishika vibaya na ndio wimbo wa kwanza wa Diamond kufanya video na Zoom Production ambayo alionekana kuitanganza tangu 2017 kwenye akaunti yake ya Instagram. Mwongozaji wake ni Kenny. Huu ni wimbo wa tatu kutolewa na Zoom baada ya Dede ya Lavalava, ya pili kufanywa na Zoom ya Harmonize, "Nishachoka". Wimbo umetayarishwa na Laizer Classic kupitia studio ya Wasafi Records. Huu ni wimbo wa tatu wa Diamond Platnumz kuimba kwa huzuni sana baada ya Ntapata Wapi (2014) na Utanipenda (2015). Humu inaonekana kawaida sana kwa Diamond kuweka bayana maisha yake binafsi. Wimbo anazungumzia maisha yake ya mahusiano na wanawake mbalimbali, huku akielezea mikasa kadha wa kadha anayokubali kama mwanadamu ameyapitia licha ya kuwa na changamoto mbalimbali.

Maudhui[hariri | hariri chanzo]

Kwa ujumla wimbo unahusu mahusiano yake aliyowahi kuyapitia hadi kukutana na mama watoto wake Zarina Hassan au maarufu Zari the Boss Lady.

Ubeti wa kwanza[hariri | hariri chanzo]

Sampuli ya "Sikomi" ubeti wa kwanza, kiitikio na daraja.

Ubeti huu anazungumzia maajabu ya Muumba jinsi alivyotoka kiajabuajabu leo hii na yeye anawika kwa kupitia muziki. Mambo haya ya umaarufu alikuwa anayasikia kwenye vyombo vya habari tu, leo hii na yeye kawa miongoni mwa watu maarufu Tanzania. Halkadhalika kuwa na mahusiano na watu maarufu ilikuwa ndoto kubwa katika maisha yake. Ghafula, anadondokea mikoni mwa Wema Sepetu wa Bongo Movie.
"Niliposikiaga Habari,
Yakisifika nikakesha nangojea,
Akabariki Jalali na nikawika muziki nikauotea,
Ile pruuu mpaka Macca,
Nikadandiaga Bongo movie"

Mahusiano yao yalikuwa na mingi mikasa, magazetini kila siku na walikuwa vivuruge kwelikweli. Mara wameachana, mara wamerudiana. Mapenzi ya kuzima na kuwasha. Wema Sepetu ndiye mpenzi pekee wa Diamond aliyekuwa na mahusiano nae na kuachana, halafu kurudiana, halafu kuachana tena na kutiana fitna mbalimbali na hatimaye kuelewana na kubaki marafiki wa karibu kwa kushauriana mambo mbalimbali. Diamond ana kiri mambo mengi anamshauri Wema, hata suala la baadhi ya vitu katika pafyumu yake kuna mkono wa Wema.

Katika wimbo Wema kamtaja kama mwanamke machepele, aliyejaribu kujitia ujuzi wa mapenzi kwa mtu ambaye hahitaji ujuzi. Mistari inasema:

"Mwenzenu nikaoza haswa,
Na kujitia kitandani mjuzi,
Eti nataka fukuza paka,
Badala ya mbwa nikafuga mbuzi"

Kwa kuwa haya yalikuwa mapenzi yake ya kwanza kuwa na mtu maarufu, Diamond alijimwaga na kujitia mjuzi wa mapenzi ili asimwagwe. Umaarufu wa Wema ulikuwa mkubwa sana kiasi Diamond wivu ukawa moto. Hasikii la mwadhini wala mnadi swala, wivu ukatawala maisha yake. Rejea:


"Wivu ukanifanya nikagombana na marafiki,
Ugomvi na mamangu akiniambia siambiliki",

Halafu manenio anayorudia mara kwa mara baada ya kumaliza kisa cha kimepenzi cha mtu mmoja anasema:


