Nenda kwa yaliyomo

Dinosauri

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Dinosau)
Dinosauri

Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Chordata (Wanyama wenye ugwe wa neva mgongoni)
Ngeli: Sauropsida (Wanyama wanaofanana na watambaazi)
Nusungeli: Diapsida (Wanyama wenya mashimo mawili kando la fuyu la kichwa)
Oda ya juu: Dinosauria (Wanyama kama dinosauri)
Ngazi za chini

2 Orders:

  • Ornithischia
  • Saurischia

Dinosauri (pia: dinosau, dinosari, dinosaria kutoka maneno ya Kigiriki δεινός, deinos – "wa kutisha", σαῦρος, sauros - "mjusi") ni jina la kundi la reptilia wakubwa sana walioishi duniani miaka milioni kadhaa iliyopita.

Kulinganisha ukubwa wa tiranosauri na binadamu.

Wataalamu huamini ya kwamba dinosauri walitokea miaka milioni 230 iliyopita wakatoweka ghafla miaka 65 iliyopita. Ndege hutazamwa kuwa katika nasaba ya dinosauri.

Ujuzi kuhusu wanyama hao unatokana na visukuku vyao (mabaki ambayo yamekuwa mawe) kama vile mifupa, nyayo, mayai au samadi. Visukuku vya dinosau vimepatikana kwenye mabara yote, hata Antaktika, kwa sababu waliishi wakati mabara yote yalikuwa bado pamoja kama bara kubwa asilia la Pangaia.

Spishi zao

Hadi sasa spishi 500 zimegundulika na idadi ya spishi zilizotambuliwa inazidi kuongezeka.

Kutokana na meno yao imewezekana kutambua chakula chao, kwamba wengine walikuwa wala majani, wengine walanyama.

Wale wakubwa sana walikula majani kama vile apatosauri na brakiosauri na hao walikuwa ndio viumbehai wakubwa kabisa waliowahi kutembea duniani.

Walanyama walikimbia kwa miguu miwili ya nyuma jinsi wanavyofanya watu lakini pia mijusi kadhaa wa leo.

Kulikuwa pia na reptilia wakubwa walioruka hewani walioitwa pterosauri, lakini kinasaba hawakuwa karibu sana na dinosauri.

Wengine wakubwa waliishi baharini kama ikhtiosauri na plesiosauri; hata hao walikuwa kundi lingine.

Kuangamia kwa dinosauri

Kuwepo kwa dinosauri kumejulikana kutokana na visukuku vyao, yaani mifupa na mabaki mengine yaliyopatikana kwenye sehemu nyingi za Dunia. Katika Tanzania ni hasa maeneo ya Tendaguru (Lindi) ambako viunzi mifupa kamili vilipatikana.

Kupatikana kwa mabaki haya katika matabaka maalumu chini ya ardhi kuliwezezesha wataalamu kukadiria umri wa visukuku hivyo. Kumbukumbu ya visukuku vya dinaosauri ni kunzia takriban miaka milioni 230 iliyopita[1].

Baada ya wakati wa miaka milioni 66 iliyopita hakuna visukuku vya dinosauri tena. Isipokuwa ilitambuliwa kuwa ndege wa siku hizi ni viumbe vya nasaba moja na dinosauri. Hapa wataalamu hukubaliana kuwa kulikuwa na mabadiliko yaliyosababisha kufa kwa dinosauri karibu wote kote duniani katika muda mfupi[2].

Wataalamu walishangaa muda mrefu kuhusu sababu zinazoweza kutajwa kwa kutoweka kwa ghafla kwa dinosauri. Siku hizi wengi wanakubaliana kuwa kupigwa kwa Dunia na asteroidi kubwa (pale Chixculub, Meksiko), pamoja na kuleta milipuko ya volkeno iliyosababishwa na mshtuko huu, kulileta mabadiliko ya ghafla ya tabianchi na hasa kupoa kwa halijoto kote duniani yaliyosababisha kufa kwa viumbehai wengi pamoja na dinosauri wote wakubwa[3]. Mababu ya ndege pekee waliokuwa dinosauri wadogo waliweza kuendelea.

Picha

Picha zifuatazo zinaonyesha kwanza visukuku vya kweli vya dinosau halafu uchoraji au sanamu zinazoonyesha jinsi gani wataalamu wanadhani mnyama alionekana.

Tanbihi

  1. When did dinosaurs live?, tovuti ya Natural Hstory Museum, London-Uingereza, makala ya 2012 iliyosahihishwa 2018
  2. Paleobiogeography and biodiversity of Late Maastrichtian dinosaurs: how many dinosaur species went extinct at the Cretaceous-Tertiary boundary?, makala kwenye geoscienceworld.org ya December 01, 2012
  3. Baby, it's cold outside: Climate model simulations of the effects of the asteroid impact at the end of the Cretaceous Archived 23 Aprili 2019 at the Wayback Machine., makala ya Geophysical Research Letters, tovuti ya AGU100 (Advancing Earth and Space Science) ya 20 December 2016

Viungo vya nje

Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Makala hii kuhusu mnyama fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Dinosauri kama uainishaji wake wa kibiolojia, maisha au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.