Nenda kwa yaliyomo

Dk. Omar Ali Juma

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Omar Ali Juma)

Dk. Omar Ali Juma (26 Juni 19414 Julai 2001) alikuwa Makamu wa Rais wa serikali ya awamu ya tatu nchini Tanzania, iliyokuwa inaongozwa na Rais Benjamin William Mkapa.

Wasifu[hariri | hariri chanzo]

Dk. Omar alizaliwa tarehe 26 Juni 1941 katika kijiji cha Wawi, Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Pemba Kusini.

Elimu yake ya msingi aliipata tangu mwaka 1949 mpaka mwaka 1957 katika Shule ya Msingi ya wavulana ya Chake, ambayo kwa sasa inajulikana kama Shule ya Msingi Michakaini.

Elimu ya sekondari aliipata tangu mwaka 1957 hadi 1960 katika Shule ya Sekondari ya Euan Smith Madressa, ambayo nayo hivi sasa imebadilishwa jina na kuitwa Shule ya Sekondari ya Haile Selassie.

Kuhusu elimu ya juu aliipatia kwenye vyuo mbalimbali vilivyomo nchini Tanzania na nje. Alianza kusoma katika Chuo Kikuu cha Moscow State, ambako alimaliza mwaka 1967 na pia mwaka 1969 alimaliza katika Chuo Kikuu cha Cairo, Misri.

Pia alisoma Chuo Kikuu cha Edimburgh ambapo napo alimaliza masomo yake mwaka 1977, akapata nafasi tena ya kwenda kusoma Chuo Kikuu cha Florida, Marekani na alimaliza mwaka 1980.

Dk. Omar aliendelea na masomo yake na mwaka 1982 alikuwa mmoja wa wahitimu katika Chuo Kikuu cha Reading, Uingereza na pia kiongozi huyo alipata fursa ya kwenda kusoma katika Chuo cha Kivukoni Ideological mwaka 1982.

Shughuli za kiserikali[hariri | hariri chanzo]

Dk. Omar Ali Juma alikuwa mfanyakazi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tangu mwaka 1967 hadi mwaka 1984 ambapo alihamishiwa katika serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1995 hadi alipofariki dunia.

Alipokuwa mfanyakazi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) alishika nyadhifa nyingi kubwa.

Mwaka 1967 - 1969 alikuwa Ofisa Wanyama Msaidizi, mwaka 1969 - 1970 alikuwa Ofisa Wanyama na mwaka 1970 hadi 1971 alikuwa Ofisa Wanyama Mwandamizi.

Mwaka 1971 -1972 alikuwa Ofisa Mifugo, halafu alikuwa Ofisa Mkuu wa Mifugo katika miaka ya 1972-1978.

Miaka 1978-1984, alifanikiwa kushika wadhifa wa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mifugo, mwaka 1984-1987 alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, Zanzibar, na Januari 1988 - 1995, alikuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]

Alitanguliwa na
Cleopa David Msuya
Makamu wa Rais wa Tanzania
1995-2001
Akafuatiwa na
Ali Mohamed Shein