"Moyo ukanambia Nasibu sasa mapenzi basi,
Ila nang'ang'ania najaribu kuipinga nafsi,
Esma ananiambia mdogo wangu mapenzi basi,
Ila nang'ang'ania,
Nikiumizwa na huyu kesho nna mwingine"

Ubeti wa pili[hariri | hariri chanzo]

Kwa ujumla wake, aliyeimbwa sana ni Wema. Inaonekana dhahiri mahaba ya Chibu kwa Wema ni makubwa na kamwe hayatofutika katika moyo wake. Halkadhalika mabaya ambayo Wema amemtenda Chibu kamwe hatoyasahau. Ubeti unaanza tena na Wema kwa kusema:


"Aliyonifanyia wa central,
Haki ya Mungu siyawezi sema,
Ila nimejifunza kesho nisiwaamini wacheza sinema,
Moyo walinipatia mateso,
Siwezi kumeza siwezi tema"


Hajaishia hapo, anarudia tena kuelezea jambo la Wema la kutoka CCM kwenda CHADEMA baada ya ile kashfa ya bangi na kuburuzwa mahakamani kwa hila.[1][2][3]


"Ndio maana sikushanga ile ghafla Toka CCM kwenda CHADEMA"


Bado anasononekea penzi la mara ya pili. Kajikaza na madhila yote ya Wema, kwani ndio keshapenda. Kupenda ni upofu, kaingia tena mzima, lakini yaliyomkuta tena ni makubwa. Hakuwa na budi kuyavumilia lakini je, nani kuweza kuvumilia maumivu hayo muda wote.


Anatoka kwa Wema anaenda kwa Hamisa Mobeto aliyezaa nae mtoto Abdul. Mobeto ameonekana kutembelea nyota ya Zari kwa hali na mali. Anapigania mkate wa mtoto wake kwa nguvu za ajabu. Hadi kupelekana mahakamani ili kudai fedha za kujikimu za matumizi ya mtoto.[4] Hamisa alimfanya mtoto wake mtaji wa kutokea kimaisha. Hata hivyo kesi iliisha na Diamond alisema hawezi kulipa milioni 5 za matumizi ya mtoto kwa mwezi. Hatimaye mahakama ikatupilia mbali ombi hilo.[5]


Baada ya mkasa huo mkubwa uliowahi-kumtokea Chibu, anarudia sasa tukio lile katika mistari hiyo:

"Wanasema kitanda ukitandika sharti ukilalie,
Nikajitia ukamanda yatakwisha,
Wacha nivumilie,
Kila kiza kikitanda,
Ndo visa machozi me nilie,
Penzi yakatia parapanda,
Kuwaita waje washambulie"

Hakuishia hapo, anakumbuka uhusiano wake wa mwendokasi na Penny mtangazaji wa DTV.[6] Chibu anaonekana mwepesi sana kuzama katika madimbwi la mapenzi. Vilevile mikosi ya kutendwa pindi tu anapoonesha nia ya kupenda zaidi. Penny alijifanya ana mimba, kumbe danganya toto. Haijulikani nini hasa kiliwaachanisha wawili hawa. Labda suala hili au mashauzi ya Penny yalimshinda Chibu. Chibu kamgusia kidogo tu, Penny. Tazama mstari huu:
"Acha na penny we darling,
Nilio muhongaga gari aliponambia ana mimba,
Mwisho wa siku akaichomoa chaliiiii"

Kitu pekee anacho Chibu tofauti na wasanii wengine ni kumwa mwazi kwa maisha yake binafsi. Kukubali kama kakosa hadharani hasa kwa wale anaowapenda. Katika wimbo anaumizwa na kusikitishwa na tendo la kumsaliti Zari. Tena amekiri dhahiri kwenye vyombo vya habari kupitia kipindi cha Leo Tena cha Clouds Media Group mnamo mwezi Septemba, 2017 alikiri kuwa mtoto wa Hamisa Abdulatif ni wake.[7][8] Rejea mistari hiyo:

