Muziki wa Tanzania

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Historia ya Tanzania
Coat of Arms of Tanzania
This article is part of a series
Uendo
Historia ya Zanzibar
Afrika Mashariki 1800-1845
Ukoloni
Afrika ya Mashariki ya Kijerumani
Mkataba wa Zanzibar-Helgoland
Mkwawa
Vita vya Maji Maji
Vita vikuu vya kwanza Afrika Mashariki
Tanganyika
Mapambano ya uhuru Tanganyika
Uhuru
Uhuru wa Tanganyika
Mapinduzi ya Zanzibar
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
Julius Nyerere
Ujamaa
Tamko la Arusha
Vita vya Kagera
Ali Hassan Mwinyi
Benjamin Mkapa
Jakaya Kikwete
John Magufuli
Samia Suluhu Hassan

Tanzania Portal

Muziki wa Tanzania ni muziki wenye asili yake katika eneo la Tanzania ya leo. Kama ilivyokuwa kwa binadamu wengine, wakazi wa eneo hilo, walikuwa na utamaduni wao. Utamaduni huo ulikuwa ukitofautiana kati ya kabila na kabila. Moja ya vipengele ilikuwa muziki. Kiasili, hakukuwa na ‘muziki’ katika makabila hayo kabla ya ujio wa wageni, hivyo hakuna kabila lenye tafsiri ya neno muziki.

Lakini watu waliimba, walicheza ngoma, walipiga vyombo mbalimbali, ila walikuwa na utamaduni mwingine kuhusu kitu hiki tunachokiita siku hizi muziki. Watafiti wanatuambia tulikuwa na ngoma, ambayo tafsiri yake ni kubwa kuliko muziki.

Ngoma ilikuwa chombo kile kilichotoa muziki, ngoma ilikuwa shughuli yenyewe, kwa mfano ngoma ya mavuno, ngoma ya mashetani na kadhalika, na pia watu walicheza ngoma. Pamoja na kukosekana kwa maandiko yenye kina kuhusu hali ya ngoma katika kipindi hicho lakini tunajua watu waliimba na kucheza ngoma kwa matukio mbalimbali, hali ambayo inaendelea mpaka leo.

Historia[hariri | hariri chanzo]

Zama za ukoloni wa Kijerumani[hariri | hariri chanzo]

Magnetoph kutoka katika kituo cha redio cha Kijerumani katika Vita ya Pili ya Dunia.

Wajerumani ndio walioleta neno muziki, na wakati wao ndipo kuliingia muziki wa bendi za askari na kuingizwa katika shule ya kwanza ya serikali wakati huo, Tanga School. Katika kipindi hicho pia mchango wa madhehebu mbalimbali kuingiza muziki na vyombo vya muziki vipya uliongeza kasi ya huo muziki mpya.

Pengine kipindi hicho kwaya nazo zilianza kushika kasi, nalo neno kwaya pia ni jipya likitokana na Kiingereza choir. Historia inatueleza kuwa Mjerumani hakufanya jitihada za kuzuia muziki wa kiasili, hivyo basi muziki mpya na wa kiasili ulienda sambamba.

Zama za ukoloni wa Kiingereza[hariri | hariri chanzo]

Silinda ya Edison kwenye miaka ya 1899.

Utawala wa Mwingereza ulileta mabadiliko mengi katika muziki nchini. Askari waliotoka vitani KAR maarufu kama askari kea walirudi na hadithi kuhusu muziki, vyombo vya muziki, na hata muziki walioukuta katika safari zao vitani, vyombo kama akodian na gitaa kavu (isiyotumia umeme) viliingia wakati huo. Kutokana na watu wa makabila mbalimbali kuchanganyika na miji kuzaliwa kukaanza kuweko na utamaduni mpya.

