Nenda kwa yaliyomo

Wadominiko

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Mdominiko)
Lebo ya shirika
Dominiko wa Guzmán, mwanzilishi wa Shirika la Ndugu Wahubiri
Mdominiko katika kanzu rasmi ya shirika

Wadominiko ni jina fupi linalotumka kuhusu wafuasi wote wa Dominiko wa Guzmán (1170-1221), hasa wa Shirika la Ndugu Wahubiri alilolianzisha, mojawapo kati ya mashirika ya kitawa ya Kanisa Katoliki, aina ya Ombaomba. Ufupisho wa jina la shirika ni O.P.

Historia

[hariri | hariri chanzo]

Shirika lilianzishwa na Dominiko wa Guzmán, mkanoni wa jimbo la Burgo de Osma-Ciudad de Osma: mwaka 1203 aliongozana na askofu wake Diego wa Acevedo katika safari ya kibalozi kwa niaba ya mfalme Alfonso VIII wa Castilia kwa mfalme Valdemaro II wa Denmark. Wakati wa kurudi, wakipitia mkoa wa Langadoque (Ufaransa Kusini), waling'amua uzushi wa Wakatari ulivyoenea naye akaamua kuungana na mabalozi wa Papa Inosenti III katika jitihada za kurudisha watu hao katika Kanisa Katoliki.

Akikusanya kundi dogo la wasichana walioacha Ukatari, maka 1207 alianzisha huko Notre-Dame-de-Prouille, karibu Fanjeaux, monasteri ya kike ambayo ikawa kitovu cha kazi yake ya kitume.

Dominiko aliendelea kuwahubiri kwa amani Wakatari hata baada ya balozi wa Papa Petro wa Castelnau kuuawa (1208), akikataa kujiunga na vita vya msalaba vilivyotangazwa dhidi ya Wakatari.

Kwa msaada wa askofu wa Tolosa Folco, mwaka 1215 alikusanya wenzi kadhaa wenye nya ya kuhubiri kama yeye akawaingiza katika maisha ya kitawa: shirika hilo lilipata kwanza kibali fulani cha Papa Inosenti III halafu kibali rasmi cha mwandamizi wake, Papa Onori III, tarehe 22 Desemba 1216.

Baada ya hapo Shirika la Ndugu Wahubiri lilienea kati Ulaya nzima, hasa katika miji ambapo vilikuwa vinaanza vyuo vikuu, kama vile vya Bologna na Paris, vilivyosaidiwa sana na Wadominiko kupata ustawi.

Kwa agizo la Mtaguso IV wa Laterano ndugu hao walipaswa kujichagulia kanuni iliyowahi kukubaliwa na Kanisa, wakaamua kushika ile ya Agostino wa Hippo, wakiiongezea katiba ya kwao, maarufu hasa kwa kutumia kiasi fulani cha demokrasia, ambayo ilitumiwa kama mwongozo kwa nyingine hata za kiserikali.

Ni hasa ile ya kuhubiri, ambayo wakati ule ilikuwa ya nadra, kutokana na hali ya elimu hata kati ya makasisi. Utume huo, uliokubaliwa na Papa kwa wanashirika wote, ukawa msaada mkubwa kwa Kanisa pia kwa sababu uliendana na maisha ya ufukara wa Kiinjili.

Mambo muhimu ya shirika ni:

  • Kuhubiri Injili
  • Kuishi kijumuia
  • Kuadhimisha liturujia
  • Kushika taratibu za kitawa
  • Kusoma


Tarehe 31 Desemba 2005, Shirika lilikuwa na konventi 615 zenye ndugu 6.077, ambao 4.495 kati yao ni mapadri. Mbali ya hao, kuna masista wengi wa maisha ya sala tu na wa maisha ya sala na utume. Pia kuna walei wanaofuata karama ya shirika hilo katika maisha ya kawaida.