Ugomvi wa Waarabu na Israeli
Ugomvi wa Waarabu na Israeli (kwa Kiarabu: الصراع العربي الإسرائيلي, Aṣ-Ṣirāʿ al-ʿArabī al-'Isrā'īlī; kwa Kiebrania: הסכסוך הישראלי-ערבי, HaSikhsukh HaYisre'eli-Aravi) ni ugomvi wa muda mrefu kati ya nchi za Kiarabu za Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini upande mmoja na nchi ya Israeli upande mwingine.
Ugomvi ulianza wakati wa kuundwa kwa taifa la kisasa la Israeli mwaka 1948 ukaendelea hadi leo. Chanzo chake kilitokea wakati wa miaka ya 1940 ambako kuundwa kwa Israeli kuliandaliwa katika Palestina pamoja na vita ya uhuru ya 1948-49 na kufukuzwa kwa Wapalestina wengi kutoka maeneo ya Israeli. Uliendelea kwa njia ya vita mbalimbali.
Utangulizi
[hariri | hariri chanzo]Mizizi ya mgongano ilikuwa katika harakati za Uzayuni na uhamiaji wa Wayahudi kutoka Ulaya kuelekea Palestina zilizoanza mnamo mwaka 1880. Wakati ule idadi kubwa ya Wayahudi walikaa katika nchi za Ulaya, hasa Ulaya ya Mashariki na ya Kati. Kama jumuiya ya kidini walikuwa na uhusiano wa kiroho na nchi ya mababu wao iliyowahi kuitwa kwa majina kama Israeli au Yuda lakini iliyoitwa wakati ule "Palestina" ikiwa ni sehemu ya Milki ya Osmani na kukaliwa na wasemaji wa lugha ya Kiarabu waliokuwa Waislamu, Wakristo na Wayahudi. Mnamo 1880 Palestina ilikuwa na wakazi wapatao 450,000. Asilimia 80 walikuwa Waislamu, asilimia 10-12 Wakristo na takriban 5-8 Wayahudi wenyeji.
Ubaguzi na mateso dhidi ya Wayahudi vilianza kuzidi hasa katika nchi za Milki ya Urusi na kusababisha idadi kubwa ya Wayahudi kuhama. Ilhali wengi walihamia Ulaya ya Kati na Marekani kulitokea pia na harakati ya Uzayuni iliyoona Wayahudi kuhamia nchi ya mababu wao. Wafuasi wa Uzayuni walifika Palestina wakanunua ardhi na kuunda vijiji vya Kiyahudi pekee pamoja na Wayahudi waliowahi kuishi kule.
Wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia Milki ya Osmani ilipigana upande wa Ujerumani dhidi ya Urusi, Ufaransa na Uingereza. Mwaka 1917 serikali ya Urusi ilipinduliwa na sasa Uingereza ilitafuta kushawishi Urusi na Marekani kujiunga pamoja na vita upande wa Uingereza. Hapo serikali iliona vema kutafuta usaidizi wa jumuiya za Kiyahudi zilizokuwa kubwa hasa Urusi na Marekani. Hapo waziri Balfour aliandika barua kwa msemaji ya Wayahudi wa Uingereza ambamo aliahidi usaidizi wa Uingereza kwa kukubali kuanzishwa kwa "maskani ya kitaifa kwa Wayahudi" (a national home for the Jewish people).
Baada ya vita na kuporomoka kwa Milki ya Osmani Palestina ilikuwa eneo la kudhaminiwa lililotawaliwa na Uingereza kwa niaba ya Shirikisho la Mataifa. Uhamiaji wa Wayahudi wa harakati ya Kizayuni uliongezeka kiasi pamoja na kuundwa kwa vijiji vya ujamaa aina ya kibbuz. Uhamiaji wa Wayahudi kufika Palestina ulisababisha kukua kwa uchumi. Wakazi waliongezeka kutokana an Wayhudi waliofika na pia Waarabu kutoka nchi jirani waliotafuta kazi.
Mateso ya Wayahudi katika Ulaya tangu kufika serikali ya Adolf Hitler katika Ujerumani yaliongeza idadi ya wahamiaji. Kwenye mwisho wa Vita Kuu ya Pili kulikuwa na Wayahudi kutoka pande zote za Ulaya waliokombolewa katika kambi za mauti na maelfu kati ya hao walitafuta pia njia za kufika Palestina. Wakati ule idadi ya Wayahudi ilifikia tayari takriban theluthi mja ya wakazi wote wa PAlestina waliokuwa mnmao milioni 2.