Muziki uliyokuwa unakubalika kwa makabila yote ulianza, aina ya muziki maarufu kama Beni ilienea katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki. Waafrika waliokuwa wamesoma nao wakaanza kuwaiga Wazungu hata kuanza kutengeneza Club zao ambazo zilikuwa maarufu kama Dancing Clubs. Katika club hizo kulipigwa nyimbo mbalimbali kwa kutumia santuri na wapenzi kucheza muziki katika staili mbalimbali kama vile Cha cha, Tango, Foxtrot, Swing, Waltz na kadhalika.

Inasemekana club ya kwanza Tanganyika ilianzishwa Tanga, ikiitwa Young Noverty Dancing Club, na baadaye Dar es Salaam ikawa na Young Generation Dancing Club. Club hizo zilikuwa ndio chanzo cha bendi za kwanza Dar es Salaam, Social Orchestra, ambayo baadaye ilikuja kuwa maarufu kama Dar es Salaam Jazz Band, na pia kulikuweko na YMCA Social Orchestra, wakati huo ilikuwa katika kipindi cha kati ya miaka 1920 na 1935. Baada ya vita ya pili ya dunia 1945, Wamarekani waliweka radio yenye nguvu katika mji unaoitwa sasa Kinshasa: redio hiyo iliweza kusikika sehemu nyingi, Afrika Mashariki, ya Kati na Magharibi, na kuanza kwa lebo maarufu ya Loningisa nchini Kongo mwaka 1947 ilianzisha kusikika na kuigwa kwa muziki wa Kikongo kuanzia wakati huo.

Lebo ya Galotone ya Afrika Kusini pia ilisambaza santuri ambazo ziliingiza staili za Jive katika nchi hii, kwa miaka mingi vijana walikuwa na vikundi wakicheza jive, na bendi kadhaa ziliiga upigaji wa jive ukiambatana na upigaji wa filimbi kumuiga mwanamuziki Spokes Mashiyane. Magitaa ya umeme kwa bendi za muziki wa dansi yalianza kutumiwa kati ya mwaka 1957 na 1959, Dar Jazz tena hutajwa kama bendi ya kwanza ya muziki wa dansi kuanza kutumia gitaa hilo, ikifuatiwa na Western Jazz na bendi nyinginezo.

Kwenye mwaka 1954 Kenya ikaanza kuwa kituo kikubwa cha kurekodi muziki, na kwa miaka mingi iliyofuata bendi za Afrika Mashariki zililazimika kwenda Kenya ili kutoa santuri. Kuna wanamuziki wengine mpaka leo hufikiriwa ni Wakenya au nyimbo zao kudhaniwa kuwa zilitoka Kenya, kwa mfano Frank Humplink na dada zake ambao walitoa vibao ambavyo bado vinasikika katika anga za muziki hadi leo, Embe Dodo, Tufurahi Harusi na kadhalika.

Baada ya Uhuru katika miaka ya 1960/1970[hariri | hariri chanzo]

Santuri za miaka ya 1970

Pamoja na mapungufu yanayotajwa ya utawala wa chama kimoja, kulikuweko mambo yaliyowezekana kutokana na hali ya chama kimoja kuwa na dira inayoeleweka na hivyo kuelekeza kila kitu kadri ya matakwa ya chama. Sanaa ya Tanzania haikukwepa mwongozo wa TANU, sehemu za kazi, vijiji, miji, viliagizwa kuwa na vikundi vya ‘utamaduni’ ambavyo vingekuwa ndio vikundi vya burudani baada ya kazi na pia jukwaa la kuelezea mipango na malengo ya chama na serikali. Zikatengenezwa bendi za majeshi, polisi, JWTZ, Magereza, Uhamiaji; mashirika ya umma nayo hayakuwa nyuma, BIMA, TANCUT, DDC Mlimani, UDA na miji nayo ikawa na bendi Kurugenzi Arusha Kurugenzi Dodoma. Na ni ukweli usiopingika nyimbo nyingi maarufu kama zilipendwa zilipatikana katika kipindi hicho.

