Nenda kwa yaliyomo

Mpagazi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Mahamali)

Kwa matumizi mengine ya jina Hamali angalia hapa Hamali (kundinyota)

Msafara wa wapagazi wanaobeba vifaa na vyakula kwa kambi la kuchimbua mifupa ya dinosauri pale Tendaguru, Lindi, Tanzania. Picha ilichukuliwa na kiongozi wa msafara Walter Janensch kati ya miaka 1909 na 1912.
Chifu Kaware safarini akibebwa na wapagazi, Rwanda mnamo mwaka 1900.
Hamali wa kabila la Sherpa akibeba ubao katika milima ya Himalaya karibu na Mount Everest.

Mpagazi (pia: mchukuzi, hamali, kuli) ni mtu anayembebea mtu mwingine mizigo yake.

Mahamali kihistoria

[hariri | hariri chanzo]

Katika historia ya binadamu watu, yaani wapagazi, walitumika kusafirisha mizigo kwa muda mrefu. Katika Asia, Ulaya na Afrika ya Kaskazini walipatikana wanyama walioweza kufanya kazi hii kama vile farasi, punda, ng'ombe au ngamia. Lakini katika sehemu kubwa ya Afrika na pia Amerika utamaduni asilia ulitegemea nguvu ya wapagazi wa kibinadamu. Pia katika maeneo yenye milima mikali au misitu minene yenye matope wanyama wa kubebea mizigo walishindwa, hivyo mizigo ilitegemea nguvu ya binadamu.

Katika Afrika kusini kwa Sahara biashara ya misafara ilitegemea hasa wapagazi.

Wapagazi siku hizi

[hariri | hariri chanzo]

Siku hizi wapagazi wanapatikana kwenye vituo vya usafiri vyenye watu wengi kama vile kituo cha reli, cha mabasi au uwanja wa ndege. Kuna pia mahamali wanaosaidia wateja kwenye masoko makubwa.

Katika nchi zilizoendelea sana mahamali karibu wamepotea kwa sababu gharama ya maisha imesababisha kupanda kwa mishahara hadi watu wamependelea kubeba mizigo yao wenyewe. Katika nchi kama hizo mikokoteni ya mzigo iko tayari kila mahali ichukuliwe na wateja au wasafiri kwa hiari yao.

Wapagazi kwenye safari za milimani

[hariri | hariri chanzo]

Hadi leo kuna wapagazi katika maeneo yasiyo na barabara hasa mlimani. Wasafiri, wapelelezi, wanasayansi au watalii hupaswa kuwakodisha wakitaka kusafiri katika mazingira hayo.

Watu wanaopanda Mlima Kilimanjaro hupaswa kuwa na mwenyeji atakayewaongoza lakini kwa kawaida wanakwenda pia na hamali anayewabebea mzigo. Sababu kuu ni kwamba mtu asiye mwenyeji hukosa nguvu za kubeba mizigo katika kimo kikubwa kwa kuwa hajazoea wala kimo wala hewa, hivyo humhitaji mwenyeji. Mtu anayeishi kwenye kimo cha juu anazoea kupumua hewa yenye kiwango kidogo zaidi cha oksijeni.

Watu wanaotoka kwenye maeneo mengine ya dunia wanahitaji muda wa wiki kadhaa au hata miezi mpaka mwili uwe umezoea hali hiyo.

Katika milima ya Himalaya, ambayo ni mirefu kushinda Kilimanjaro, wapagazi wenyeji ni wa lazima kabisa. Mara nyingi huitwa kwa jina la "sherpa" ambalo kiasili ni jina la kabila fulani lakini siku hizi neno latumiwa pia kwa maana ya "mpagazi" au "hamali".

Makala hii kuhusu mambo ya utamaduni bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mpagazi kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.