Nenda kwa yaliyomo

Kifaru

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Vifaru)

Kwa gari la kijeshi linalobeba silaha tazama hapa: Kifaru (jeshi)

Kifaru
Kifaru mweusi (Diceros bicornis)
Kifaru mweusi (Diceros bicornis)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Chordata (Wanyama wenye ugwe wa neva mgongoni)
Ngeli: Mammalia (Wanyama wenye viwele wanaonyonyesha wadogo wao)
Oda: Perissodactyla (Wanyama wenye kidole kimoja au vitatu mguuni)
Familia: Rhinocerotidae
Gray, 1820
Ngazi za chini

Jenasi 4, spishi 5, nususpishi 16:

Vifaru au faru ni wanyamapori wakubwa wa familia Rhinocerotidae. Spishi mbili zinapatikana Afrika na nyingine tatu huko Asia. Nchini Uhindi wanabaki faru 2700 tu na hata faru weupe nao wameadimika sana duniani.

Faru hufahamika sana kwa umbo lake kubwa (ni miongoni mwa wanyama walanyasi wakubwa sana ambao wanabakia); huku kila spishi ya faru ikikaribia kuwa na uzito wa tani moja na ngozi ngumu ya kujilinda, yenye unene wa sentimeta 1.5 – 5.0; ubongo mdogo wa mamalia (gramu 400 – 600) na pembe kubwa. Hula sana majani.

Faru wana uwezo mkubwa wa kusikia na kunusa, lakini uoni wao si mzuri sana. Weusi huishi kwa miaka 60 na zaidi.

Faru huthaminiwa sana kutokana na pembe zao. Pembe hizo zimetengenezwa kwa keratini, protini, sawa na ile inayopatikana kwenye nywele na kucha.[1] Faru wa Afrika na wa Sumatra wana pembe mbili huku wale wa Uhindi na wa Java wakiwa na pembe moja tu. Faru wa Afrika hukosa meno ya mbele na kutegemea zaidi magego katika kusaga chakula.

Uainishaji

[hariri | hariri chanzo]

Kuna spishi tano zinazoweza kuwekwa katika makundi matatu. Spishi mbili za Afrika, faru mweupe (white rhinoceros) na faru mweusi (black rhinoceros) walitokea kama miaka milioni 5 iliyopita. Tofauti kubwa kati ya faru mweupe na faru mweusi ni muundo wa midomo yao. Faru mweupe ana mdomo mpana kwa ajili ya kula nyasi huku mdomo wa faru mweusi ikiwa imechongoka kiasi.

Faru mweupe (Ceratotherium simum)

[hariri | hariri chanzo]
Faru mweupe huyu kimsingi ni wa kijivu

Faru weupe kwa muonekano ni wa kijivu. Neno "mweupe" ni tafsiri ya neno la Kiingereza "white". Nadharia maarufu ni kwamba neno hilo linatokana na neno la Kiholanzi "wijd" au la Kiafrikaans "wyd", lililo na maana ya "pana", kwa sababu mdomo wa spishi hii ni mpana wenye umbo la mraba. Lakini nadharia hiyo inatiliwa shaka siku hizi[2][3].

Spishi hii ina nususpishi mbili: faru mweupe kaskazi (C. s. cottoni) na faru mweupe kusi (C. s. simum). Wale wa kusini bado ni wengi kiasi, lakini leo (2022) majike wawili wa kaskazini wanabaki tu katika Hifadhi ya Ol Pejeta karibu na Nanyuki, Kenya.

Faru mweupe ndiyo mnyama mkubwa wa nchi kavu baada ya tembo. Anakaribiana kidogo na faru wa Uhindi na kiboko. Faru weupe wana mwili uliojaa, na kichwa kikubwa, shingo fupi na kifua kipana. Faru anaweza kuzidi uzito wa kilogramu 3,500 na urefu wa mita 3.5 – 4.6 kuanzia kichwani na mabega ya urefu wa sentimeta 180 – 200. Uzito wa faru mweupe uliovunja rekodi ni ule wa kilogramu 4,500.[4] Ana pembe mbili huku ile ya mbele ikiwa kubwa zaidi hata kufikia urefu wa sentimeta 90 – 150. Faru weupe pia wana nundu kubwa inayoshikilia vichwa vyao vizuri. Huwa na nywele kadhaa hasa kwenye masikio yao na mkiani, sehemu nyingine za mwili zikiwa zimesambaa kidogo tu.

Faru mweusi (Diceros bicornis)

[hariri | hariri chanzo]
Faru mweusi ana mdomo uliochongoka.

Faru weusi wana mdomo uliochongoka. Wanafanana kwa rangi na faru weupe. Hii inachanganya sana, sababu majina yao ni tofauti lakini rangi zao ni sawa kabisa. Spishi hii ina nususpishi tiso ndani yake, ambazo tatu zimeisha sasa na moja labda pia. Faru mkubwa mweusi huwa na urefu wa sentimeta 132 – 180 mabegani mwake na urefu wa mita 2.8 – 3.8 kuanzia kichwani mwake.[5] Huwa na uzito wa kilogramu 850 mpaka 1600, na wachache mpaka kg 1800, huku faru jike wakiwa na umbo dogo kiasi kuliko wanaume. Pembe kubwa mbili zimetengenezwa kwa keratini huku ile kubwa ya mbele ikiwa ina urefu wa mpaka sentimeta 50, na mmoja aliwahi hata kufikia sentimeta 140. Wakati fulani hata pembe la tatu hujitokeza. Faru weusi ni wadogo kiasi kuliko faru weupe, na wana mdomo uliochongoka kwa ajili ya kukusanya majani kabla ya kula.