Uhamiaji huu uliongeza fitina kati ya wakazi Waarabu wa Palestina na wakazi Wayahudi na hapo Uingereza uliamua kujiondoa nchini na kuandaa uhuru wake.
Mwaka 1947 Umoja wa Mataifa uliamua mpango wa kugawa Palestina ambako madola mawili yangeanzishwa, moja ya Kiarabu na moja ya Kiyahudi pamoja na Yerusalemu kama eneo la pamoja. Nchi za Waarabu na za Waislamu zilipinga azimio lililopita kwa kura 33 ndiyo dhidi 13 hapana ilhali 10 hazikupiga kura. Nadani ya Palestina ilianza mara moja vita ya wenyewe kwa wenyewe kati ya kundi ta Wayahudi na Waarabu wenye silaha ilhali Wingereza waliingilia mara kadhaa tu kwa sababu waliandaa kujiondoa nchini.
Kwenye Mei 1948 ilifuata mwisho wa utawala wa Uingereza juu ya Palestina. Wayahudi walitangaza mara moja nchi yao kuwa "Dola la Israel" (Eretz Yisrael, State of Israel). Siku ileile jeshi za nchi jirani Misri, Yordani, Lebanoni, Syria na Iraki zilivamia Palestina na kushambulia maeneo ya Wayahudi waliowahi kujitetea. Katika Vita ya Palestina ya 1948-49 Waarabu walishindwa. Palestina iligawiwa kwa sehemu tatu:
- Nchi ya Israeli
- Ukingo wa Magharibi wa Yordani (West Bank) yaliyokuwa chini ya Ufalme wa Yordani
- Ukanda wa Gaza iliyotawaliwa na Misri.
Wakimbizi Wapalestina na Wayahudi
[hariri | hariri chanzo]Kati ya wakazi Waarabu 810,000 waliokaa Palestina mnamo 1948 wengi walikimbia au walifukuzwa kutoka maeneo yaliyobaki chini ya Israel. Lakini katika maeneo ambako amani iliweza kutunzwa Waarabu 168,000 walibaki waliokuwa baadaye raia Waarabu wa Israeli, takriban asilimia 15-20 za raia wote wa nchi hii.
Nchi jirani za Waarabu hawakutambua kuundwa kwa Israeli na kwa miaka ya kwanza walifuata lengo la "kuwarudisha Wayahudi baharini" siku mmoja. Wakimbizi kutoka Palestina walipangwa katika kambi zilizokusudiwa kuwa za muda lakini zipo hadi leo ilhali ziliendelea kutoka kambi za hema kuwa vijiji na mitaa ya miji penye nyumba. Lakini Yordani ilikuwa nchi ya pekee iliyoamua kuwapa Wapalestina uraia, wengine waliokaa Syria, Lebanoni, Misri na Iraki waliendelea na hali ya kukosa uraia na kuishi na vitamulisho vya Umoja wa Mataifa hadi kizazi cha tatu au nne.
Kwa upande mwingine harakati ya Wayahudi kurudi Palestina na mipango wa kugawa nchi ilichukiwa na wanasiasa wengi Waarabu pamoja na viongozi wa dini ya Uislamu kati ya Waarabu. Hii ilisababisha mashambulio dhidi ya Wayahudi wenyeji katika nchi kama Misri, Iraki, Syria au Yemen. Hapo Wayahudi wengi wa nchi hizi waliowahi kukaa huko tangu karne nyingi walikimbia katika miaka 1948 - mnamo 1960, wengi wakielekea Israeli. Idadi ya wakimbizi hao Wayahudi ikadiriwa kuwa takriban 400,000 hadi 1960. Chuki dhidi ya Wayahudi kati ya Waarabu iliendelea hivyo karibu Wayahudi wote wameondoka katika nchi hizi; isipokuwa Morokko na Tunisia ni nchi za pekee za Waarabu ambako bado Wayahudi maelfu kadhaa wamebaki. Katika nchi kama Misri na Iraki zilizokuwa na jumuiya kubwa za Wayahudi tangu siku za Biblia idadi iliyobaki ni chini ya 100.
