Orange Democratic Movement

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search

Orange Democratic Movement (ODM) au kwa jina kamili Orange Democratic Movement Party of Kenya ni chama cha kisiasa nchini Kenya. Kilianzishwa mwaka 2006 katika maandalizi ya uchaguzi wa bunge la Kenya 2007. Katika Agosti 2007 chama kilifarakana kati ya wafuasi wa Kalonzo Musyoka aliyeendelea kwa ODM-Kenya na maungano ya viongozi wengi zaidi pamoja na Raila Odinga walioendelea kama ODM. Sababu ya farakano ilikuwa swali la nani atakuwa mgombea wa urais upande wa ODM.

Chanzo ni kambi la machungwa katika kura ya katiba mpya[hariri | hariri chanzo]

Chanzo cha ODM ilikuwa kura maalumu ya wananchi ya 2005 kuhusu katiba mypa. Katiba ilipendekezwa na rais Mwai Kibaki na wafuasi wake. Wabunge wa LDP walipinga pendekezo la katiba pamoja na chama cha upinzani cha KANU chini ya Uhuru Kenyatta. Pande mbili katika kura hii zilipewa alama za ndizi (kambi ya "ndiyo") na chungwa (kambi ya "hapana").

LDP na KANU zilishirikiana pamoja na vyama vingine kama NPK ya Charity Ngilu katika kambi ya machungwa. Baada ya katiba kukataliwa na wananchi katika kura maalumu Kibaki aliondoa wafuasi waote wa kambi la machungwa katika serikali yake.

Kuunda chama na farakano[hariri | hariri chanzo]

Hapa waliamua kuandaa chama kipya pamoja na KANU kwa ajili ya uchaguzi wa 2007. Chama kiliundwa kwa jina la ODM-Kenya kwa sababu wakili Mugambi Imanyara asiyekuwa na uhusiano wowote na harakati aliwahi mwaka 2005 kuandikisha kisiri chama kwa jina la ODM pamoja na nembo la chungwa. Hatua hii ilitazamiwa kama jaribio la kuzuia kwa kuandikisha chama kipya chenyewe.

KANU ilijiondoa kabla ya uchaguzi na kuhamia upande wa rais Kibaki lakini viongozi kadhaa kama vile Musalia Mudavadi na William Ruto walibaki upande wa machungwa.

Swali la kumteua mgombea wa urais liligawa ODM-Kenya kwa sababu viongozi mbalimbali walitaka kushika nafasi hii. Hii ilileta farakano kati makundi ya Raila Odinga na ya Kalonzo Musyoka.

Matatizo ya majina[hariri | hariri chanzo]

Baada ya farakano kutokea swali la jina likajitokeza. Kundi la Raila likawa kubwa zaidi. Lakini ofisi ya Msajili Mkuu wa Kenya ilidai kuwa haijapokea habari za wenye cheo waliochaguliwa hivyo jina la ODM-Kenya likabaki mkononi wa watu waliokuwa upande wa Musyoka. Hapa kundi la Raila likaanza majadiliano na wakili Imanyara aliyekabidhi jina la "ODM" kwao.[1]. Inasemekana ya kwamba kambi la Odinga lililipa mamilioni kadhaa kwa jina hili.[2].

Uchaguzi wa 2007[hariri | hariri chanzo]

Katika uchaguzi wa 2007 ODM ilifaulu vizuri upande wa viti vya bunge la Kenya. Ilipata karibu nusu ya wabunge wote yaani 99 kati ya 120.

Katika uchaguzi wa rais Raila Odinga alitangaziwa kuwa ameshindwa na rais Kibaki kwa kura 230,000. Lakini watazamaji wengi waliona kasoro katika hesabu ya kura na ODM ilidai kuwa Odinga ni mshindi halali.