Nenda kwa yaliyomo

Aime Cesaire

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Aime Cesaire

Aimé Fernand David Césaire (25 Juni 1913 - 17 Aprili 2008) alikuwa mshairi, mwandishi na mwanasiasa Mfaransa mwenye asili ya Afrika kutoka kisiwa cha Martinique katika Bahari ya Karibi.

Pamoja na Léopold Sédar Senghor na Léon-Gontran Damas alianzisha dhana ya negritude. Alikuwa mwalimu wa Frantz Fanon.

Baada ya kupita nafasi zote za elimu kisiwani Martinique alipewa nafasi ya kusoma huko Ufaransa kuanza mwaka 1931. Masomoni alikutana na Leopold Senghor wakawa marafiki.

Mwaka 1939 alirudi Martinique akawa mwalimu shuleni akimfundisha Frantz Fanon. Kabla ya kurudi aliandika shairi kubwa lenye urefu wa kitabu "Cahier d'un retour au pays natal" (daftari ya kurudi kwenye nchi nilikozaliwa).

Mwaka 1945 alichaguliwa kuwa meya wa Fort-de-France na mbunge katika bunge la Ufaransa huko Paris wa msaada wa chama cha kikomunisti. Bungeni alipeleka sheria iliyotaka kuyapa makoloni hadhi ya mikoa ya Ufaransa. Baada ya uvamizi wa Hungaria uliofanywa na jeshi la Umoja wa Kisovyeti aliachana na Wakomunisti.

Mwaka 1950 aliandika "Discours sur le colonialisme" (Hotuba kuhusu ukoloni). Katika kitabu hiki Aimé Césaire aliadhiri ukoloni wa Ufaransa.

Aliendelea kuwakilisha Martinique bungeni hadi mwaka 1993. Kwao kisiwani alikuwa mwenyekiti wa bunge la mkoa kati ya 1983 na 1988.

Mwaka 2001 alijiuzulu katika siasa.

Kiwanja cha Ndege cha Martinique kilipewa jina la "Martinique Aimé Césaire International Airport" kwa heshima yake tarehe 15 Januari 2007.

  • Juu ya ukoloni

Mkoloni anayemwangalia mwanadamu mwenzake kama mnyama ili kutuliza dhamira yake huyu mkoloni atageukia kuwa mnyama mwenyewe. - Naambiwa habari za maendeleo na magonjwa yaliyoponywa lakini mimi naongea juu ya tamaduni zilikanyagwa na watu maelfu waliokandamizwa. Nonaongea juu ya watu mamilioni waliofundishwa kutetemeka, kupiga magoti, kukata tamaa.

  • Juu ya umoja wa watu wote

Hakuna mbari ambao pekee yake una uzuri, akili, nguvu; kwa wote kuna nafasi kwenye mkutano wa washindi