Ilhali wakimbizi Wayahudi waliofika Israel walipokelewa katika jamii (ingawa utamaduni wao ulikuwa na tofauti nyingi na utamaduni wa Wayahudi waliotoka Ulaya) malakhi ya wakimbizi Waarabu waliendelea kuishi bila uraia. Hii ilikuwa msingi wa harakati za ukombozi wa Palestina iliyounda uadui na Israeli kwa miongo kadhaa.
Vita
[hariri | hariri chanzo]Hali ya chuki baina ya Israeli na majirani waliokataa kuitambua ilisababisha vita vifuatazo kati yao:
- Vita ya Palestina ya 1948
- Vita ya Suez 1956
- Vita ya Siku Sita ya 1967
- Vita ya Yom Kippur ya 1973
Pamoja na vita hizi kubwa kulikuwa na mashambulizi madogo madogo mpakani, mara nyingi na wanamigambo Wapalestina kutoka makambi ya wakimbizi wakisaidiwa, kuchochewa au kuvumiliwa tu na serikali ya nchi jirani. mashambulio haya yalileta mipaka ya Israeli kuimarishwa kwa fensi na kuta.
Isipokuwa mwaka 1956 majirani Waarabu walishambulia wakashindwa. 1956 Israeli ilishambulia Misri ikapaswa kurudi nyuma kufuatana na matishio ya Marekani na Urusi.
Kati ya matokeo ya vita hizi ni uvamizi wa Ukingo wa Magharibi wa Yordani na Ukanda wa Gaza tangu 1967. Pia milima ya Golan (Syria) upande wa mashariki ya Ziwa Galilaya ilivamiwa na kutawaliwa na Israeli.
Baada ya ushindi wa Israeli katika vita ya 1967 nchi za Waarabu walipatana katika azimio la Khartum ya kwamba hawatakubali kamwe amani na Israeli, hawatatambua Israeli na hawataingia katika majadiliano na Israeli.
Amani
[hariri | hariri chanzo]Lakini baada ya vita ya 1973 Marakani ilisaidia kuanzishwa mikutano kati ya Israeli na Misri iliyofikia mwaka 1978 mkataba wa amani baina Israeli na Misri. Israeli iliondoa jeshi na raia zake kwenye Rasi ya Sinai, Misri ilikubali uhuru wa meli zote kupita Mlango wa Tiran na nchi hizi mbili zilianzisha uhusiano wa kibalozi. Yordani ilifuata mwaka 1974. Kati ya majirani ya moja kwa moja Syria iliendelea kukataa Israeli. Lebanoni haikushiriki katika vita baada ya 1948 lakini haikubali Israeli ikifuata jirani kubwa.
Harakati ya Wapalestina Waarabu iliendelea kupigania uhuru. Lakini waliona ya kwamba nchi za Waarabu hawakuwa tayari kuwasaidia hali halisi kwa hiyo walianza kutafuta njia za kuelewana na Israeli. Katika mapatano ya Oslo ya mwaka 1993 baina ya Israeli na Palestine Liberation Organization (PLO) yalianzishwa Mamlaka ya Kitaifa ya Palestina yaliyotangaza "Dola la Palestina". Mamlaka yake yanahusu maeneo katika Ukingo wa Magharibi ya Yordani unaoendelea kusimamiwa na Israeli na kuwa na vijiji na miji ya walowezi Waisraeli kwa hiyo hakuna eneo kamili pamoja na Ukanda wa Gaza. Lakini mamlaka hii ina matata mengi kutokana na mafarakano baina ya vyama mbalimbali. Uongozi rasmi wa mamlaka uko upande wa PLO kwenye Ukingo wa Magharibi wa Yordani lakini Ukanda wa Gaza uko chini ya serikali ya harakati kali ya HAMAS.
Katika Israeli vyama vilivyotafuta maelewano na Wapalestina vilishindwa katika uchaguzi na kwa sasa kuna mielekeo mikali zaidi inayokazia kuingiza maeneo mengi ya Ukingo wa Magharibi ya Yordani ndani ya eneo la Israeli lenyewe na kutokubali serikali ya Kipalestina katika maeneo yanayobaki.
Kwa sasa haieleweki usuluhisho unaweza kupatikana kwa njia gani.