Bendi zilitunga nyimbo, ambazo zilipitiwa na kamati kabla ya kuruhusiwa kurekodiwa na kurushwa hewani. Kwa upande wake serikali nayo ikatengeza idhaa tatu katika redi ya taifa, External Service, iliyokuwa ikitangaza kwa lugha ya Kiingereza na lugha ya nchi za kusini zilizokuwa zikipigania uhuru wakati huo, kukaweko na Idhaa ya Biashara ambayo ilikuwa na vipindi vikitangaza biashara mbalimbali vilivyodhaminiwa na wafanyabiashara, katika idhaa hii, uliweza kusikia muziki kutoka popote duniani, lakini kwa makusudi kabisa kukaweko na idhaa ya Taifa ambako huku ungesikia kila aina ya muziki wa nchi hii, pamoja na kuwa kwa sasa kuna vituo vya radio zaidi ya 80 vimeshindwa kufanya kazi hii iliyoweza kufanywa na kituo kimoja cha Taifa, bahati mbaya kituo hicho cha Taifa kimeshapoteza muelekeo wake huu uliokuweko awali.

Katika miaka ya mwanzoni ya 1960, bendi ziliingia katika utamaduni wa kunakili nyimbo kutoka Kongo, kilichofanyika ni kuimba Kiswahili tu, kuna nyimbo kama Napenda nipate lau nafasi, Mtoto wacha kupiga mayowe na nyingi sana ambazo zilikuwa ni za kunakili moja kwa moja nyimbo za Kongo. Hali ilifikia kuwa mbaya mpaka bendi nyingine ziliingilia kati na kutunga nyimbo za kuwaasa wenzao watunge nyimbo zao... Koma koma koma kaka wewe tunga zako... ilikuwa baadhi ya maneno ya kuwafanya wanamuziki waliokuwa wakiiga waache kuiga.

Lakini pamoja na haya kulikuweko wanamuziki waliokuwa wakiangalia na kuiga nyimbo kutoka nchi za magharibi na baadaye wakichanganya vyombo na melody za asili na kuanza muziki uliojulikana kama Afro Rock, na kuwa sambamba na nchi nyingine katika Afrika. Katika kipindi hiki mwanasiasa mmoja aliwahi kupiga marufuku muziki wa bugi, ambao ulikuwa ni maonyesho ya muziki ya mchana yaliyokuwa yakisha saa kumi na mbili. Kupiga marufuku muziki huo kulikuwa ni sawa leo upige marufuku wanamuziki wa kizazi kipya: pengo aliloliweka halijaweza kujazwa tena.

Katika miaka ya 1980/1990[hariri | hariri chanzo]

Katika kipindi hiki kulikuweko na mfumo wa utawala wa shughuli za Utamaduni ambao pamoja na kuweko Maafisa Utamaduni wa Wilaya, Maafisa Utamaduni wa Mkoa , pia kulikuweko na Baraza la Muziki la Taifa (BAMUTA), ambapo kulizaliwa vyama ambavyo vilifanya kazi kubwa katika kuunganisha wanamuziki kama vile CHAMUDATA na Tanzania Taarab Association. Na itakuwa ni makosa kutotaja show iliyokuwa kubwa sana na iliyounganisha wanamuziki wa nchi nzima TOP TEN Show.

Show hii iliyowezekana kwa ushirikiano wa BASATA, Umoja wa Vijana, Radio Tanzania, halijawahi kutokea tena onyesho lenye ukubwa wa aina hiyo mpaka leo. Kuvurugika kwa mfumo wa uongozi wa utamaduni kwa kuwaondoa Maafisa Utamaduni walioko chini ya Wizara ya Utamaduni umeacha shughuli za Utamaduni mkononi mwa wafanyabiashara pekee, ambao kwao lengo ni kupata faida za kiuchumi, matatizo na mtokeo ya kufa kwa utamaduni si lolote kwao. Serikali inatakiwa ichukue mzigo huu wa kufadhili ukuaji na uendelezaji wa Utamaduni, na kuacha shughuli za biashara ya kazi za sanaa kwa wafanya biashara.

