Nenda kwa yaliyomo

Vita ya Umoja wa Kisovyeti dhidi ya Finland

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Winter War)
Vikosi vya skii vya Kifini.

Vita ya Umoja wa Kisovyeti dhidi ya Finland ilipigwa kuanzia Novemba 1939 hasi Machi 1940. Ilhali ilipiganiwa katika miezi ya baridi inaitwa pia "Vita ya msimu wa baridi" (kwa Kifini: talvisota, kwa Kiswidi vinterkriget, kwa Kirusi Зимняя война Zimnyaya voina).

Chanzo chake kilikuwa madai ya serikali ya Umoja wa Kisovyeti kukabidhiwa maeneo ya Ufini yaliyokuwa karibu na mji wa Leningrad (leo Sankt Peterburg). Baada ya Ufini kukataa, Jeshi Jekundu lilishambulia nchi jirani tarehe 30 Novemba 1940.

Uongozi wa Kisovyeti ulitarajia ushindi wa haraka katika wiki chache, kwa sababu Jeshi Jekundu lilikuwa na vifaru, mizinga na ndege nyingi kuliko jeshi la Kifini.

Vifaru, malori na maiti ya kisovyeti mwaka 1940.

Walakini, vikosi vya Kifini vilijitetea kwa nguvu na kwa muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa. Sababu moja ya vikosi vya Kifini kufanya vizuri zaidi ni kwamba walikuwa na nguo nzuri za msimu wa baridi na walivaa kanzu nyeupe ambazo zilikuwa kamafleji bora katika theluji. Vilevile, wanajeshi Wafini walizunguka wakitumia skii zilizowapa mwendo wa haraka kulingana na Warusi waliotembea kwa miguu. Vilevile wanajeshi Warusi walikosa nguo za msimu baridi na sare za kuvaa rangi ya kijani ambazo ziliwafanya rahisi kuonekana katika theluji. Kwa jumla matatizo upande wa Kisovyeti yalionyesha uhaba wa viongozi wenye maarifa, kwa sababu serikali ya Stalin iliwahi kuendesha takaso ya kisiasa kati ya majenerali ambao wengi walitupwa katika kambi za jela au kuuawa.

Hata hivyo, katika mwezi wa Februari 1940, Jeshi Jekundu lilishambulia upya na kuvunja utetezi wa Wafini. Wafini waliomba amani. Stalin alikubali bila kufikia shabaha zake zote kwa sababu alihofia kuingilia kati kwa Uingereza; pia viongozi wa Kijeshi waliogopa mwisho wa baridi na kutokea kwa matope wakati ardhi iliyoganda inayeyuka, hali ambayo ingesimamisha vifaru na magari.

Tarehe 13 Machi 1940 pande zote mbili zilitia sahihi mkataba wa amani; Ufini ulipaswa kukabidhi asilimia 11 za eneo lake kwa Umoja wa Kisovyeti, hasa maeneo ya Karelia[1].

Nyekundu: Maeneo yaliyohamishwa kutoka Ufini kwenda Umoja wa Kisovyeti baada ya vita

Kurasa zinazohusiana

Tanbihi

Viungo vya nje

Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Vita ya Umoja wa Kisovyeti dhidi ya Finland kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.