Nenda kwa yaliyomo

Kristoforo Kolumbus

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Christopher Columbus)
Kristoforo Kolumbus
Jahazi ya Santa Maria imejengwa tena kwa mfano wa jahazi ya Kolumbus miaka 500 iliyopita
Msanii alichora picha hii mwaka 1893 akitaka kumwonyesha Kolumbus jinsi alivyofika Amerika mwaka 1492
Ramani ya safari nne za Kolumbus

Kristoforo Kolumbus (kwa Kiitalia: Cristoforo Colombo; kwa Kihispania: Cristóbal Colón; kwa Kilatini: Columbus; Genova, Italia, 1451; Valladolid, Hispania, 20 Mei 1506) alikuwa mfanyabiashara na mpelelezi aliyegundua njia ya usafiri kati ya Ulaya na Amerika.

Mara nyingi aliitwa Mzungu wa kwanza wa kufika Amerika, lakini baadaye imejulikana ya kwamba Waviking walitangulia kufika Amerika ya Kaskazini mnamo mwaka 1000. Ila jitihada zake zilianzisha njia ya mawasiliano ya kudumu kati ya Amerika na mabara mengine tofauti na safari zote zilizovuka bahari kabla yake.

Upande wa dini, alikuwa Mkristo wa Kanisa Katoliki, tena mwanachama wa Utawa wa Tatu wa Mt. Fransisko.

Mipango ya Kolumbus

[hariri | hariri chanzo]

Nia ya Kolumbus ilikuwa kugundua njia ya kufika Uhindi kwa kuelekea magharibi. Sababu yake ilikuwa hali ya siasa ya wakati wake: njia zote za mawasiliano kati ya Ulaya na Uhindi zilitawaliwa na Waislamu. Bei za bidhaa zote zilizofika Ulaya kutoka Uhindi zilikuwa ghali sana kwa sababu ya vituo vingi vya biashara kati ya Uhindi na Ulaya.

Kolumbus alitaka kufika Uhindi kwa meli bila kupitia maeneo ya Waislamu upande wa mashariki. Alitaka kufanya majaribio: kama dunia ilikuwa kweli tufe ya mviringo -jinsi walivyoanza kufundisha wataalamu- ni lazima kuwe na njia kufika mashariki kwa kuelekea magharibi. Alijua taarifa ya msafiri Marco Polo aliyewahi kufika Uchina akaona bahari kubwa upande wa mashariki. Kolumbus aliamini ya kwamba bahari ile ingekuwa ileile ya Atlantiki inayoanza upande wa magharibi ya Ulaya. Hakutegemea ya kwamba angekuta nchi mpya kabisa kati ya Ulaya na Uhindi.

Nchi hii mpya ilikuwa bahati yake. Katika mipango yake alifanya kosa la kukadiria umbali kati ya Ulaya na Asia kuwa mdogo mno. Akiba za chakula na maji katika jahazi zake zisingetosha kufika Uchina. Kukuta nchi mpya njiani ambayo hakutegemea kulimwokoa.

Safari ya mwaka 1492

[hariri | hariri chanzo]

Kolumbus aliondoka Hispania kwa jahazi tatu tarehe 3 Agosti 1492. Tarehe 12 Oktoba 1492 alikanyaga mara ya kwanza eneo la Amerika katika kisiwa kimoja kisichojulikana ni kipi kwa hakika katika funguvisiwa ya Bahama. Akaendelea hadi Kuba na kisiwa cha Dominica akarudi Hispania mwaka 1493.

Alipofika kwenye visiwa vya Karibi katika Amerika ya Kati aliamini ya kwamba hivi vilikuwa visiwa vya Kihindi. Akaviita "Uhindi wa Magharibi" na wakazi kwa lugha ya Kihispania "Indio" yaani Wahindi. Hadi kifo chake hakutaka kukubali ya kwamba nchi hii haikuwa Uhindi wala sehemu yoyote ya Asia ila kitu kipya.

Safari tatu za baadaye

[hariri | hariri chanzo]

Kwa jumla Kolumbus alifanya safari nne hadi Amerika. Mwaka 1498 katika safari yake ya tatu alifika mara ya kwanza kwenye bara lenyewe katika mdomo wa mto Orinoco katika Venezuela. Kwa jumla alipoteza jahazi 9 katika safari zake.

Makala hii kuhusu mtu huyo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kristoforo Kolumbus kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.