Zama hizi ndizo zilizozaa muziki wa kizazi kipya maarufu kama Bongo Flava. Zama hizi kuna mapinduzi makubwa sana katika muziki nchini Tanzania, mabendi mengi ya muziki wa dansi yalianzishwa, hasa kwa wale wakongwe na kuunda bendi zao binafsi. Kukua kwa teknolojia na kuanza matumizi ya kompyuta katika utayarishaji wa muziki. Hapa hasa vijana ndipo waliposhika hatamu na muziki wa kizazi kipya. Ottu Jazz Band miaka hii walitumia mtindo wa "Discipline" na walitingisha hasa katika miaka hii. Miaka hii ndipo palipoanza kuwa na taasisi au kampuni kubwa-kubwa za uburudishaji wa muziki kama vile Radio One, Clouds FM, Radio Uhuru, Times FM na nyingine nyingi tu.

Sehemu kubwa ya vijana waliozaliwa miaka ya 1980 na 1990 mwanzoni walianza hamasa ya kutaka kuwa wanamuziki na kujishughulisha na kazi muziki kwa kiasi kikubwa sana. Kipindi hiki ndiko kulikotokea makundi mbalimbali ya muziki wa hip hop ikiwa ni pamoja na Gangwe Mobb, Dewplomatz, S.O.S B., Kwanza Unit, Underground Soulz, Hard Blasterz, na wengine wengi tu. Kipindi hiki ndicho alipoibuka Saleh Jabri anayesemekana kuanzisha muziki wa hip hop kwa Kiswahili nchini Tanzania. Moja ya kazi za Saleh ni ile aliyorudia wimbo wa Vanilla Ice "Ice Ice Baby" kwa kutia maneno ya Kiswahili.

Katika miaka ya 2000/2010[hariri | hariri chanzo]

Katika kipindi hiki, muziki uliokuja juu sana ulikuwa "Bongo Flava na muziki wa dansi ambao hasa vijana wapya au wa muda kiasi walirudi kwa kasi katika kipindi hiki. Hapa bendi ambazo zilijaribu katika kipindi cha miaka ya 1990 katikakati na mwishoni zilirudi ama zilivuma kupita kiasi. Bendi kama African Revolution iliyokuwa inatumia jina au mtindo wa Chumvi-Chumvi Tutalamba ilirudi na jina la "Tam-Tam" chini ya uongozi wake Kocha wa Dunia Mwinjuma Muumini. Vilevile T.O.T Plus Band, The African Stars, akina Bob Rudala, Jungle Survivors Band na nyimbo yao ya Maprosoo, Malaika Band, Extra Bongo, Double M Sound ya Mwinjuma Muumin, Mchinga Sound, Diamond Sound, Akudo Impact, Inafrica Band na bendi nyinginezo nyingi zilitingisha katika zama hizi. Chuchu Sound Band ni miongoni mwa bendi zilizotamba sana mwanzoni mwa miaka ya 2000. Waliimba mtindo wa chakacha au mduara kwa lugha maarufu. Bendi hii ilikuwa tishio katika mtindo huo. Bila kuisahau Kilimanjaro Connection Band.

Kiufupi, wakati huu ushindani uilkuwa mkubwa sana na wanamuziki au waimbaji wengi walihama kutoka bendi moja kwenda nyingine hasa kwa kufuatia utitiri wa mabendi ya muziki wa dansi nchini. Kipindi hiki ndicho alichokuja mkali wa sauti nchini Tanzania "King of Melody" Christian Bella akitokea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kipindi hiki ndicho kilichounda bendi ya "Wajelajela Original" (Stono Musical), baadaye FM Academia chini ya ungozi wake Nyoshi El Sadat. Hii FM Academy ilikuwa moja na Stono Musica kabla ya kutengana na Nyoshi kabaki na jina halisi lakini kaongeza neno kama "The Dream Team". Zama hizi wanamuziki vijana wa Kikongo walifurika hasa kuja nchini Tanzania.

Kwa upande wa muziki wa kizazi kipya, ukiacha wale walioanza kabla ya 2000, hapa anakuja Dully Sykes, Manzese Crew, Wandava Creek, Wehu Kumi Ngangari (W TEN N), TID, Jay Moe, Ngwair, Daz Nundaz, Madee, Mandojo na Domo Kaya, Mr. Blue, Complex, Dudu Baya, Juma Nature na FSG, A.Y., G.K., Q Chillah, Mwana FA, Lady Jay Dee na Ray C.. Jay Dee ndiye msanii wa kwanza kurekodi albamu yenye gharama kubwa mno kuliko zote tangu kuanza kwa muziki wa kizazi kipya kwa kipindi kile cha mwanzoni mwa miaka ya 2000. Ndiye aliyeanza kupiga video na Benchmark Production kwa kipindi haikuwa rahisi sana kufanya kazi na kampuni hiyo. Jay Dee na A.Y. ni wasanii wa mwanzo kabisa kuthubutu kutoka nje ya mipaka ya Tanzania katika kufanya muziki na wasanii wa nchi za nje.

Hili halijawahi kufanywa hapo awali na wasaniii wowote wa kizazi kipya isipokuwa wawili hawa. Ray C. ni moja kati ya wasanii wa Bongo Flava walioweza kufanya vizuri, lakini nae hanasa za maisha zilimfanya kufuta urithi wake wote katika muziki. Haonekani tena thamani yake hasa kwa kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya. Kulikuwa na makundi yaliyoingia na kutoka. Aidha kwa kukosa udhamini au kujitangaza vya kutosha. Kundi kama "Boyz from the Army", Born Crew, Hot Grils, Big Dog Pose (BDP), Hot Port Family, Wateule, Mambo Poa, Uswahilini Matola, na wengine wengi waliingia na muda mchache hawajafua dafu wakapotea jumla. Sehemu ya kikosi cha wanamuziki waliokuwa wanajiita New Jack Family, watoto wa Kariakoo. Nao walizingua sana katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya. Hasa kwa msanii wao Dully Sykes. Kundi kama G.W.M. baadaye likaja kuwa sehemu ya Wachuja Nafaka - huku kukiwa na ongezeko la Juma Nature na Doro.

Wachuja Nafaka lilikuwa kundi la mradi tu (super group) lililodumu muda mchache tu. Wasanii wengine waliotamba katika 2001/2002/2003/2004 ni pamoja Zahrani a.k.a Big Punisher wa Bongo, Spulla, Bushoke, Mr. Nice ambaye kiukweli alitamba kupita maelezo na nyimbo za kuchukua ala za kitoto na kuzirudia katika mtindo wa Bongo Flava aliotamba nao kwa jina la TAKEU. Aliupeleka muziki wa Kitanzania mbali sana, hasa katika nchi za Burundi, Rwanda, Kongo na nchi zingine za Afrika. Bahati mbaya, hakudumu sana, hasa kwa kuendekeza hanasa za maisha nakuepelekea kuanguka mazima katika fani ya muziki. Buibui, Mpaki, Nurueli, Bab Lee, Snoop Lee, Man X na wengine wengi.

Professor Jay katika upande wa wasanii wa kiume, alionekana kuunyanyasa sana muziki wa kizazi katika miaka ya 2001/2005. Zama hizi Professor Jay alionekana kutokuwa na mpinzani, inasemekana yeye ndiye aliyesababisha wazee wasikilize muziki wa kizazi kipya. Ilikuwa mwaka 2000 na kibao chao cha Chemsha Bongo ambamo maneno mazito aliyoongea humo yalipelekea wazee wengi kusikiliza muziki huu. Kabla ya 2000, wazee wengi waliona muziki wa kizazi kipya ni kama uhuni tu. Huenda Professor Jay ndiye aliyevutia vijana wengi kuingia katika muziki kama jinsi ilivyo kwa siasa Zitto Kabwe kuvutia vijana wengi kujiunga na siasa.

