Nenda kwa yaliyomo

Malkia Cixi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Dowager Cixi)
Malkia Cixi wa China

Malkia Cixi wa China (29 Novemba 183515 Novemba 1908) alikuwa mwanamke Mchina aliyeshika utawala wa China kwa miaka mingi wakati wa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20. Cheo chake rasmi kilikuwa "mjane wa kaisari" (mjane wa kifalme) akatawala kwa kushika mamlaka kwa niaba ya Kaisari wa nasaba ya Qing aliyekuwa mdogo mno. Katika mapokeo ya China ya Kale mama wa mtoto wa kifalme aliyerithi cheo cha baba alitawala kwa niaba ya mtoto kwa muda baada ya kifo cha Kaisari kama mtoto alikuwa bado mdogo.

Cixi aliingia katika ikulu ya kaisari wa China kama suria au mke mdogo wa Kaisari Xianfeng. Kila kaisari alioa wake 14: malkia mmoja, wake wawili na wake wadogo 11. Cixi aliteuliwa mwaka 1855 pamoja na mabinti 60 walioangaliwa kama mahawara akateuliwa kuwa mmoja wa wake wadogo 11 wa kaisari mpya.

Mwaka 1856 alimzaa mtoto wa kiume. Mwaka 1861 nyumba ya kifalme ilipaswa kukimbia Beijing wakati wa vita ya afyuni dhidi ya Uingereza. Alipokaa nje ya mji mkuu Kaisari aliugua na saa chache kabla ya kifo chake alimteua mtoto wa Cixi kama mrithi wake na mjane wake wa kwanza yaani malkia pamoja na Cixi walipewa cheo cha "wajane wa Kaisari" walioshika kwa pamoja nembo ya Kaisari lililopaswa kuonekana chini ya kila sheria au amri ya kifalme. Hali halisi serikali yenyewe ilikuwa mkononi mwa halmashauri ya mawaziri; lakini hao waligombana kati yao mara kwa mara na hivyo kumpa mjane wa kaisari nafasi kubwa.

Baada ya kifo cha mjane mwenzake Cixi alibaki peke yake katika nafasi hii muhimu hadi mtoto kuwa mkubwa mwaka 1872. Katika kipindi hicho uwezo wake wa kisiasa ulikuzwa akafaulu kuwaondoa madarakani mawaziri waliompinga hata kutamka adhabu ya kifo juu ya mpinzani kwa kumshtaki kama msaliti.

Kaisari mpya alikufa mapema mwaka 1875 kabla hajamzaa mrithi. Hivyo mpwa mdogo wa Cixi aliteuliwa kuwa kaisari mpya Guangxu. Cixi alichukua tena nafasi ya mjane wa Kaisari kwa niaba ya mtoto huyo hadi mwaka 1889.

Mwaka 1898 katika kipindi kigumu cha siasa alimpindua Kaisari Guangxu akamfunga ndani ya jumba la kifalme akachukua utawala moja kwa moja hadi kifo chake mwaka 1908. Kabla ya kifo chake alimteua mtoto Pu Yi kama Kaisari mpya lakini mapinduzi ya China ya 1911 yalimaliza ufalme wa China na kutangaza jamhuri.

Ci-Xi alipokuwa bado mke mdogo wa Kaisari.

Viungo vya Nje

[hariri | hariri chanzo]
Wikiquote ina mkusanyiko wa dondoo kuhusu:
Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Malkia Cixi kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.