"Mola akanitunuku Zari,
Akanzalia dume na mwali,
Niliyvo mjinga nikacheat aibu mpaka,
Kwa vyombo vya habari"

Katika mahojiano hayo, Chibu alifunguka kupita maelezo. Alionesha hisia zake za dhati kwa Zarina Hassan. Haijaisadia kitu, Zari alionekana kuchukizwa sana na jambo hilo. Tangu hapo, Zari amekuwa mtu wa maneno mengi sana ya vijembe mitandaoni.[9] Zari aliandika hivi kwenye akaunti yake ya Instagram:

"Hahahaha unajidanganya, unasema uongo kuhusu mimi kujua kuhusu michepuko yako, malizana na balaa ulilolianzisha. Mimi kunyamaza haimaanishi ni mpumbavu. Kuwa makini na maneno yako."

Na ilivyofika tarehe 14 Februari, 2018 - siku ya wapendanao, Zari alituma posti katika ukurasa wake wa Instagram wa kuachana na Diamond rasmi. Aliweka posti yenye uwa jeusi badala ya jekundu. Alielezea masikitiko na maumivu yake yote moyoni.[10]

Katika wapenzi wake, huyu Mobeto alionekana kuweka siri sana tangu walipoanza ote kuhusiana katika miaka ya 2009-2010. Hadi hii mara ya pili walipozaa kabisa ndipo hasa anatoa habari kamili ya mahusiano yao ambayo waliyazima na kuyawasha. Ilivyofika tarehe 8 Februari, walirudi tena mahakama ya Kisutu, Dar, na kuyamaliza kikubwa. Katika mahojiano yake Diamond alionesha hali halisi ya kwamba upande wa Mobeto kuna watu walikuwa wanatia chumvi mambo ili yawe makubwa zaidi. Alienda mbali zaidi kwa kusema mtoto ana mahitaji mengi na si kuwekeana viasi fulani vya matumizi ya mtoto. Dhahiri maelewano yalipata.[11]

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

 1. Wema Sepetu ahamia Chadema Gazeti la Mwananchi THURSDAY, FEBRUARY 23, 2017
 2. Wema ahamia CDM Archived 27 Februari 2017 at the Wayback Machine. wavuti ya Swahili Times 23 Feb, 17
 3. PICHAWema Sepetu ahamia Chadema, aungana na Mbowe mahakamani Bongo5 23 Feb, 17.
 4. Diamond afikishwa mahakamani kwa matunzo ya mtoto Gazeti la Mwananchi Oktoba 5, 2017.
 5. MAHAKAMA YAFUTA KESI YA DIAMOND, HAMISA MOBETO Archived 16 Desemba 2017 at the Wayback Machine. wavuti ya Magazetini Novemba 11, 17.
 6. DIAMOND NDANI YA PENZI ZITO LA VJ ENNY WA DTV blogu ya Afrokija, 24 Januari, 2013.
 7. http://bongo5.com/diamond-akiri-mtoto-wa-hamisa-mobeto-ni-wa-kwake-09-2017/ Diamond akiri mtoto wa Hamisa Mobeto ni wa kwake] wavuti ya Bongo5 Septemba 19, 2017.
 8. Diamond akiri kuzaa na Hamisa Mobeto Archived 25 Januari 2018 at the Wayback Machine. blogu ya Ghafla Septemba 19, 2017.
 9. Zari ageuka Mbogo,kisa diamond kuzaa na Hamisa Mobetto Archived 17 Machi 2018 at the Wayback Machine. blogu ya Togoro Media
 10. ARI : NIMEACHANA KABISA NA DIAMOND VITENDO VYAKE NA MA X WAKE VIMENIFANYA NIDHALILIKE Archived 24 Februari 2018 at the Wayback Machine. wavuti ya Tanzania-Today 23-Feb-2018 - chanzo kutoka BBC.
 11. Alichozungumza Diamond Platnumz baada ya Kesi yake na Hamisa katika idhaa ya Millard Ayo - YouTube mnamo tarehe 08 Feb, 2018..

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]