Huwezi kutaja muziki wa kizazi kipya bila Prof. Jay. Mb Doggy ndiye mwanzilishi wa muziki wa mapenzi mazito, hata kama awali waliimba, lakini si kwa kiwango cha Mb Doggy. Mwaka 2005/2006 ilikuwa ni kipindi chake cha kuunyanyasa muziki wa kizazi kipya. Mb Doggy kutoka Tip Top Connection alionyesha uwezo wake mkubwa sana katika tasnia hii. Miaka hii ya 2005/2006 Ferouz nae alikuja juu sana. Lakini hakwenda mbali, dawa za kulevya zikamwangusha mazima.

Ni miaka hii, alipokuja Matonya, Abby Skills, Enika, Ali Kiba, Queen Darleen (ijapokuwa alikuwepo tangu enzi za Historia ya Kweli ya Dully Sykes), lakini hakuwa msanii kama msanii mpaka kipindi hiki. Kipindi hiki muziki wa Taarab ulipamba moto. Mwaka wa 2006, Jahazi Modern Taarab ilianzishwa chini ya uongozi wake Mzee Yusuph. Mzee Yusuph aliufikisha mbali sana muziki huo, alisababisha kila mtu asikilize taarab hasa kwa tungo zake. Baadaye zikazuka bendi nyingine nyingi tu za taarab.

Katika miaka ya 2010 -[hariri | hariri chanzo]

Katika kipindi hiki, muziki wa kizazi kipya na muziki wa dansi ulibadilka sana. Vijana wengi walikuja katika muziki wa dansi. Lakini Bongo Flava imepiga hatua maradufu. Msanii kama Diamond Platnumz ameupeleka mbali muziki wa Tanzania nje ya nchi kwa kiasi kikubwa kupita msanii yeyote yule tangu muziki huu ulipoanza. Katika kipindi hiki, rundo la wasaniii wa muziki wa Bongo Flava (walibatizwa kama wabana pua), waliongezeka na kuigana kupita kiasi. Watayarishaji wa muziki huu waliongeza maradufu. Bongo Flava, ilianza kuchukua miundo mbalimbali ya miziki mingine kama vile Kwaito, Zouk Rhumba, Singeli, Raggae, muziki wa Nigeria hasa waliiga na kadhalika. Na ndicho kipindi kilichoanza na ushamba katika muziki, hasa kwa kuanzisha makundi-makundi kati ya msanii na msanii.

Mambo hayo yaliitwa "TeamFulani" mara fulani. Lakini timu zilizokuwa na ushandani mkubwa ni za Ali Kiba na Diamond. Kipindi hiki ndicho walichovuma akina Ben Pol, Top C., Bob Junior, Darassa, One Incredible, Nikki Mbishi, Nikki wa Pili, Geez Mabovu, Baraka da Prince, Galatone Tena, Samir, Belle 9, Kassim Mganga, Nuh Mziwanda, Z. Anthony, Dullayo, Sam wa Kweli, Barnaba, Marlaw, Izzo Business, Mabeste, Linah, Gosby, Godzilla na wengine wengi tu. WCB lebo ya muziki iliyozalisha wasanii wapya kama Harmonize na Rayvanny. Vile imechukua wasanii wengine maarufu kama Richie Mavoko. Kwa pamoja wameweza kuutingisha muziki wa kizazi kipya kwa mwaka wa 2015/2016. Vilevile kuanzia Agosti 2015, Darassa ameonekana kuutawala muziki wa kizazi kipya kwa kiasi kikubwa sana. Hasa kwa kufuatia yeye anafanya hip-hop. Huenda Darassa ni msanii pekee wa hip-hop aliyeweza kufikisha watazamaji wengi kwa muda mfupi katika Youtube kuliko msanii yeyote yule wa hip-hop ya Kitanzania hasa kwa kufuatia kibao chake cha Muziki na Too Much kilichotoka Julai 15 na Muziki Novemba 23, 2016.[1] Vilevile kipindi hiki ndicho kulipozaliwa muziki wa Singeli. Wanamuziki maarufu wa Singeli ni pamoja na Man Fongo, Msaga Sumu, Sholo Mwamba na wengine wengi.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Darassa amekuwa msanii wa pili kuweka rekodi hii kwenye HipHop ya Bongo. MillardAyo.com

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]