Kiangazi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Kipindi cha Kiangazi)
Kiangazi katika Hifadhi ya Tarangire, Tanzania

Kiangazi (pia msimu au majira ya kiangazi) ni kipindi cha kila mwaka cha mvua kidogo, hasa katika tropiki. Hali ya hewa katika nchi za tropiki inatawaliwa na ukanda wa mvua wa kitropiki, ambao hutoka kaskazini hadi kusini mwa tropiki na kurudi katika kipindi cha mwaka. Nje ya tropiki, msimu wa joto ni kama kiangazi katika maeneo mengi. Msimu wa baridi pia unaweza kuhesabiwa kama msimu wa ukame kwa kusema kifiziolojia, kwa sababu hata ikiwa kuna mvua katika mfumo wa theluji, baridi hufanya mimea isiweze kufyonza maji kutoka udongo.

Ukanda wa mvua wa kitropiki[hariri | hariri chanzo]

Ukanda wa mvua wa kitropiki uko katika nusutufe ya kusini takriban kuanzia Oktoba hadi Machi. Wakati huo tropiki ya kaskazini huwa na kiangazi chenye mvua kidogo na kwa kawaida siku huwa na jua kotekote. Kuanzia Aprili hadi Septemba ukanda wa mvua uko katika nusutufe ya kaskazini na tropiki ya kusini ina kiangazi chake. Kulingana na Uainishaji wa hali ya hewa wa Köppen kwa hali ya hewa ya tropiki, mwezi wa kiangazi hufafanuliwa kama mwezi ambapo wastani wa mvua ni chini ya mm 60[1].

Ukanda wa mvua hufika kaskazini takriban kama Tropiki ya Kansa na kusini takriban kama Tropiki ya Kaprikoni. Karibu na latitudo hizo kuna msimu mmoja wa mvua na msimu mmoja wa kiangazi kila mwaka. Kwenye ikweta kuna misimu miwili ya mvua na miwili ya kiangazi, wakati ukanda wa mvua hupita mara mbili kwa mwaka, mara moja kuelekea kaskazini na mara moja kuelekea kusini. Kati ya Tropiki na ikweta maeneo yanaweza kukumbwa na msimu mfupi wa mvua (vuli) na msimu mrefu wa mvua (masika) na kiangazi kifupi na kiangazi kirefu. Jiografia ya maeneo mahususi inaweza kurekebisha mifumo hii ya hali ya hewa kwa kiasi kikubwa.

Ukame[hariri | hariri chanzo]

Wakati wa kiangazi unyevunyevu ni mdogo sana hata kusababisha baadhi ya mashimo ya maji na mito kukauka. Ukosefu huo wa maji (na ukosefu wa chakula unaofuatana nao) unaweza kulazimisha wanyama wengi walishao kuhamia maeneo yenye unyevu zaidi. Mifano ya wanyama hao ni: pundamilia, ndovu, twiga, vifaru, swala, nyumbu, nyati wa maji, nyati wa Afrika, gauru, tapiri, emu, mbuni, rea na kangaruu. Kwa sababu ya ukosefu wa maji katika mimea, mioto ya msituni ni ya kawaida[2].

Magonjwa[hariri | hariri chanzo]

Takwimu zinaonyesha kuwa katika Afrika mwanzo wa msimu wa kiangazi unaambatana na kuongezeka kwa visa vya surua na magonjwa mengine ya kuambukiza, ambayo watafiti wanaamini huenda yanachangiwa na msongamano mkubwa wa watu wakati wa kiangazi, kwani shughuli za kilimo karibu haiwezekani bila umwagiliaji. Wakati huo baadhi ya wakulima huhamia mijini na hivyo kutengeneza maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu na kuruhusu magonjwa kuenea kwa urahisi zaidi[3].

Utafiti[hariri | hariri chanzo]

Data mpya zinaonyesha kuwa katika sehemu za Msitu wa Amazon katika Amerika ya Kusini ukuaji na ufunikaji wa majani hutofautiana kati ya misimu ya kiangazi na ya mvua, na takriban 25% zaidi ya majani na ukuaji wa haraka zaidi wakati wa kiangazi. Watafiti wanaamini kwamba Amazon yenyewe ina athari katika kuleta mwanzo wa msimu wa mvua, kwa sababu kwa kukua majani mengi huvukiza maji zaidi[4]. Walakini, ukuaji huo unaonekana tu katika sehemu zisizo na usumbufu za bonde la Amazon, ambapo watafiti wanaamini kwamba mizizi inaweza kufikia ndani zaidi na kukusanya maji zaidi ya maji ya ardhini[5]. Imeonyeshwa pia kwamba viwango vya ozoni ni vya juu zaidi wakati wa kiangazi kuliko msimu wa mvua katika bonde la Amazon[6].

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Updated world Köppen-Geiger climate classification map.
  2. Wet & Dry Seasons.
  3. Dry Season Brings On Measles In Sub-Saharan Africa. ScienceDaily (February 7, 2008).
  4. Amazon rainforest does have rainy and dry seasons. mongabay.com (March 12, 2007).
  5. Amazon rainforest greens up in the dry season.
  6. V. W. J. H. Kirchhoff, I. M. O. Da Silva, E. V. Browell (1990). "Ozone measurements in Amazonia: Dry season versus wet season". Journal of Geophysical Research 95 (D10): 16913. Bibcode:1990JGR....9516913K. doi:10.1029/jd095id10p16913. Archived from the original on 2011-06-06. Retrieved 2008-04-21.  Unknown parameter |url-status= ignored (help)