Hadithi za Mtume Muhammad
Sehemu ya mfululizo wa makala juu ya |
Imani na ibada zake |
Umoja wa Mungu |
Waislamu muhimu |
Abu Bakr • Ali |
Maandiko na Sheria |
Qur'an • Sunnah • Hadithi |
Historia ya Uislamu |
Historia |
Tamaduni za Kiislamu |
Shule • Madrasa |
Tazama pia |
Hadithi au Sunnah ni maneno na vitendo ambavyo Mtume Muhammad alikuwa akisema au akifanya katika kipindi chake cha utume. Hadithi hizi ni mmoja kati ya miongozo ya imani kwa Waislamu.
Hadithi hizi zinajumuisha pia mambo aliyoyaona au kuyasikia katika muda wa utume wake akalinyamazia kimya au akawa hakulipinga na akalikubali.
Asili
Muhammad aliishi miaka kama arobaini bila kuwa na imani ya Mungu pekee.
Kisha Mwenyezi Mungu akamletea mjumbe kutoka kwake aitwaye malaika Jibrili anayeaminiwa na Waislamu kuwa ndiye aliyempa aya zilizoko katika msahafu wa Waislamu, Kurani.
Inaelezwa kuwa Jibrili alimpa Muhammad aya hizo kwa muda wa miaka ishirini na mitatu mpaka alipofariki dunia akiwa na umri wa miaka 63.
Hadithi za Mtume Muhammad zimekusanywa katika vitabu vingi sana na wanazuoni mbalimbali wa Hadithi, lakini vitabu vya hadithi ambavyo ni muhimu na vinategemewa na wengi katika Uislamu ni hivi vifuatavyo:
Vitabu vya Hadithi
- 1- Sahih Al-Bukhari
- 2- Sahih Muslim
- 3- Sunan An-Nasai
- 4- Sunan At-Tirmidhi
- 5- Sunan Ibn Majah
- 6- Sunan Abu Daud
- 7- Muwatt'a Ibn Maalik
- 8- Musnad Ahmad bin Hanbal
Mtume Muhammad alikuwa hapendelei Hadithi zake ziandikwe wakati mmoja na Kurani, yasije yakachanganyika maneno yake na yale ya Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo Hadithi zilichelewa kuandikwa mpaka baada ya kufariki kwake dunia kwa muda mkubwa kidogo, na kwa sababu hiyo Hadithi zikatawanyika sehemu mbalimbali kulingana na usahihi wake au udhaifu wake au uwongo wake.
Hivyo kuna Hadithi aina nne kulingana na fahamu na kutegemewa kwa msimulizi wa hiyo Hadithi: Hadithi Sahihi, Hadithi Hasan (Nzuri), Hadithi Dhaifu na Hadithi Maudhu'u (Hadithi ya Uwongo).
Vile vile, kuna aina nyingine za Hadithi zilizogawanyika kwa mujibu wa mambo mengine kama vile: kwa mujibu wa wapokezi, au mfululizo wa wasimulizi, au idadi ya wasimulizi katika kila sehemu ya mfululizo, au kwa mujibu wa simulizi lenyewe na msimulizi wake.
Hadithi kwa mujibu wa fahamu na kutegemewa kwa msimulizi
- Hadithi Sahihi huwa imesimuliwa kutegemewa ukweli wake na dini yake na mtu ambaye anafahamu nini anasimulia, na kuieleza hadithi kama alivyoipokea kutoka kwa Mtume Muhammad.
- Hadithi Hasan au Nzuri huwa inajulikana asili yake na wasimulizi ni watu maarufu.
- Hadithi Dhaifu huwa ile isiyofikia daraja ya Hasan, kwa sababu ya upungufu wa mmoja katika wasimulizi, au mfululizo wa wasimulizi haufikii mpaka kwa Mtume unakatika kwa mojawapo ya Masahaba, au mmoja katika wasimulizi si wa kutegemewa, na kuna kasoro fulani katika mambo haya.
- Hadithi Maudhu'u (ya Uwongo) ni ile hadithi iliyobuniwa ikatiwa katika Hadithi za Mtume, na huwa kawaida inakwenda kinyume na Qurani au Hadithi nyinginezo Sahihi au Hasan, au kutonasibiana na maneno yake Mtume au kuwa msimulizi wa Hadithi hii ni mwongo, au kuwa msimulizi hakukutana na yule ambaye amesema amepokea kwake katika mfululizo wa wasimulizi waliotajwa, au kuweko kasoro fulani katika maelezo au matukio yaliyotajwa ndani ya Hadithi hio.
Hadithi kwa mujibu wa wasimulizi
- Hadithi Qudsi ni ile hadithi ambayo Mtume Muhammad ameisimulia kutoka kwa Mola wake
- Hadithi Marfu'u ni hadithi iliyopokewa na mfululizo wa wasimulizi na kufikishwa mpaka kwa Mtume
- Hadithi Mauquf ni ile hadithi iliyosimuliwa na masahaba lakini wasiseme kuwa wameipokea kutoka kwa Mtume mwenyewe.
- Hadithi Maqtu'u ni ile hadithi iliyokatika silsila au mfululizo wake .
Viungo vya nje
- http://www.hadiths.eu Ilihifadhiwa 12 Aprili 2012 kwenye Wayback Machine.