Nenda kwa yaliyomo

Nzi-ning'inia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Bittacidae)
Nzi-ning'inia
Nzi-ning'inia wa Kimmins (Bittacus kimminsi) katika Afrika Kusini
Nzi-ning'inia wa Kimmins (Bittacus kimminsi) katika Afrika Kusini
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye miguu yenye viungo)
Nusufaila: Hexapoda (Wanyama wenye miguu sita)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Ngeli ya chini: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda: Mecoptera (Wadudu walio na mabawa marefu na miguu mirefu)
Hyatt & Arms, 1891
Familia: Bittacidae
Handlirsch, 1906
Ngazi za chini

Jenasi 15:

Nzi-ning'inia (kutoka kwa Kiing. hangingfly) ni wadudu wakubwa kiasi (sio nzi wa kweli) wa familia Bittacidae katika oda Mecoptera ambao hujining'inia kwenye uoto wakitumia jozi ya miguu ya mbele tu kushika mmea. Miguu mingine minne hutumika kwa kukamata mbuawa. Bittacus ni jenasi ya pekee inayotokea barani Afrika. Wananafana na nzi miguu-mirefu ambao ni aina za mbu kwa kweli.

Nzi-ning'inia ni wadudu wakubwa kiasi wenye mwili wa urefu wa mm 10-26. Wana miguu mirefu ambayo huwafanya waonekane kama nzi miguu-mirefu, lakini tofauti na hao wana mabawa manne marefu yenye umbo sawa, ambayo yanaweza kuwa mangavu au kuwa na mabaka au milia ambayo mara nyingi ni meusi, kijivu au kahawia. Kichwa kina mdomo mrefu ambao huingiza vimeng'enya kwenye mbuawa wao. Fumbatio yao ni kahawia, hudhurungi au rangi ya maziwa[1].

Wadudu hawa ni mbuai na wakiruka hukamata nzi wadogo na wadudu wengine. Wananyakua mbuawa wao kwa jozi ya pili na ya tatu ya miguu, ambayo hutoholewa kwa kusudi hili. Kisha huingiza vimeng'enya ndani ya mbuawa, baada ya hapo wanashika jani au tawi ndogo kwa miguu yao ya mbele. Wakining'inia huku miguu yao ya kati na ya nyuma ikishikilia mbuawa, wanangoja vimeng'enya kuyeyusha tishu zake na kisha kufyonza kioevu.

Kabla ya kupandana dume humpa jike mdudu mbuawa ili kumtongoza. Ikiwa mbuawa amepokelewa, wanapandana wakati jike akila[2]. Mayai hutagwa kwenye takataka za majani au chini kidogo ya uso wa udongo katika maeneo manyevu. Lava wanafanana sana na viwavi, kwa kuwa wana miguu sita halisi kwenye thoraksi na jozi za miguu ya bandia kwenye pingili sita hadi nane za fumbatio. Pingili ya kumi inabeba kisahani cha mfyonzo au si ya kawaida sana jozi ya kulabu. Wana mandibulo kubwa kiasi. Chakula chao kinajumuisha hasa mimea na kwa kiasi fulani wadudu waliokufa. Bundo hana kifukofuko bali hulala katika udongo au mbao zinazooza wenye miguu na mandibulo huru.

Spishi za Afrika ya Mashariki

[hariri | hariri chanzo]
  • Bittacus aequalis
  • Bittacus alluaudi
  • Bittacus berlandi
  • Bittacus discors
  • Bittacus erythrostigma
  • Bittacus fumosus
  • Bittacus lachlani
  • Bittacus leptocercus
  • Bittacus lineatus
  • Bittacus montanus
  • Bittacus moschinus
  • Bittacus pobeguini
  1. Gullan, P.J.; Cranston, P.S. (2014). The Insects: An Outline of Entomology. Wiley. ku. 1345–1347. ISBN 978-1-118-84616-2.
  2. Gao, Qionghua; Hua, Baozhen (3 Desemba 2013). "Co-Evolution of the Mating Position and Male Genitalia in Insects: A Case Study of a Hangingfly". PLOS ONE. 8 (12): e80651. Bibcode:2013PLoSO...880651G. doi:10.1371/journal.pone.0080651. PMC 3849121. PMID 24312490.{{cite journal}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
Makala hii kuhusu mdudu fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Nzi-ning'inia kama uainishaji wake wa kibiolojia, maisha au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.