Joyce Kiria
Joyce Kiria (alizaliwa Marangu, Mkoa wa Kilimanjaro, mnamo Desemba 1980) ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Haki za Wanawake (HAWA) na mtangazaji wa kipindi chake cha Wanawake Live kinachorushwa na EATV.
Maisha yake
[hariri | hariri chanzo]Joyce ni kifungua mimba katika familia ya Emmanuel Kiria na mkewe Tharisila Mboya, yenye watoto saba.
Mnamo mwaka 1996, alifanikiwa kupata elimu ya msingi katika Shule ya Nkonyaku mkoani Kilimanjaro. Alishindwa kuendelea na masomo ya sekondari kutokana na uwezo duni wa kiuchumi wa wazazi wake na hiyo ilimpelekea kwenda Dar es Salaam kufanya kazi za ndani kwa miaka miwili.
Halafu alipata kibarua katika kiwanda cha mablangeti ambapo hakuweza kufanya kazi kwa muda mrefu maana alikuwa anasumbuliwa na kifua kutokana na vumbi la mablangeti.
Aliamua kujiajiri katika biashara za kutengeneza sambusa na kuuza nguo Kariakoo kwa fedha alizopata wakati wa kuajiriwa. Alikuwa na ndoto ya kuwa mtangazaji maarufu, kwa hiyo aliamua kwenda redio Clouds kujitolea ili ajifunze utangazaji.
Kazi yake
[hariri | hariri chanzo]Joyce Kiria ni mtangazaji maarufu wa kipindi chake cha Wanawake Live kinachorushwa na EATV kila Alhamisi katika juma.[1] Joyce ni mpiganaji wa haki za wanawake katika kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanandoa, hasa akinamama. Anajishughulisha sana na masuala ya akinamama waliokuwa hasa na familia. Kupitia fani yake ya utangazaji, anawasaidia sana akinamama kupaza sauti zao dhidi ya ukatili wa kijinsia na kujadili changamoto zao.
Pia, Joyce ni mkurugenzi wa taasisi ya Wanawake (HAWA) ambayo inayowapatia wanawake elimu ya ujasiriamali na kuwaongoza kupata mikopo kwenye vikundi mbalimbali kupitia kaulimbiu za ndoano na mwanamke jipe shughuli. Dhumuni kubwa la michakato hii ya HAWA ni kuwawezesha akinamama ili waweze kujimudu vizuri kichumi na kuondokana na migogoro mingi ndani ya ndoa zao.