Ayuki

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Ayuki (Alpha Aurigae, Capella)
Ukubwa wa nyota nne zinazofanya Ayuki-Capella na Jua letu ("sol")
Kundinyota Hudhi (Auriga)
Mwangaza unaonekana 0.08
Kundi la spektra K0 III
Paralaksi (mas) 76.20 ± 0.46
Umbali (miakanuru) 42.9
Mwangaza halisi +0.167
Masi M☉ Aa: 2.56; Ab: 2.48
Nusukipenyo R☉ Aa: 12; Ab: 8.8
Mng’aro L☉ Aa:78.7; Ab: 72.2
Jotoridi usoni wa nyota (K) Aa: 4970; Ab: 5730
Majina mbadala α Aurigae, α Aur, Alpha Aurigae, Alpha Aur, 13 Aurigae, 13 Aur, ADS 3841, BD+45 1077, CCDM J05168+4559, FK5 193, GC 6427, GJ 194, HD 34029, HIP 24608, HR 1708, IDS 05093+4554, LTT 11619, NLTT 14766, PPM 47925, SAO 40186, WDS 05167+4600A
Ayuki - Capella katika kundinyota Hudhi (Auriga)

Ayuki (ing. na lat. Capella ka-pel-la, pia α Alpha Aurigae, kifupi Alpha Aur, α Aur) ni nyota angavu zadi katika kundinyota la Hudhi (Auriga). Ni pia nyota angavu ya sita kabisa kwenye anga. Mwangaza unaoonekana ni 0.08 mag. Iko karibu na Dunia ikiwa umbali wa miaka nuru 43.[1]

Jina

Ayuki ilijulikana kwa mabaharia Waswahili tangu miaka mingi wakifuata njia yao baharini wakati wa usiku kwa msaada wa nyota. [2]. Walipokea jina hili kutoka kwa Waarabu waliosema العيوق al-ayuq ambalo linamaanisha “Kizuizi” au “Kitenganishi” kwa sababu waliona nyota hii inatenganisha Dabarani na Kilimia [3].

Hapa hawakutafsiri jina la Wagiriki waliosema "Αιξ" aiks yaani mbuzi.[4]. Hapa walifuata Wababeli wa Kale waliotangulia kuona hapa mbuzi.

Katika picha ya Hudhi inayodhaniwa angani Ayuki iko mbegani wa kushoto.

Jina la Kilatini lililopokelewa na kuthibitishwa na UKIA ni “Capella” [5] na maana ya jina ni « mbuzi mdogo ».

Katika mitholojia ya Kigiriki kuna masimulizi ya mungu Zeus aliyefichwa baada ya kuzaliwa kwa sababu babake mungu Kronos alimeza watoto wake wote; hivyo Kronos alidanganywa kwa kupewa jiwe katika vitambaa vya mtoto na Zeus mdogo alifichwa kwenye kisiwa cha Krete katika pango na humo alilishwa na mbuzi.

Tabia

Ayuki - Capella ilitambuliwa baada ya kupatikana kwa darubini bora zaidi si nyota moja bali nyota maradufu katika mfumo wa nyota nne. Zinakaa kama jozi mbili za mapacha.

Jozi ya kwanza ni nyota mbili kubwa zinazoitwa Capella Aa na Capella Ab. Jozi ya pili ni nyota ndogo zinazokaa kwa umbali wa vizio astronomia 9,500 kutoka Aa-Ab na hizi zinaitwa Capella H na Capella L.

Aa ni nyota jitu jekundu iliyomaliza tayari akiba ya hidrojeni na sasa inayeyunganisha heli yake kuwa kaboni na oksijeni. Spektra yake ni ya aina G8III. Masi yake ni mara 2.69 masi ya Jua ikiwa na ng'aro mara 78.5 ya Jua letu. solar luminosities (Capella Aa), 77.6 (Capella Ab),.

Ab ina masi ya jua mara 2.56 na spektra yake ni ya aina G0-1 III. Aa na Ab zinazungukana kwa umbali wa kizio astronomia 0.72 au kilomita milioni 108 katika muda wa siku 104.

Nyota za H (aina ya spektra M1-M2.5) na L (spektral M5) ni nyota kibete nyekundu inayozungukana kwa umbali wa vizio astronomia 49

Tanbihi

  1. Kaler, Capella
  2. ling. Knappert 1993
  3. “it is [said to be] called العيوقbecause of its [being regarded as] impeding الدبران from meeting الثُرَيَا” (yaani waliona inazuia Dabarani kukutanana na Kilimia); Lane Arabic-English Lexicon I-5, uk. 2199
  4. Hivi Ptolemaio katika orodha yake ya Almagesti kufuatana na Allen uk 87; hata hivyo Allen anahisi ya kwamba Kiarabu "ayuq" ni namna ya kuandika jina la Kigiriki "aiks".
  5. Naming Stars, tovuti ya Umoja wa Kimataifa wa Astronomia (Ukia), iliangaliwa Novemba 2017


Viungo vya Nje

Marejeo

    • Allen, Richard Hinckley: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, ukurasa 67 (online kwenye archive.org)
  • Knappert, Jan: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331
  • Lane, Edward William: Arabic-English Lexicon, in eight parts; Book 1- part 5, Lahore 1978, uk 2199; online hapa kwenye archive.org