Kutokana na umuhimu wa wanyama hawa nchi ya Tanzania imeamua kuwatunza faru kwa kuwaweka sehemu isiyorasmi kwao kwa uangalizi mkubwa, maeneo kama grumeti na pia kwa kuwapa majina, kwa mfano Faru John.

Faru wa Uhindi (Rhinoceros unicornis)

[hariri | hariri chanzo]
Faru wa Uhindi na mwanae.
Sanamu ya Faru wa shaba, wa Western Han (202 K.K – 9 BK) nyakati za China

Faru wa Uhindi hasa wanapatikana sana huko Nepal na hasa kaskazini – mashariki mwa India. Sasa wanapatikana Pakistan mpaka Bama na wamefika hadi China. Lakini kutokana na mwingiliano wa binadamu, uwepo wao umeathirika na wameanza kupungua. Ngozi yao pana ya kahawia karibu na kijivu yenye mikunjo. Juu ya miguu yao na mabega yao kuna vijinundu, na wana nywele kidogo kwenye miili yao. Faru dume huwa wakubwa kiasi kuliko faru jike kufikia uzito wa kilogramu 2500 – 3200. Faru hawa wana urefu wa sentimeta 175 – 200 mabegani. Faru jike wa india hufikia mpaka uzito kilogramu 1900. Faru hawa hufikia mpaka urefu wa mita 3.0 – 4.0. Karibu theluthi mbili ya faru wote waliobaki duniani, wanapatikana katika mbuga ya Taifa Kaziranga huko India.

Faru wa Java (Rhinoceros sondaicus)

[hariri | hariri chanzo]

Hawa ndio mamalia wakubwa walio hatarini kutoweka. Mpaka mwaka 2002, walikuwa wamebaki faru 60, huko Java Indonesia na Vietnam. Hii ndio spishi ndogo kuliko wote. Wanyama hawa wanapenda kukaa kwenye misitu ya mvua, nyasi ndefu na maeneo yenye mafuriko ya hapa na pale na matope.

Faru wa Java pia wana pembe moja. Pia ngozi yao ya kijivu ina mikunjo na wana nundu kama faru wa India, na hawana nywele. Urefu wa mwili wake ni mita 3.1 – 3.2, pamoja na kichwa na urefu wa mita 1.5 – 1.7. Faru wakubwa wanaripotiwa kufikia uzito wa kilogramu 900 – 1400 au 1360 – 2000, kwa chanzo tofauti. Pembe za faru dume hufikia mpaka sentimeta 26 huku faru jike huwa na nundu tu, na wakati mwingine hawana kabisa.

Faru wa Sumatra (Dicerorhinus sumatrensis)

[hariri | hariri chanzo]
Faru wa Sumatra huko Bronx Zoo

Hawa ndio faru wadogo kabisa katika spishi zote za faru na ndiye huyu pekee mwenye manyoya mengi na anayeweza kuishi katika sehemu za juu hasa za Borneo na Sumatra. Kutokana na kuharibika kwa makazi yao na ujangili, wameadimika sana na miongoni mwa mamalia walioadimika sana. Mpaka sasa inaaminika sana kwamba wamebaki faru 275 wa spishi hii.

Faru wa Sumatra wana kimo cha urefu wa sentimeta 130 mpaka mabegani, na mwili wake wa urefu sentimeta 240 – 315, na wana uzito wa kilogramu 700, japo baadhi yao wana uzito hata kufikia kilogramu 1000. Kama faru wa Afrika, hao wana pembe mbili zenye urefu mpaka sentimeta 25 – 27 na ile pembe ya pili ni ndogo na huwa ndogo kufikia sentimeta 10. Faru dume wana pembe kubwa kuliko faru jike. Nywele/manyoya ya miili yao hupungua kadiri wanavyoongezeka umri. Rangi ya faru hawa ni kahawia – nyekundu. Mwili wao ni mfupi na miguu yao pia na midomo yao ina nguvu sana.

  1. "Scientists Crack Rhino Horn Riddle?". Ohio University. 11 Novemba 2006. Iliwekwa mnamo 15 Oktoba 2014.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  2. Skinner, John D.; Chimimba, Christian T. (2005). The Mammals of the Southern African Subregion. Cambridge University Press. uk. 527. ISBN 978-0-521-84418-5.
  3. Rookmaaker, Kees (2003). "Why the name of the white rhinoceros is not appropriate". Pachyderm. 34: 88–93. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2022-08-18. Iliwekwa mnamo 2022-08-18. {{cite journal}}: Unknown parameter |dead-url= ignored (|url-status= suggested) (help)
  4. "African Rhinoceros?". Safari Now. 18 Desemba 2013. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2014-08-14. Iliwekwa mnamo 15 Oktoba 2014.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  5. "Black Rhinoceros?". Bisbee's Conservation Fund. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2015-12-05. Iliwekwa mnamo 15 Oktoba 2015.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)