Meno

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Jino)
Meno bora
Meno ya hatari!

Meno ni viungo vya mwili vilivyopo kinywani vyenye kazi ya kutafuna yaani kumega chakula.

Meno hupatikana kwa vertebrata (wanyama wenye uti wa mgongo). Nje ya kutafuna chakula hutumiwa pia kama silaha za kujilinda au kushambulia wanyama wengine. Wanyama kadhaa huwa na meno nje ya mdomo kwa matumizi kama silaha (mfano: tembo) yanayoweza kutumiwa pia kama vifaa vya kuchimba (mfano: nguruwe-mwitu).

Kwa binadamu meno hupatika kinywani tu. Kazi kubwa ya meno kwa binadamu ni katika umeng'enyaji wa chakula anachokula na mara chache katika kusaidia kukata vitu mbalimbali kama kutatua kitambaa au kukata kamba au waya. Binadamu ana aina mbalimbali za meno zinazomsadia kula vyakula vya aina mbalimbali kama vile vya mimea na nyama. Kwa kawaida mtu mzima huwa na meno thelathini na mbili.

Utangulizi[hariri | hariri chanzo]

Aina za meno kinywani

Umeng'enyaji wa chakula huanzia kinywani. Humo tunakitafuna kwa meno mpaka kiwe laini.

Binadamu huwa na aina mbili za meno. Tunazaliwa na mbegu za meno ya utoto yanayobadilishwa wakati wa kubalehe kwa meno ya kudumu. Kwa hiyo kuna wakaa mbili za meno.

Idadi ya meno ya utoto katika wakaa ya kwanza ni 20. Huanza kuota mtoto anapokuwa na umri wa miezi sita na kawaida yote huwa yamekwisha kuota mtoto anapotimiza umri wa miaka miwili.

Idadi ya meno katika wakaa ya pili ni 32. Huanza kuota katika umri wa miaka sita, yakakamilika katika umri wa miaka 18-20. Lakini mwingine huota upesi au hukawia.

Aina za Meno[hariri | hariri chanzo]

Umbo la meno hufuatana na kazi ambayo inayapasa kufanya. Meno yaliyopo katikati ya kila taya huwa na kingo kali za kukatia chakula. Haya huitwa meno ya kukatia au meno ya mbele (ing:incisors). (meno 8 ya kukatia, katika kila taya yapo meno 4).

Meno yanayofuata meno ya kukatia ni machonge (canine teeth). Yapo machonge 4 kwa ujumla; katika kila taya kuna machonge 2. Kazi yao ni kurarua chakula.

Meno yanayofuata machonge huitwa magego madogo (premolars) (jumla ya magego madogo ni 8; na katika kila taya yapo 4); na meno yanayoyafuata hayo huitwa magego (molars) (magego yote ni 12, na katika kila taya kuna magego 6. Magego madogo na magego ni kwa kusagia chakula. Katika wakaa wa kwanza huwa hakuna magego madogo.

Muundo wa Jino[hariri | hariri chanzo]

Muundo wa jino

Meno hukaa kwa uthabiti ndani ya vitundu vya mataya. Kila jino lina sehemu mbalimbali. Sehemu ambayo huonekana kinywani ni kichwa cha jino (tajino), na sehemu iliyomo ndani ya taya ni kizizi cha jino.

Sehemu kubwa ya jino ni mfupa laini unaoitwa dentini. Dentini kwenye sehemu ya tajino au kichwa hufunikwa kwa gamba la jino. Kichwa ni cha ufupa mgumu sana wenye rangi nyeupe ya kung’aa unaoitwa enameli ya jino. Kazi yake ni kulinda mfupa laini zaidi ya ndani. Pembe ya shina hulindwa na tabaka aina ya saruji ijulikanayo kwa jina la kitaalamu kama sementi ya jino (ing. cementum).

Katikati hasa ya sementi ya jino na mfupa wa taya kuna utando, ambao unasaidia kukuza jina katika kitundu chake, nao (utando huo) hulingana na ufizi wa meno.

Ndani ya jino kuna uwazi mwenye tishu ya neva na mishipa ya damu. Neva pamoja na mishipa ya damu huingia katika mvungu penye ncha ya kizizi cha jino.

Magonjwa ya Meno[hariri | hariri chanzo]

Kuoza kwa meno[hariri | hariri chanzo]

Kuoza kwa meno. Chakula cha hatari kwa meno ni baadhi ya kile chenye kabohidrati hasa aina za sukari. Kikiachwa kinywani huganda kwenye uso wa meno kama ganda la mashapo. Katika mashapo haya kwenye meno huishi bakteria zinazoendelea kula mabaki ya vyakula ndani yake zinastawi vema hasa kwenye sukari iliyomo hapa. Bakteria hizi zinatengeneza asidi inayoshambulia enameli cha kichwa cha meno na pia mfupa wa dentini. Kwa njia hii vitundu vinaweza kutokea. Vikienea hadi fofota ya jino neva ndani yake hailindwi tena iko wazi na maumivu ya jina yanaanza. Hatimaye neva itaoza na kufa kabisa. Hapa maumivu hutulia kabisa. Lakini usikubali kudanganywa. Kwa njia ya mvungu hata nafasi inayozunguka ncha ya jino itashambuliwa, na vijidudu vitaenea hadi kwenye utando wa ule mfupa na hatimaye kusababisha jipu na madhara mengine kinywani.

Kiseyeye[hariri | hariri chanzo]

Zaidi ya kuoza kwa meno kuna ugonjwa wa mishipa inayozunguka meno, ndiyo kiseyeye (Pyrrohoea). Katika ugonjwa huu ufizi unaweza kuvimba na kutoka damu ukiguswa kidogo tu, kama kwa mfano mtu anaposafisha meno yake kwa mswaki. Ugonjwa ukizidi ule mfupa unaozunguka jino utaharibika na jino litalegea na mwishowe hata kutoka lenyewe. Ugonjwa huu husababishwa na ukosefu wa vitamini C mwilini.

Magonjwa mengine yanayosababishwa na meno mabovu[hariri | hariri chanzo]

Licha ya magonjwa meno, hata magonjwa mengine yanaweza kutokea. Mara nyingi vijidudu vya jipu huingia moja kwa moja katika njia ya damu, au pengine usaha unaomezwa pamoja na vijidudu huweza kuanzisha ugonjwa wa kuvimba katika sehemu nyingine za mwili.

Utunzaji wa meno[hariri | hariri chanzo]

Inampasa kila mtu kusafisha meno yake baada ya kula na kuondoa vipande vyote vya chakula vinavyobaki hasa kati ya jino na jino. Wakati mwingine ulio bora kwa kusafisha meno kabla ya kwenda kulala. Ili ufanikiwe kusafisha meno vizuri tumia mswaki; na ili kuondoa vipande vya chakula vilivyomo kati ya jino na jino tumia kijiti chenye ncha kali au kilichochongeka. Wakati ugonjwa wa meno unapoanza, ikiwa daktari wa meno yuko katika mtaa au kijiji chako, umwendee ili azibe tundu la jino lako. Jino lolote bovu lisiloweza kutibiwa tena inafaa ling’olewe ili lisiweze kuambukiza ugonjwa katika sehemu nyingine za mwili.

Angalia Pia[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  • Roberts, M. (2000). Advanced Biology, Nelson, London.
  • Franks, A. S. T. (1973). Geriatric Dentistry, Oxford


Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Makala hii kuhusu mambo ya anatomia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Meno kama matumizi yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.