Isfahan
Nchi | Iran |
Jimbo / Mkoa | Isfahan |
Manisipaa | Isfahan |
Anwani ya kijiografia | 32.644722, 51.6675 |
Kimo | m 1,574 |
Eneo | km2 551 |
Wakazi | 3,989,070[1] |
Simu | 031 |
Tovuti rasmi | www.isfahan.ir |
Isfahan au Esfahān (matamshi ya Kiajemi ya اصفهان) ni jiji katika nchi ya Iran. Iko takriban km 340 upande wa kusini wa Tehran.
Idadi ya wakazi wa mji wenyewe ni mnamo milioni 2, pamoja na mapambizo ni takriban milioni 4, hivyo ni mji mkubwa wa tatu nchini baada ya Tehran na Mashhad.
Jiografia
[hariri | hariri chanzo]Isfahan iko katika kitovu cha Iran kwenye kimo cha mita 1500 katika bonde la mto Zayandeh Rud. Bonde hilo lilikuwa na rutuba kubwa kwa karne nyingi lakini miradi mikubwa ya umwagiliaji imetoa maji mtoni na katika miezi sita ya kwanza ya mwaka 2018 mto ndani ya jiji ulikauka kabisa.
Upande wa Kusini wa Isfahan kuna milima ya Zagros, upande wa kaskazini na mashariki ziko nyanda za juu za Iran zinazoendelea katika majangwa makubwa.
Historia
[hariri | hariri chanzo]Isfahan ilianzishwa takriban miaka 2,500 iliyopita kutokana na miji na makazi mbalimbali kando ya Mto Zayandeh Rud.
Jina linatokana na neno la Kiajemi "aspahan"au "ispahan" linalomaanisha mahali pa jeshi na jina hili limeshuhudiwa na Klaudio Ptolemaio katika kitabu chake juu ya historia [2]
Kando yake kulikuwa na mji wa Kiyahudi ulioitwa "Yahudiyya" na waandishi Waarabu wa karne za kati. Wayahudi wa mji huo wanatunza kumbukumbu kuwa mwaka 538 KK baada ya ushindi wa mfalme Koreshi I juu ya Babeli, Wayahudi waliokuwa uhamishoni waliruhusiwa kurudi, lakini wengine walipendelea kuhamia Uajemi walipojenga makazi kando ya Zayandeh Rud. Kuna pia kumbukumbu kwamba mke Myahudi wa mfalme Yazdegerd I (399–420 BK) alijenga makazi kwa walowezi Wayahudi katika eneo la Isfahan.
Wakati wa uvamizi wa Waarabu Waislamu hao mabwana wapya walifanya mji kuwa makao makuu ya jimbo la Iran ya Kati lililoendelea kuwa chini ya khalifa kwenye mji wa Baghdad. Wakati mamlaka ya ukhalifa wa Waabbasi ilianza kufifia katika karne ya 10, magavana wa Isfahan kutoka nasaba ya Kiajemi ya Buwayhidi walianza kutawala maeneo makubwa kutoka mji wao na kuupamba kwa majengo mazuri. Katika karne ya 11 Waturuki Waseljuki walivamia Iran na hao pia walitawala kwa muda kutoka Isfahan. Baada ya kuporomoka kwa mamlaka yao Isfahan ilirudi nyuma, haikuwa tena mji mkubwa wa nchi.
Katika karne ya 16 mji uliona kipindi kipya cha kustawi; Shah Abbas I alihamisha mji mkuu wake kutoka Qazvin kwenda Isfahan na chini ya utawala wake iliendelea kuwa mmoja ya miji mikubwa na mizuri duniani. Majengo mengi ya enzi yake yanasimama hadi leo, pamoja na Uwanja wa Naqsh-e Jahan, misikiti mizuri na jumba la kifalme, pia madaraja mazuri juu ya mto Zayandeh Rud. Hizo ni sababu ya Isfahan kuwa mahali pa urithi wa Dunia katika orodha ya UNESCO.
Shah Abbas aliunda pia mtaa wa Kikristo katika mji wake kwa kuhamisha Waarmenia kutoka mji wa Jolfa kuja Isfahan katika sehemu ya "Jolfa Jipya" walipoweza kujenga makanisa yao na kuendesha biashara.
Utajiri wa Isfahan ulikwisha baada ya kushambuliwa na kuchomwa na Waafghani mwaka 1722, haukuwa tena mji mkuu.
Ni katika karne ya 20 tu kwamba uchumi na idadi ya watu vilianza kuinuka tena.
Uchumi
[hariri | hariri chanzo]Leo hii Isfahan ni mji wa viwanda, biashara na utalii. Kuna viwanda vya vyakula, feleji, vya kusafisha mafuta, vya vitambaa na nguo. Utalii unalisha mafundi wengi wanaozalisha bidhaa kwa wageni. Kuna taasisi za utafiti wa nishati ya kinyuklia na kiwanda cha fueli ya nyuklia.
Kuna Uwanja wa ndege na reli ya metro iliyokamilika kilomita 11 chini ya ardhi.
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ "Major Agglomerations of the World - Population Statistics and Maps" tovuti ya citypopulation.de, 13 Septemba 2018
- ↑ J. Hansman and EIr Isfahan IV pre-islamic period, tovuti ya Encyclopedia Iranica online, December 15, 2006, update March 30, 2012)
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]Makala hii kuhusu maeneo ya Asia bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Isfahan kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |