Mnyoo-taya

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mnyoo-taya
.....
.....
Minyoo-taya chini ya hadubini: juu Gnathostomula paradoxa, chini Haplognathia filum
Minyoo-taya chini ya hadubini: juu Gnathostomula paradoxa, chini Haplognathia filum
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia
Nusuhimaya: Eumetazoa
Faila ya juu: Platyzoa
Faila: Gnathostomulida
Ax, 1956
Ngazi za chini

Oda 2, nusuoda 2:

Minyoo-taya (kutoka kwa Kiing. jaw worm) ni minyoo wadogo wa bahari wa faila Gnathostomulida walio na mdomo wenye mataya na kibamba kama tupa.

Minyoo-taya wanaojulikana wana urefu wa mm 0.5-1. Ukubwa wao mdogo huwawezesha kuishi kati ya chembe za mchanga wa maji ya pwani ya kina kifupi. Mara nyingi ni minyoo wembamba hadi kama nyuzi na wana mwili mwangavu kwa ujumla. Katika oda Bursovaginoidea, eneo la shingo ni jembamba kidogo kuliko mwili wote, inayowapa kichwa dhahiri[1].

Kama minyoo-bapa wana epidermisi iliyofunikwa kwa silio, lakini tofauti na minyoo-bapa wana silio moja kwa kila seli[2]. Silio hizo huwaruhusu minyoo kuteleza mbele ndani ya maji kati ya chembe za mchanga, ingawa pia hutumia misuli kukunja au kubana mwili wao.

Hawana uwazi wa mwili wala mfumo wa mzunguko wa damu au wa upumuaji. Mfumo wa neva ni sahili na umezuiliwa kwa tabaka za nje za ukuta wa mwili. Ogani za fahamu pekee ni silio iliyobadilishwa, ambazo ni nyingi haswa katika eneo la kichwa.[1]

Mdomo uko nyuma ya ncha ya kichwa kwenye upande wa chini wa mwili. Una jozi ya mataya yaliyoundwa kutoka kutikulo ambayo misuli yenye nguvu imeunganishwa nayo, na mara nyingi hubeba meno madogo sana. Kibamba kidogo kwenye tako la mdomo ambacho kinabeba muundo kama kitana, pia kiko. Kibamba hicho hutumiwa kukwangua viumbe vidogo, kama vile bakteria na diatomu, kutoka kwa chembe za mchanga zinazounda makazi yao duni ya oksijeni[3]. Koromeo hii yenye ulinganifu wa pande mbili na sehemu tata za mdomo huwafanya waonekane kuwa na uhusiano wa karibu na vidudu-gurudumu na washirika wao. Mdomo hufungua katika neli bila njia ya kuondoka ambapo mmeng'enyo hufanyika, kwa hivyo hakuna mkundu wa kweli[1]. Walakini, kuna tishu zinazounganisha utumbo na epidermisi ambazo zinaweza kutumika kama tundu la mkundu[4].

Minyoo-taya ni huntha. Kila mnyoo ana ovari moja na korodani moja au mbili. Baada ya utungisho yai pekee hupasua kupitia ukuta wa mwili na kushikamana na chembe za mchanga zilizo karibu. Mzazi anaweza kuponya haraka jeraha linalosababishwa. Yai hutoa toleo dogo sana la mpevu bila hatua ya lava[1].

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. 1.0 1.1 1.2 1.3 Barnes, Robert D. (1982). Invertebrate Zoology. Philadelphia, PA: Holt-Saunders International. ku. 311–312. ISBN 0-03-056747-5. 
  2. Ruppert, Edward E., Fox, Richard S., Barnes, Robert D. (2004) Invertebrate Zoology (7th edition). Brooks/Cole-Thomson Learning, Belmont, US
  3. Barnes, R.F.K. et al. (2001). The Invertebrates: A Synthesis. Oxford: Blackwell Science.
  4. Knauss, Elizabeth (December 1979). "Indication of an Anal Pore in Gnathostomulida". Zoologica Scripta 8 (1–4): 181–6. doi:10.1111/j.1463-6409.1979.tb00630.x.  Check date values in: |date= (help)