A7, Tanzania
Barabara ya kitaifa ya A7 ni barabara kuu nchini Tanzania inayounganisha Dar es Salaam na Iringa. Ni barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 492.
Inaanza ndani ya jiji la Dar es Salaam kwenye Barabara ya Morogoro. Ndani ya jiji ni pana yenye njia 4, katika mwaka 2019 ilianza kupanuliwa vile hadi Kibaha ambako yako makao makuu ya Mkoa wa Pwani; inatarajiwa kupanuliwa kama barabara ya malipo hadi Chalinze. Baada ya Mlandizi A7 inatelemka bondeni ikivuka mto Ruvu kwenye daraja jipya la Ruvu. Kwa km 105 pale Chalinze A14 inaanza kuelekea Tanga na Mombasa. Baadaye inaingia katika Mkoa wa Morogoro kwa km 140 ikivuka mto Ngerengere.
A7 hupita Morogoro na Milima ya Uluguru ikiendelea katika nchi ya vilima hadi Hifadhi ya Taifa Mikumi. Inapita hifadhi ya taifa ambako magari yanaweza kupita bila kulipa kiingilio na kwa kubahatika wanaweza kuona wanyamapori. Ndani ya hifadhi magari yanapaswa kufuata mwendo kasi wa km 50 kwa saa. Takriban km 336 baada ya Dar es Salaam A7 inafika kwenye Mto Ruaha Mkuu na kuifuata hadi daraja la Mbuyuni inapoingia katika Mkoa wa Iringa kwa kufuata bonde la Mto Lukosi.
Takriban km 420 baada ya Dar es Salaam njia inapanda na kufika kwenye nyanda za juu za Uhehe. Barabara kuu inapita Lugalo kwa km 451 baada ya Dar es Salaam penye mnara wa ukumbusho wa mapigano ya mwaka 1891 ambako Wahehe walishinda kikosi cha Jeshi la Schutztruppe la Wajerumani.
Baada ya km 492 A7 inafika Iringa.