Nenda kwa yaliyomo

Kidukari

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Aphididae)
Kidukari
Vidukari wa kabichi (Brevicoryne brassicae)
Vidukari wa kabichi (Brevicoryne brassicae)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye mwili wa pingili na miguu ya kuunga wasio na ugwe wa mgongo kama wadudu, nge, buibui)
Nusufaila: Hexapoda (Arithropodi wenye miguu sita)
(bila tabaka): Dicondylia (Wadudu walio na mandibula zenye condyle mbili)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Nusungeli: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda ya juu: Paraneoptera
Oda: Hemiptera
Nusuoda: Sternorrhyncha
Familia ya juu: Aphidoidea
Familia: Aphididae
Latreille, 1802
Ngazi za chini

Nusufamilia 24:

Vidukari, vidukali au wadudu-mafuta ni wadudu wadogo wa familia Aphididae katika oda Hemiptera ya nusungeli Pterygota (wenye mabawa). Aphididae ni familia pekee ya familia ya juu Aphidoidea iliyopo hadi sasa; familia nyingine zimekwisha zote. Vidukari ni miongoni mwa wadudu wasumbufu sana katika kilimo na katika bustani na juu ya mimea nyumbani, kwa sababu wanafyunza utomvu wa mimea, ule wa floemi hasa lakini mara kwa mara ule wa ksilemi pia. Utomvu wa floemi una ukolezi mkubwa wa sukari na ukolezi mdogo wa asidi-amino. Ili kupata asidi-amino za kutosha, lazima kidukari afyunze utomvu mwingi na kwa sababu ya hii anapata sukari zaidi ya kiasi anachohitaji. Kiasi cha sukari kilichozidi kinatolewa kama mana (kitone cha shira chenye ukolezi mkubwa sana wa sukari: honeydew kwa Kiing.). Sisimizi wanapenda mana sana lakini hawawezi kunywa yote. Kwa hivyo mana nyingi inaanguka kwenye majani na hapa kuvu nyeusi inaanza kukua juu yake. Kuvu hii inazuia majani yasifanye usanidimwanga na mmea unanywea. Kwa bahati nzuri wakulima wana wadudu rafiki ambao hula vidukari kama wadudu-kibibi (lava na wadudu wapevu), wadudu mabawa-vena (lava na wapevu), nzi-wangamaji (lava tu), nyigu wa kidusia (lava tu), buibui-kaa n.k. Pia kuna kuvu viuawadudu (entomopathogenic fungi) inayoambukiza wadudu hawa, kama Metarhizium anisopliae, Beauveria bassiana, Isaria fumosorosea na Lecanicillium longisporum.

Vidukari ni wadudu wadogo. Wapevu wa takriban spishi zote wana urefu wa mm 1-5, lakini spishi nyingine zinaweza kufika mm 10. Kiwiliwili cha vidukari kina umbo wa pea mara nyingi au kimerefuka kidogo. Kiunzi-nje ni chororo lakini kimepakiwa nta ya kuhifadhi mara nyingi. Nta hii hutolewa kutoka mirija miwili nyuma kwenye fumbatio. Vipande vya mdomo vimeungana katika mrija pia na mrija huu hutumika ili kufyunza utomvu. Wakati wa majira mazuri vidukari hawana mabawa lakini wakati majira yanakuwa mabaya au ubora wa chakula unaanza kuwa mbaya, vidukari wenye mabawa huzaliwa ambao huhamia mimea ingine.

Jinsia ya vidukari ni ya kike kwa kawaida. Kwa hivyo mayai ya majike hukua bila kurutubishwa. Vidukari wengi zaidi huzaa lava waliotoka kwa mayai ndani ya ovarioli za mama. Lava wanafanana na mamao isipokuwa ukubwa wake. Kwa kawaida lava huambua mara nne kabla ya kuwa wapevu. Spishi nyingi huzaa madume wakati majira yanakuwa mabaya. Baada ya kupandana majike huyataga mayai ambayo yanapumzika mpaka majira mazuri.

Spishi zilizochaguliwa

[hariri | hariri chanzo]