Nenda kwa yaliyomo

Shilole

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Shilole
Taarifa za awali
Jina la kuzaliwaZena Yusuph Mohammed
Pia anajulikana kamaShishi Trump
Amezaliwa20 Desemba 1987 (1987-12-20) (umri 37)
Igunga, Tanzania
Kazi yakeMwimbaji, mwigizaji, mjasiriamali
Miaka ya kazi2008–hadi sasa

Zuwena Yusuph Mohammed (anayejulikana kwa jina lake la kisanii kama Shilole au "Shishi Baby" na Shishi Trump; amezaliwa 20 Disemba 1987) ni msanii wa maigizo na muziki wa kizazi kipya kutoka nchini Tanzania.[1]

Maisha ya awali

[hariri | hariri chanzo]

Shilole alizaliwa tarehe 20 Disemba wilayani Igunga, Tabora Tanzania mnamo 1987. Amelelewa na mama tu ambaye alifariki akiwa angali mdogo. Kwa sababu hiyo, Shilole alilazimika kufanya kazi mbalimbali kwa bidii ili ayashinde magumu ya maisha. Maisha ya Shilole niwa kipekee sana tofauti na wasanii wengi wa Tanzania.

Alisoma shule ya msingi Igunga mpaka darasa la saba na alifaulu kwenda Igunga sekondari ingawaje aliishia kidato cha pili baada ya kubakwa na kubeba ujauzito akiwa na umri wa miaka 14.[2]

Maisha baada ya masomo

[hariri | hariri chanzo]

Baada ya kuishia kidato cha pili alianza kujishughulisha na biashara ndogondogo kama za kuuza maji na mikate katika stendi ya Igunga, kipindi hicho akiwa na umri wa miaka 15, pia alikuwa akisambaza mikate katika nyumba za watu.

Baada ya hapo alianza kujitegemea kwa kupanga chumba chake mwenyewe kwa kulipia kodi ya shilingi 3000 kwa mwezi, alifanya hivyo kwa miaka miwili.

Kazi anazofanya sasa ni mwanamuziki na mjasiriamali.

Maisha binafsi

[hariri | hariri chanzo]

Mbali ya muziki na uigizaji Shilole vilevile ni mjasiriamali anayejishughulisha na biashara ndogondogo na za mama ntilie. Jambo ambalo sio rahisi kwa wasanii wengi wa maigizo wa Tanzania. Mgahawa wake unaitwa 'Shishi Food.[3]

Shilole ndiye msanii wa kwanza wa kike wa muziki wa kizazi kipya kupata wafuasi wengi zaidi ya milioni moja katika akaunti yake ya Instagram - kabla kuja kushika nafasi ya nne baada ya wasanii wengine kama akina Wema Sepetu ambao wameonekana kushikilia taji hilo kwa muda mrefu.[4] Vilevile Shilole ni msanii pekee wa Bongo Flava na filamu kutoka Tanzania, ambaye haioni aibu wala hajisikii vibaya kutojua kwake Kiingereza. Amekuwa mwepesi sana kutaka kujua Kiingereza na wala haoni aibu juu ya suala hilo. Vicheko na kebehi zote hazijawahi kumshughulisha kabisa.[5][6][7]

Kimaisha, Shilole na Diamond Platnumz ni wasanii ambao wanapenda sana au hawaoni tabu kuweka maisha yao halisi hadharani ukilinganisha na wasanii wengine. Shilole amepitia maisha ya dhiki mno, hadi kufikia hapa si kingine bali juhudi binafsi. Ni miongoni mwa wasanii waliolewa katika umri mdogo, kuyapita mazima madhila ya dunia hadi kuwa msanii mkubwa. Mwingi wa masihara, asiyendekeza kununa ovyo.[8]

Shilole alianza kupata umaarufu baada ya kucheza filamu ya "Fair Decision" (2010) ambayo ndani kacheza na Vincent Kigosi (Ray), Irene Uwoya, Mwanaidi Suka, Blandina Changula, Jennifer Kyaka na Jacob Stephen (JB). Filamu zingine ni pamoja na Don’t Play, Chungu ya Nafsi, Curse of Marriage, Zawadi ya Birthday na Talaka Yangu.

Baadhi ya filamu alizocheza Shilole:

Shilole hakukaa muda mrefu sana katika uwanja wa maigizo kabla kuhamia mazima katika tasnia ya muziki wa Bongo Fleva na kutoa vibao kama vile Lawama (2013), Dume Dada (2013), Paka la Bar (2013) ambazo zote zilikuwa katika muundo wa mduara. Kabla kubadili muziki wa aina hiyo na kufanya bongo fleva kamili kwa kutoa kibao kama vile, Nakomaa na Jiji (2014) wimbo ambao baadaye biti yake ilikuja kutumiwa na Queen Darleen katika wimbo wake wa Wanatetemeka, Chuna Buzi (2014), Namchuka (2015), Malele (2015), Nyang’anyang’a (2016), Say My Name (2016), Hatutoi Kiki (2016) ambayo remix yake ilitoka Aprili 2017 akishirikiana na Iyo - na Kigori (2017).

Baadhi ya nyimbo za Shilole:

  • Lawama (2013)
  • Dume Dada (2013)
  • Paka la Bar (2013)
  • Nakomaa na Jiji (2014)
  • Chuna Buzi (2014)
  • Namchuka (2015)
  • Malele (2015)
  • Nyang’anyang’a (2016)
  • Say My Name (2016)
  • Hatutoi Kiki (2016)
  • Kigori (2017)
  • Sitoi Kiki (2017)

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]
  1. "JE UNAJUA HISTORIA YA MWANADADA SHILOLE". JE UNAJUA HISTORIA YA MWANADADA SHILOLE ~ MSWAHILILEO.BLOGSPOT.COM. 2017-11-09. Iliwekwa mnamo 2022-10-18.
  2. "JE UNAJUA HISTORIA YA MWANADADA SHILOLE". JE UNAJUA HISTORIA YA MWANADADA SHILOLE ~ MSWAHILILEO.BLOGSPOT.COM. 2017-11-09. Iliwekwa mnamo 2022-10-18.
  3. Shilole aeleza kwanini mgahawa wake ameupa jina ‘Shishi Food’ (Video) katika wavuti ya Bongo5. Ingizo la February 21, 2017 .
  4. Hawa ndio mastaa 20 wa kike Bongo wenye followers wengi Instagram katika wavuti ya Bongo5. Ingizo la January 26, 2017.
  5. VIDEO: Shilole alivyoongea Kiingereza na Mashabiki Wasafi Beach Party wavuti ya Millard Ayo. Ingizo la December 26, 2016.
  6. Sipangiwi kuzungumza Kiingereza - Shilole: katika wavuti ya East Africa TV. Ingizo la 22nd Mar , 2017.
  7. Kuongea Kiingereza ni kipaji – Shilole wavuti ya Bongo5. Ingizo la May 12, 2016.
  8. SHILOLE Awavunja Mbavu Wanawake Kwenye #WonderWomen By Zamaradi Mketema Idhaa ya Dizzim Online kwenye Youtube
Makala hii kuhusu mwanamuziki/wanamuziki fulani wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Shilole kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.