Nenda kwa yaliyomo

Katibu mkuu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Javier Perez de Cuelar (kushoto) na wajumbe wa kumaliza vita vya Iran-Iraq mwaka 1988.

Katibu Mkuu ni cheo cha kiongozi katika chama, shirika, kanisa, klabu au taasisi[1] . Kwa mujibu wa itifaki, yuko chini ya mkuu au mwenyekiti wa shirika, lakini mara nyingi ushawishi wake ni mkubwa kuliko wa yule ambaye ni kiongozi mkuu kwa jina. Kwa kawaida yeye ni mjumbe wa bodi kuu ya shirika, ndiye mkuu wa utawala katika shirika na mkuu wa wafanyakazi.

Kama shirika linaongozwa na kamati au bodi inayofanya maazimio ya msingi, Katibu Mkuu huwajibika kwa shughuli za kila siku.

Hata hivyo, wapo makatibu wakuu (wingi wa 'katibu mkuu') katika ngazi za serikali kama vile katibu mkuu wa baraza la mawaziri ambaye hujulikana kama katibu mkuu kiongozi hali kadhalika katibu mkuu wa wizara.[2]

Lugha ya Kiingereza ina majina kadha wa kadha kumaanisha 'katibu mkuu' kama vile secretary general, principal secretary, first secretary, executive secretary na kadhalika; tofauti na Kiswahili ambacho kina mbadala mmoja wa mtendaji mkuu.

Umoja wa Mataifa

[hariri | hariri chanzo]

Katika Umoja wa Mataifa cheo cha Katibu Mkuu wa UM kinamtaja mtendaji kiongozi wa ofisi kuu.

Serikali na wizara

[hariri | hariri chanzo]

Katika nchi nyingi kiongozi wa utawala ndani ya wizara fulani huitwa Katibu Mkuu akifanya kazi chini ya waziri ambaye ni kiongozi wa kisiasa. Ilhali mawaziri hubadilishwa mara kwa mara, watumishi wa wizara hudumu na katibu mkuu ana kazi ya kuwasimamia na kupanga kazi yao.

Vyama vya Kikomunisti

[hariri | hariri chanzo]

Katika vyama vya Kikomunisti vilivyofuata mfumo wa Umoja wa Kisovyeti, katibu mkuu aliunganisha madaraka ya mwenyekiti na kiongozi wa utawala; mfumo huo ulianzishwa na Josef Stalin, kuendelezwa hata baada yake na kuigwa na vyama vingine. Hadi leo kiongozi wa chama cha Kikomunisti katika China, Vietnam, Laos, Korea Kaskazini na Kuba anatumia cheo cha katibu mkuu au "katibu wa kwanza" na kutokana na mfumo wa utawala ndiye pia kiongozi mwenye madaraka makuu katika nchi.

Cheo rasmi Mwenye cheo tangu
Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha China Xi Jinping 15 Novemba 2012
Katibu wa Kwanza wa Chama cha Wafanyakazi wa Korea Kim Jong Un 17 Desemba 2011
Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha Vietnam Nguyễn Phu Trọng 19 Januari 2011
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi cha Wananchi wa Laos Thongloun Sisoulith 15 Januari 2021
Katibu wa Kwanza wa Chama cha Kikomunisti cha Kuba Miguel Diaz-Canel 19 Aprili 2021