Nyaraka za Kichungaji

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search

Nyaraka za Kichungaji ni kundi la maandiko ya Agano Jipya katika Biblia ya Kikristo. Jina hilo linajumlisha barua moja kwa Tito na mbili kwa Timotheo, ambao walikuwa washiriki wakuu wa kazi ya Mtume Paulo, wakawa waandamizi wake.

Wataalamu wanabishana sana kuhusu mtunzi wa barua hizo, wengi wakidhani zimeandikwa na mfuasi wa Paulo mwaka 95 hivi, huku wengine wakishikilia aliziandika mwenyewe, kwa msaada wa karani fulani, miaka ya mwisho ya maisha yake (63-67), ambapo baada ya kufunguliwa aliweza kusafiri tena mashariki (Ugiriki na nchi za kandokando) na pengine hata magharibi (Hispania).

Barua ya pili kwa Timotheo inaonekana kama wasia wake alioandika kifungoni akisubiri kuuawa.

Barua hizo zinaitwa za kichungaji kwa kuwa ziliandikwa kwa maaskofu hao ili kuwasaidia kufanya vizuri kazi zao, hasa kwa kushika imani sahihi, kupinga uzushi, kuchagua vizuri viongozi ambao wawawekee mikono, kuchunga vema Wakristo wa aina mbalimbali, kuwa na mwongozo kuhusu ibada, n.k.

Ndiyo sababu ni muhimu sana kwa miundo ya Kanisa iliyokuwa mbioni kupata sura yake ya kudumu.

Pamoja na hayo zinahimiza kukubali mateso kwa ajili ya Injili: ndio msimamo wa Mchungaji mwema (Tito 1:5-9; 2; 1Tim 1:18-2:10; 3:1-4:16; 6:2b-21; 2Tim. 1:3-14; 2:1-18; 3:14-17; 4:1-8).