Koloni nyakati za kale
Makala hii inaangalia matumizi ya neno "koloni" katika mazingira ya Mediteranea katika nyakati za kale
Koloni lilikuwa njia ya kueneza utawala wa nchi au taifa tangu enzi ya Wagiriki na Waroma wa kale.
Asili ya neno "koloni"
[hariri | hariri chanzo]Asili ya neno koloni ni katika lile la Kilatini "colonia" linalotokana na kitenzi "colere" (kulima, pia kuabudu). Colonia ilikuwa makazi ya Waroma wa Kale nje ya eneo lao la awali. Chanzo chake kilikuwa mji mpya uliokaliwa na wanajeshi wastaafu waliopewa ardhi ya shamba kama pensheni yao. Makoloni ya aina hiyo yalianzishwa hasa mpakani mwa maeneo mapya yaliyotwaliwa karibuni na kuingizwa katika Dola la Roma. Walowezi walipewa mashamba yao kwa masharti ya kuwa tayari kutetea mipaka kama vita ikitokea.
Koloni nyakati za kale
[hariri | hariri chanzo]Hata kama neno "koloni" lilitokana na lugha ya Kilatini, Waroma wa Kale hawakuwa watu wa kwanza waliounda makoloni, bali walifuata nyayo za mataifa yaliyotangulia kama Wagiriki wa Kale au Wafinisia.
Miji ya Wagiriki au Wafinisia ilikuwa miji ya biashara kando ya bahari. Walianzisha makoloni mapya hasa wakati idadi ya watu katika mji mama iliongezeka mno kulingana na eneo la mji huo. Badala ya kutwaa maeneo ya jirani walitafuta mahali papya ufukoni kwa bahari pasipo wakazi wengi nje ya eneo lao kwa sababu usafiri kwa jahazi ulikuwa rahisi kuliko kujenga barabara barani.
Hivyo Wagiriki waliunda miji mipya katika Italia ya kusini au kwenye pwani za Bahari Nyeusi. Miji mingi ya Italia ya kusini na ya kati inaonyesha hadi leo jina lenye asili ya Kigiriki kwa mfano Napoli iliyokuwa "Νεάπολις" (nea polis = mji mpya) au Ancona iliyokuwa "Ἀγκών" (ankon = bandari)
Wafinisia waliunda miji mipya hasa katika Afrika ya Kaskazini na Hispania. Koloni-mji mashuhuri zaidi la Wafinisia lilikuwa Karthago.
Makoloni-miji ya Waroma wa Kale
[hariri | hariri chanzo]"Colonia" za aina hiyo zilianzishwa na Waroma wa kale katika maeneo yaliyotwaliwa nao karibuni kwa shabaha ya kurahisisha usimamizi wa maeneo mapya. Wanajeshi wastaafu walipewa ardhi kama shukrani kwa huduma yao pamoja na masharti ya kwamba watakuwa tayari kutetea eneo kama vita ikitokea tena.
Makoloni ya aina hiyo ziliundwa awali ndani ya Italia wakati wa upanuzi wa utawala wa mji wa Roma juu ya rasi yote. Baadaye makoloni yalianzishwa pia nje ya Italia kwa mfano Gallia, Germania, Britania, Uyahudi au Afrika ya Kaskazini.
Miji kadhaa ya kisasa iliyoundwa na Waroma inatunza neno la Kilatini "colonia" hadi leo ndani ya umbo la majina yake:
- Köln nchini Ujerumani ilianzishwa kama "Colonia Ara Agrippensis" na jina lake la leo ni badiliko la neno "colonia".
- Colchester katika Uingereza ulikuwa na jina la Kiroma la "Colonia Claudia Victricensis". Silabi ya kwanza ni baki la neno la Kiroma.
- Lincoln katika Uingereza iliitwa "Lindum Colonia" na jina la leo ni namna ya kufupisha jina la kale.