Nenda kwa yaliyomo

Hakimiliki

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Alama ya hakimiliki.
Video inayoeleza historia ya hakimiliki

Hakimiliki (kwa Kiingereza: copyright) ni utaratibu wa kisheria unaompa mmiliki wa kazi za akili (kama vile kitabu, sinema, picha, wimbo au tovuti) haki ya kuamulia matumizi yake. Sheria za hakimiliki zinalenga kukinga watungaji wa kazi za akili dhidi ya matumizi ya kazi yao na wengine wanaojipatia faida kwa njia hiyo bila kumzingatia mtungaji anayeweza kukosa ruzuku kutokana na kazi yake.

Chini ya sheria za hakimiliki, kazi ya kiakili inaweza kunakiliwa pekee ikiwa mmiliki anatoa ruhusa. Ikiwa mtu ananakili kazi bila kibali, anakiuka hakimiliki.

Kutegemeana na sheria za nchi mbalimbali mkiukaji anaweza kushtakiwa chini ya sheria za biashara au wakati mwingine sheria za jinai. Mkiukaji anaweza kuhukumiwa kulipa fidia au hata kwenda jela. Kwa kawaida, sheria za hakimiliki hulinda haki za watungaji na warithi wao kwa kipindi fulani, katika sheria ya kimataifa angalau hadi miaka 50 baada ya kifo cha mtungaji[1]. Nchi mbalimbali huwa na vipindi virefu zaidi[2].

Katika nchi zinazofuata zaidi sheria za Marekani kuna kanuni zinazorahisisha kampuni kushika hakimiliki badala ya wafanyakazi wake kama kazi ilitekelezwa ofisini.

Historia ya hakimiliki[hariri | hariri chanzo]

Hakimiliki ilianzishwa kwa waandishi wa vitabu. Kabla ya kupatikana kwa uchapishaji, vitabu viliweza kunakiliwa tu kwa mkono, kazi ambayo inachukua muda mrefu. Lakini kwa kutumia mashine za kuchapa, vitabu vinaweza kunakiliwa kwa haraka na urahisi. Kwa sababu hiyo, vitabu vingi vilinakiliwa, ila waandishi walikosa mapato. Ndiyo chanzo cha kutunga sheria ya kumpa mwandishi hakimiliki kuhusu kazi yake.

Kutokana na maendeleo ya teknolojia, sheria za hakimiliki zilianza kupanuliwa zikitaja pia media kama picha, sauti, na filamu.

Nani anamiliki hakimiliki?[hariri | hariri chanzo]

Katika nchi nyingi, watungaji wanamiliki hakimiliki kwa kazi yoyote waliyotengeneza au kuunda, maadamu hawampi mtu mwingine hakimiliki.

Kama mtungaji analipwa kufanya kazi kwa mtu mwingine, mwajiri mara nyingi atapata hakimiliki badala ya mwandishi mwenyewe. Kwa mfano, ikiwa mtu anayefanya kazi kwa kampuni Microsoft inaunda mpango mpya wa programu ya kompyuta kazini, kampuni ya Microsoft inakuwa na hakimiliki. Ni kawaida kwamba kampuni itasajili hakimiliki ili kuwazuia wafanyakazi wao kudai kazi zao.

Urefu wa ulinzi wa hakimiliki[hariri | hariri chanzo]

Sheria za hakimiliki kawaida hulinda wamiliki wa hakimiliki zaidi ya maisha yao. Katika nchi nyingine, kama Kanada, New Zealand na Tanzania, kazi zinalindwa kwa miaka 50 baada ya mwandishi kufa. Katika nchi nyingine, kama Marekani na Uingereza, kinga hiyo hudumu kwa miaka 70 baada ya kifo. [3] Wakati kipindi cha ulinzi wa hakimiliki kimekwisha, muziki, kitabu, picha, au kazi nyingine yoyote ya ubunifu iko kwenye uwanja wa umma . Hii inamaanisha kuwa hakuna mwenye hakimiliki tena, na kila mtu yuko huru kuiga, kuitumia na kuibadilisha bila kuwa na ruhusa ya kuomba au kumlipa mmiliki.

Maudhui huria[hariri | hariri chanzo]

Ili kuepukana na masuala ya kisheria, vikundi vya waandishi wamekuja na wazo la maudhui huria (open content). Katika mfumo wa maudhui huria, waandishi wanampa kila mtu ruhusa ya kunakili, kubadilisha, kutoa au kuuza kazi zao, mradi tu watafuata masharti fulani. Masharti hayo yanaelezwa katika leseni ya maudhui huria. Baadhi ya masharti ya maudhui huria ni:

  1. Ikiwa mtu anabadilisha maudhui huria, au mtu akiunda kazi mpya kutona nayo, lazima amtaje mwandishi wa kwanza.
  2. Ikiwa mtu atachapisha sehemu ya kazi iliyobadilishwa au inayopatikana, lazima awakubali wengine wazitumie chini ya leseni hiyohiyo ya maudhui huria.
  3. Chini ya leseni kadhaa, mtu hawezi kuuza sehemu ya kazi au kuitumia kupata pesa.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. [https://www.wipo.int/treaties/en/text.jsp?file_id=283698#P127_22000 Art 7, Berne Convention for the Protection of Literary and Artistic Works]
  2. Nchini Tanzania sheria ni "The Copyright and Neighbouring Rights Act", 1999, inayofuata Mapatano ya Bern
  3. "Publication Right, Database Right" (PDF).

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]

Makala hii kuhusu mambo ya sheria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Hakimiliki kama historia yake au uhusiano wake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.