Angkor Wat

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Sura ya hekalu kuu
Angkor Wat inavyoonekana kutoka hewani
Sanamu ya mchezaji wa hekaluni

Angkor Wat ni hekalu kubwa katika mkoa wa Angkor, Kamboja. Hekalu hilo lilijengwa katika karne ya 12 kwa amri ya mfalme Suryavarman II kama kitovu cha mji mkuu wake. Ni hekalu la Kihindu kubwa zaidi duniani. Limetangazwa na Unesco kuwa sehemu ya urithi wa dunia.

Ibada katika hekalu zilibadilihswa baadaye kuwa za Kibuddha na leo hii imekuwa ishara ya taifa la Kamboja na sehemu ya nembo lake.

Hekalu la Angkor Wat ni sehemu ya jumla ya majengo mengine mengi ya kidini ya Angkor, iliyokuwa eneo la miji mikuu ya wafalme wa Khmer kama vile Angkor Wat, Angkor Tom na mengine katika karne ya 9 hadi karne ya 15. Hakuna mabaki ya majengo nje ya mahekalu kwa sababu Wakhmer walitumia mawe kwa majengo ya kidini pekee.

Hekalu liko takriban km 240 upande wa kaskazini-magharibi wa mji mkuu Phnom Penh.[1]

Majengo

Eneo lote la hekalu la Angkor Wat lina urefu wa km 1.5 na upana wa km 1.3. Lote limezungukwa na mfereji wa maji mwenye upana wa mita 190. Kwa hiyo hekalu liko kwenye kisiwa kilichotengenezwa na binadamu. Mawe makubwa ya ujenzi yalisafirishwa kwenye maji kwa njia ya boya.

Mawe yamenyoshwa kwa umakini na kuunganishwa bila sementi na bila kuonyesha mapengo.

Katikati ya kisiwa kuna hekalu kuu lenye minara 5 inayoitwa prasat. Mnara mkubwa una kimo cha mita 65.

Kuta za hekalu zimejaa sanamu zilizochongwa katika jiwe. Zinaonyesha hasa wachezaji wa kike wakati wa kucheza katika ibada mbele ya miungu. Sanamu hizo zimechongwa kila moja kwa namna ya pekee, hakuna mbili zilizo sawa. Kwenye ghorofa la juu kuna kanda za picha za kuchongwa katika jiwe zinazoonyesha masimulizi ya mashairi matakatifu ya Wahindu yanayoitwa Ramayana na Mahabharata.

Historia

Chanzo cha ujenzi wa miji na hekalu kilikuwa azimio la wafalme wa Khmer katika karne ya 9 la kutengeneza malambo na mifereji ya umwagiliaji katika eneo la Angkor. [[Miundombinu] hiyo iliweka msingi kwa kilimo cha mpunga chenye mazao kadhaa kila mwaka na kuleta idadi kubwa ya watu pamoja na utajiri kwa nchi. Kwa njia hiyo milki ya Khmer ilikuwa dola lenye uwezo mkubwa katika Asia Kusini Magharibi lililoweza kujenga miji mikubwa yenye mahekalu ya ajabu.

Mwaka 1113 mfalme Suryavarman II alianza kuwa mtawala wa Khmer hadi 1150. Alishinda vita kadhaa na kupanua eneo la milki. Alitengeneza upya mahekalu yaliyokuwepo na kuanzisha makazi mapya ya kifalme pamoja na hekalu kubwa la Angkor Wat. Alikabidhi hekalu kwa ibada ya mungu wa kihindu Vishnu. Wataalamu wanaona dalili ya kwamba hekalu hili lilikusudiwa kuwa baadaye pia hekalu la kaburi la mfalme huyu.

Katika miaka ya baadaye eneo la Angkor ilivamiwa na maadui wa Khmer, kurudishwa tena chini ya milki yao na tangu mwaka 1200 mfalme Jayavarman VII alianzisha mji mkuu mpya wa Angkor Tom. Mfalme huyo alikuwa mfuasi wa Buddha, si tena mfuasi wa miungu ya Uhindu. Kwa hiyo hekalu kuu la Angkor Tom likawa hekalu la Kibuddha.

Miaka iliyofuata ibada za Kihindu katika Angkor Wat zilififia na kuwa mahali pa Wabuddha.

Katika karne ya 15 Wathai walivamia na kutwaa Kamboja na eneo la Angkor halikuwa tena mji mkuu. Lakini Angkor Wat iliendelea kutumiwa na wamonaki Wabuddha. Wakati ule hapakuwa tena na pesa ya kukarabati mahekalu, hivyo majengo mengi yalifunikwa na misitu minene. Angkor Wat ilihifadhiwa kutokana na mfereji mpana wa maji uliozuia uenezaji wa misitu.

Tangu karne ya 17 wasafiri wa kwanza kutoka ng'ambo walifika Kamboja na kutembelea Angkor Wat.

Wazungu wa karne ya 19 waliandika juu ya hekalu wakishangaa jinsi gani majengo mazuri namna hii yalijengwa katika nchi iliyokuwa maskini na katika hali duni wakati wao. [2]

Tanbihi

  1. "Angkor Temple Guide". Angkor Temple Guide. 2008. Iliwekwa mnamo October 31, 2010.  Check date values in: |accessdate= (help)
  2. http://www.cambodianview.com/documents/articles/Brief_Presentation.pdf Maelezo kwa watalii katika Angkor Wat

Viungo vya Nje

Wikimedia Commons ina media kuhusu: