Nenda kwa yaliyomo

Filemoni

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mchoro mdogo wa kifodini cha Filemoni, Afia na Onesimo.

Filemoni pamoja na mke wake Afia alikuwa kati ya Wakristo wa kwanza wa mkoa wa Frigia (karne ya 1).

Ni maarufu hasa kwa kupokea barua ya Mtume Paulo kuhusu mtumwa wake Onesimo ambaye alikuwa amemtoroka na labda kumuibia. Kumbe alipokutana na Paulo aliongokea Ukristo. Hapo alirudishwa kwa Filemoni akileta hiyo barua ambayo baadaye iliingia katika Agano Jipya la Biblia ya Kikristo kama Waraka kwa Filemoni.

Inaonekana humo kwamba Filemoni alikuwa tajiri wa mji wa Kolosai ambaye Wakristo wa huko walikuwa wanakusanyika nyumbani mwake kwa ajili ya ibada.[1][2][3]

Inasemekana aliuawa kwa ajili ya imani pamoja na mke wake na wengineo.

Kwa vyovyote anaheshimiwa na madhehebu mbalimbali kama mtakatifu.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 22 Novemba[4].

Barua ya Mtume Paulo kwa Filemoni

[hariri | hariri chanzo]

1 Mimi Paulo, mfungwa kwa ajili ya Kristo Yesu, na ndugu Timotheo, ninakuandikia wewe Filemoni mpendwa, mfanyakazi mwenzetu

2 na kanisa linalokutana nyumbani kwako, na wewe dada Afia, na askari mwenzetu Arkupo.

3 Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana yesu Kristo.

4 Kila wakati ninaposali nakukumbuka wewe Filemoni, na kumshukuru Mungu

5 maana nasikia habari za imani yako kwa Bwana wetu Yesu na upendo wako kwa watu wote wa Mungu.

6 Naomba ili imani hiyo unayoshiriki pamoja nasi ikuwezeshe kuwa na ujuzi mkamilifu zaidi wa baraka zote tunazopata katika kuungana kwetu na Kristo.

7 Ndugu, upendo wako yameniletea furaha kubwa na kunipa moyo sana! Nawe umeichangamsha mioyo ya watu wa Mungu.

8 Kwa sababu hiyo, ningeweza, kwa uhodari kabisa, nikiwa ndugu yako katika Kristo, kukuamuru ufanye unachopaswa kufanya.

9 Lakini kwa sababu ya upendo, ni afadhali zaidi nikuombe. Nafanya hivi ingawa mimi ni Paulo, balozi wa Kristo Yesu, na sasa pia mfungwa kwa ajili yake.

10 Basi, ninalo ombi moja kwako kuhusu mwanangu Onesimo, ambaye ni mwanangu katika Kristo kwani nimekuwa baba yake nikiwa kifungoni.

11 Ni Onesimo yuleyule ambaye wakati mmoja alikuwa hakufai kitu, lakini sasa ananifaa mimi na wewe pia.

12 Sasa namrudisha kwako, naye ni kama moyo wangu mimi mwenyewe.

13 Ningependa akae nami hapa anisaidie badala yako wakati niwapo kifungoni kwa sababu ya Habari Njema.

14 Lakini sitafanya chochote bila kibali chako. Sipendi kukulazimisha unisaidie, kwani wema wako unapaswa kutokana na hiari yako wewe mwenyewe na si kwa kulazimika.

15 Labda Onesimo aliondoka kwako kwa kitambo tu, kusudi uweze tena kuwa naye daima.

16 Na sasa yeye si mtumwa tu, ila ni bora zaidi ya mtumwa: yeye ni ndugu yetu mpenzi. Na wa maana sana kwangu mimi, na kwako atakuwa wa maana zaidi kama mtumwa na kama ndugu katika Bwana.

17 Basi, ikiwa wanitambua mimi kuwa mwenzako, mpokee tena kama vile ungenipokea mimi mwenyewe.

18 Kama alikuwa amekukosea kitu, au alikuwa na deni lako, basi, unidai mimi.

19 Naandika jambo hili kwa mkono wangu mwenyewe: yako.)

20 Haya, basi, ndugu yangu, nifanyie jambo hilo kwa ajili ya jina la Bwana; burudisha moyo wangu kama ndugu katika Kristo.

21 Naandika nikitumaini kwamba utanikubalia ombi langu; tena najua kwamba utafanya hata zaidi ya haya ninayokuomba.

22 Pamoja na hayo, nitayarishie chumba kwani natumaini kwamba kwa sala zenu, Mungu atanijalia niwatembeleeni.

23 Epafra, mfungwa mwenzangu kwa ajili ya Kristo Yesu, anakusalimu.

24 Nao akina Marko, Aristarko, Dema na Luka, wafanyakazi wenzangu, wanakusalimu.

25 Nawatakieni ninyi nyote neema ya Bwana wetu Yesu Kristo.

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]
  1. Const. Apost., VI, 46
  2. Filemoni 1:1-2
  3.  "Philemon". Catholic Encyclopedia. New York: Robert Appleton Company. 1913.
  4. Martyrologium Romanum
Makala hii bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.