Nenda kwa yaliyomo

Nebula ya Kaa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Messier 1)
Nebula ya Kaa
Nebula ya Kaa jinsi ilivyochorwa katika karne ya 19.

Nebula ya Kaa (kwa Kiingereza: Crab Nebula, inajulikana pia kwa majina kama M1, NGC 1952 au Taurus A) ni nebula katika kundinyota la Ng'ombe. Ni wingu la mabaki ya nyota nova iliyolipuka. Mlipuko wa nova ulitazamwa mwaka 1054 na kurekodiwa na wanaastronomia Wachina walioona "nyota mpya" iliyoonekana angani wakati wa mchana. Ni kiolwa cha angani cha kwanza kilichoweza kutambuliwa kuwa na asili katika mlipuko wa nyota.

Nebula iko umbali wa miakanuru 6,500 kutoka Dunia. Nebula hii ina kipenyo cha parsek 3.4 au miakanuru 11. Inaendeleea kupanuka kwa kasi ya kilomita 1,500 kwa sekunde. Mwangaza unaoonekana ni mag. 8.4, hivyo haionekani kwa macho lakini inaweza kutambuliwa kwa kutumia darubini ndogo ya mkononi.

Nebula ilitazamwa katika karne ya 18 na wanaastronomia wa Ulaya; Charles Messier aliiorodhesha kama "No. 1" katika orodha yake. Mwaka 1844 ilitazamwa na Mwingereza Parsons kwa kutumia darubini kubwa akachora umbo lake aliloona inafanana na mnyama wa kaa. Ndiyo asili ya jina "Nebula ya Kaa / Crab Nebula".

Katika miaka iliyofuata ilionekana umbo lilibadilika kiasi[1]. Kwa kulinganisha picha za nebula iliwezekana kukadiria kasi ya upanuzi wake, hivyo kukadiria pia muda tangu mwanzo wa upanuzi wake. Muda huo ulikadiriwa kuwa takriban miaka 900. Taarifa za kale kutoka China zilionyesha kwamba kule nyota mpya ilitazamwa mnamo mwaka 1054, hivyo kwenye mwaka 1928 Edwin Hubble alipendekeza nebula hiyo kuwa sawa na nyota ya 1054. Baada ya kuchungulia taarifa mbalimbali za kihistoria inaonekana nyota nova ilitokea wakati wa Aprili au Mei 1054 ikaendelea kung'aa hadi kufikia mag -7 mwezi wa Julai. Ilionekana kwa macho matupu kwa miaka miwili hivi. Baadaye mng'aro wake ulififia[2].

  1. John C. Duncan, Changes Observed in the Crab Nebula in Taurus, Proceedings of the National Academy of Sciences of the United States of America, 1921 Jun; 7(6): 179–180.1
  2. Collins, George W., II; Claspy, William P.; Martin, John C. (1999). "A Reinterpretation of Historical References to the Supernova of A.D. 1054". Publications of the Astronomical Society of the Pacific. 111 (761): 871–880. online hapa
Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Nebula ya Kaa kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.