Mars (mungu)
Ukitafuta sayari inayoitwa Mars kwa lugha ya Kiingereza tazama Mirihi
Mars (kutoka Kilatini Mars) alikuwa mungu wa vita katika dini ya Roma ya Kale[1]. Kwa asili aliabudiwa pia kama mungu wa kilimo. [2] Alitazamwa kama mwana wa Jupiter na Juno. Aliheshimiwa kushinda miungu mingine iliyoabudiwa wakati wa vita na katika jeshi la Kiroma. Sikukuu zake nyingi zilifanyika mnamo mwezi wa tatu na mwezi huo ulipewa jina lake, kwa Kilatini Martius. Jinsi ilivyo Machi ilikuwa mwezi wa kuandaa mashamba katika mazingira ya Italia; alikuwa pia na sikukuu mnamo Oktoba, ambako mavuno yalikwisha na msimu wa kampeni za kijeshi ulianza.
Chini ya ushawishi wa utamaduni wa Kigiriki, Mars alitambuliwa kuwa sawa na Ares, mungu wa vita wa Kigiriki[3]. Visasili vya Ares vilitafsiriwa upya katika fasihi ya Kirumi vikisimuliwa kwa jina la Mars.
Madhabahu kuu ya Mars ilipatikana kwenye Campus Martius, eneo kubwa ndani ya jiji la Roma ambalo lilichukua jina lake kutoka kwa Mars likitumiwa kwa mikutano ya hadhara. Baadaye Kaizari Augusto alijenga hekalu kwake kwenye uwanja wa forum yake.[4]
Mars alitazamwa kama nguvu iliyohakikisha amani na usalama wa taifa kwa njia ya nguvu ya kijeshi. Hivyo aliheshimiwa kama Baba wa Taifa.[5] Katika visasili vya Kiroma Mars alikuwa mpenzi wa mungu wa kike Venus. Alitazamwa pia kama baba mzazi wa Romulus na Remus, waanzilishi wa mji wa Roma.
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Chapter 3, Charles E. Bennett (1907) The Latin Language – a historical outline of its sounds, inflections, and syntax.
- ↑ Mary Beard, J.A. North, and S.R.F. Price, Religions of Rome: A History (Cambridge University Press, 1998), pp. 47–48.
- ↑ Larousse Desk Reference Encyclopedia, The Book People, Haydock, 1995, p. 215.
- ↑ Paul Rehak and John G. Younger, Imperium and Cosmos: Augustus and the Northern Campus Martius (University of Wisconsin Press, 2006), pp. 11–12.
- ↑ Isidore of Seville calls Mars Romanae gentis auctorem, the originator or founder of the Roman people as a gens (Etymologiae 5.33.5).
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- Fowler, William Warde (1911). "Mars (deity)". In Chisholm, Hugh. Encyclopædia Britannica. 17 (11th ed.). Cambridge University Press. pp. 760–761.
- c. 700 images of Mars Ilihifadhiwa 2 Juni 2013 kwenye Wayback Machine. at the Warburg Institute Iconographic Database