Kuvu Kiuawadudu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Nzige waliouawa na kuvu kiuawadudu Metarhizium acridum

Kuvu kiuawadudu ni kuvu inayokua kama kimelea ndani ya kiwiliwili cha mdudu na kumwua mwishowe. Nyingine ni vimelea vya faradhi nyingine ni vimelea vya hiari. Vile vya kwanza vinaweza kukua ndani ya mdudu tu, lakini vile vyingine vinaweza kukua katika udongo vilevile. Pia kuna kuvu ambazo zinakua ndani ya mdudu bila kumwua lakini mdudu adhoofishwa na kutaga mayai machache kuliko mududu mzima.

Mzunguko wa maisha wa kawaida[hariri | hariri chanzo]

Kidukari kijani wa mfyulisi (Myzus persicae) aliyeuawa na kuvu Pandora neoaphidis. Alama ya kipimo = mm 0.3.

Kwa kawaida spora (vijimbegu) za kuvu hizi hujiambatisha kwa kiunzi nje cha mdudu. Kama halijoto na unyevuanga ni nzuri spora hizi huota na kuumba nyuzi nyeupe ambazo zinatoboa kiunzi kwa msaada wa vimeng'enya. Zikifika ndani ya kiwiliwili nyuzi hujigawa katika seli (blastospora) ambazo zinazidisha katika damu ya mdudu. Zikiwa zimejaza kiwiliwili na kumaliza virutubishi, mdudu afa. Kama hali ya hewa ni kavu kuvu huzaa spora ndani ya mzoga, lakini kama unyevuanga ni mkubwa kuvu hukua nje na juu ya mzoga ambapo spora zizaliwa. Spora mpya zinaweza kuambukiza wadudu wengine.

Makundi[hariri | hariri chanzo]

Kuvu viauwadudu hazimo katika kundi moja monofiletiki lakini katika makundi kadhaa ya himaya ya Fungi, k.m. katika oda Entomophthorales na ngeli Ascomycota. Divisheni Microsporidia ina vimelea vya wadudu visivyowaua.

Spishi kadhaa[hariri | hariri chanzo]

 • Entomophthorales
  • Entomophaga grylli
  • Entomophthora muscae
  • Pandora neoaphidis
  • Zoophthora radicans
 • Ascomycota
  • Beauveria bassiana
  • Cordyceps melolonthae
  • Isaria fumosorosea
  • Lecanicillium lecanii
  • Metarhizium anisopliae
  • Nomuraea rileyi
 • Microsporidia
  • Nosema locustae
  • Vairimorpha ephestiae

Kuvu zilizo na mnasaba na kuvu viuawadudu huambukiza na kuua invertebrata wengine (k.m. nematodi).

Udhibiti wa visumbufu[hariri | hariri chanzo]

Popote duniani watu wanavutika na kutumia kuvu viuawadudu katika udhibiti wa kibiolojia wa wadudu na arithropodi wasumbufu wengine, kwa sababu kuvu hizi zinatoka kwenye uasilia na zinachukuliwa kama kutokuwa na hatari kwa mazingira. Mahususi, hatua bila jinsia za Ascomycota kama spishi za Beauveria, Metarhizium, Isaria, Lecanicillium n.k. zina sifa nzuri kwa kuzitumia kama dawa za kibiolojia. Kuvu hizi zinaweza kukua juu ya chakula chenye wanga wengi ndani yake, kama nafaka.

Spishi za Entomophthorales zina uwezo mkubwa wa kuua wathiriwa wao na husababisha magonjwa ya mlipuko katika umma za wadudu. Lakini spishi za makundi mengine hazifanyi hii mara nyingi. Kuvu viuawadudu haziui wadudu wote lakini kila spishi ya kuvu huua nambari fulani ya spishi za wadudu tu. Ili kufaa kama dawa ya kibiolojia lazima kuvu iwaue idadi kiasi ya wadudu. Vilevile lazima kuvu hii ichanganyikwe na maji au mafuta na viambato vyingine au katika unga, na mchanganyiko huu lazima uweze kuhifadhiwa angalau miezi sita. Watu wanahitaji pia njia ya kunyunyiza dawa hii: aina ya bomba la kupulizia, dozi, wakati wa siku n.k.

Angalia pia[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]