Nenda kwa yaliyomo

Mwezi mpevu sana

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Supermoon)
Mwezi mpevu sana jinsi ulivyoonekana huko Minneapolis, Marekani tarehe 14 Novemba 2016.

Mwezi mpevu sana (pia: mwezi mpevu ajabu, kwa Kiingereza Supermoon) ni hali ya pekee ya mwezi mpevu unaotokea kila baada ya miaka kadhaa.

Hali hii inapatikana kama mwezi mpevu unatokea wakati mwezi uko karibu na dunia inavyowezekana. Hapo mwezi ni mwangavu zaidi kiasi kuliko mwezi mpevu wa kawaida.

Chanzo cha jina na ufafanuzi

[hariri | hariri chanzo]

Asili ya jina la "supermoon" si katika fani ya astronomia. Liliwahi kubuniwa na mnajimu Mwingereza Nolle mnamo mwaka 1979[1]. Nolle alidai mwezi kukaribia vile kunasababisha milipuko ya volkeno na mitetemeko ya ardhi, lakini hakuweza kuonyesha uhusiano wa kisayansi.

Mwezi mpevu ukionekana mkubwa zaidi wakati wa perijio (hali ya kuwa karibu zaidi) na ukionekana mdogo zaidi wakati wa apojio (hali ya kuwa mbali zaidi).

Kutokana na matumizi ya mara kwa mara ya jina hilo katika media, polepole wanaastronomia walianza kulitumia wakitangaza tukio la mwezi mwandamo karibu na perijio (ing. perigee-syzygy). Mnajimu Nolle alijaribu kueleza kuwa "supermoon" inatokea kama mwezi unafikia asilimia 90 za perijio lakini kuna wataalamu wa astronomia wanaopendelea kutumia jina hili pekee kama mwezi uko kweli karibu sana na perijio, yaani 98 au 99 %.

NASA ilianza kutumia jina la "supermoon" kama mwezi mpevu unatokea karibu kuliko wastani wa obiti yake. Kwa hesabu hii kuna supermoon mara kadhaa kila mwaka.[2]

Mabadiliko ya umbali wa Mwezi na Dunia 2016-2018

Umbali na uangavu wa mwezi

[hariri | hariri chanzo]

Uangavu wa mwezi mpevu unategemea umbali wake na dunia. Obiti ya mwezi unapozunguka dunia si umbo la duara bali la duaradufu ambako umbali wa mahali kwenye obiti hadi dunia kama kitovu chake unabadilika. Mahali pa karibu zaidi pa mwezi hadi dunia (perijio ing. perigee) pana umbali wa kilomita 356,410, mahali pa mbali zaidi (apojio ing. apogee) kilomita 406,740.

Mwezi mpevu wa Novemba 2016 umekaribia kilomita 356,508 kutoka dunia. Huu ni umbali mdogo tangu tarehe 26 Januari 1948. Mwezi mwandamo sana wa mwaka 2034 utakuwa karibu zaidi tena.

Si rahisi kutambua tofauti ya ukubwa kwa macho matupu bila kupima. Maana ukubwa wa mwezi mpevu unaoonekana wakati wa kuwa karibu mno (perijio) ni asilimia 14 zaidi kuliko ukubwa unaonekana wakati wa kutokea mbali zaidi (apojio); tofauti katika uangavu ni 30%.

Lakini hali hizi mbili hazifuatani kutoka mwezi mmoja hadi mwingine. Kwa hiyo ni mtazamaji hodari sana tu atakayetambua tofauti kwa macho, hasa kwa sababu uangavu halisi wa mwezi unachezacheza kutegemeana na mawingu, ukungu, vumbi au moshi hewani au pia kutokana na kuwepo kwa taa duniani jinsi ilivyo karibu na mji au hata mjini.

Mwezi na graviti yake unaathiri dunia kwa namna mbalimbali:

Kwa hiyo kama mwezi ni karibu zaidi au mbali zaidi maji kujaa hupanda kidogo juu zaidi kuliko kwenye hali ya wastani[3]. Lakini kiwango hiki ni kidogo. Madai ya wanajimu ya kwamba mwezi mpevu sana unaweza kusababisha milipuko ya volkeno au tsunami hayana msingi wa kisayansi.[4].

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
  1. http://www.astropro.com/features/articles/supermoon/, tovuti ya Bw. Nolle, iliangaliwa 13 Novemba 2016
  2. 2016 Ends with Three Supermoons, tovuti ya NASA, iliangaliwa 14 Novemba 2916
  3. Apogee and Perigee of the Moon, iliangaliwa 13 Novemba 2016
  4. Bad Astronomy « The Panic Virus Japan earthquake info » No, the "supermoon" didn't cause the Japanese earthquake Ilihifadhiwa 22 Oktoba 2019 kwenye Wayback Machine., Discover magazine, iliangaliwa 13 Novemba 2016]