Nenda kwa yaliyomo

Mlangobahari wa Torres

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Torres Strait)
Mlangobahari wa Torres na visiwa vyake.
Kisiwa cha Alhamisi, katika Mlangobahari wa Torres.

Mlangobahari wa Torres ni sehemu nyembamba ya bahari kati ya Australia na Guinea Mpya. Unaunganisha Bahari ya Matumbawe upande wa mashariki na Bahari ya Arafura upande wa magharibi. Upana wake ni km 150 ukiwa na visiwa vingi na miamba tumbawe ndani yake.

Jina linatokana na nahodha Mhispania Luis Vaez de Torres aliyepita huko mwaka 1606 akiwa baharia wa kwanza aliyeshika kumbukumbu ya mapito haya kwenye ramani.

Ndani ya mlangobahari kuna visiwa 240 hivi ambavyo ni eneo la Australia, jimbo la Queensland. Kuna visiwa 17 vyenye watu. Idadi ya wakazi ni 6,800 na takriban watu 42,000 wenye asili ya visiwa hivi kwa sasa wana makazi yao Australia bara.

Utawala wa sehemu hii ya bahari pamoja na visiwa uko mikononi mwa Torres Strait Regional Authority yenye makao makuu kwenye Kisiwa cha Thursday.[1]

Mahali pa Mlangobahari wa Torres.

Jiografia

[hariri | hariri chanzo]

Mlangobahari huu ni njia muhimu ya usafiri wa meli lakini ni vigumu kupita salama kutokana na kina kifupi cha maji na idadi kubwa ya visiwa na miamba tumbawe.

Visiwa ni mchanganyiko wa aina tofautitofauti. Baadhi ya visiwa karibu na Guinea Mpya vimetokana na mchanga na matope yaliyomwagwa na mito baharini. Upande wa magharibi kuna visiwa vya miamba ambavyo ni vilele vya milima inayoanza chini ya uso wa bahari. Visiwa vingine vimejengwa na matumbawe. Upande wa mashariki wa mlangobahari kuna pia visiwa vilivyojengwa na volkeno zilizomwaga lava chini ya uso wa bahari na kukua juu yake.

Visiwa kadhaa visivyo na mwinuko mkubwa juu ya usawa wa bahari vimeona mafuriko ya mara kwa mara kutokana na kupanda kwa usawa wa bahari.

Wakazi asilia huitwa leo "Torres Strait Islanders". Ni Wamelanesia wanaofanana na Wapapua wa Guinea Mpya. Wenyeji wa visiwa hivi wana utamaduni wa pekee na historia ndefu. Walifanya biashara na Wapapua kwenye kaskazini na Waadithinngithigh wa Australia kwa maelfu ya miaka.

  1. "Torres Strait Islands". Charting the Pacific (kwa English). ABC Radio. Iliwekwa mnamo 2009-12-12.{{cite web}}: CS1 maint: unrecognized language (link)