Nenda kwa yaliyomo

Farasi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Equus ferus)

Kwa habari kuhusu nyota angalia Farasi (kundinyota)

Farasi
Farasi
Farasi
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Chordata (Wanyama wenye ugwe wa neva mgongoni)
Ngeli: Mamalia (Wanyama wenye viwele wanaonyonyesha wadogo wao)
Oda: Perissodactyla (Wanyama wenye kidole kimoja au vitatu mguuni)
Familia: Equidae (Wanyama walio na mnasaba na farasi)
Nusufamilia: Equinae (Wanyama wanaofanana na farasi)
Jenasi: Equus (Farasi na punda)
Spishi: E. ferus
(Boddaert, 1785)
Ngazi za chini

Nususpishi 3:

Farasi (kutoka neno la Kiarabu فرس, faras) ni mnyama mkubwa katika ngeli ya mamalia. Wamefugwa na binadamu kwa maelfu ya miaka iliyopita. Matumizi yao ni kubeba watu au mizigo au kufanya kazi ya kuvuta magari na plau. Wamefugwa pia kwa ajili ya nyama na maziwa yao.

Aina za farasi

[hariri | hariri chanzo]

Farasi afugwaye au Farasi-kaya ni nususpishi moja ya tatu za spishi Equus ferus. Nususpishi moja nyingine inabaki sasa na hii ni farasi pekee wa porini wa kweli inayobaki (Farasi wa Pzrewalski). Farasi wa Ulaya au Tarpani amekwisha duniani. Kuna farasi wengine porini mahali pengi duniani, lakini hawa ni farasi waliofugwa zamani na walitoroka kwenye pori. Familia ya Equidae ina spishi saba nyingine, kujumuisha punda na punda milia.

Ufugaji umeleta aina nyingi za farasi; aina kubwa sana huwa na kilogramu 1,000 wakitumiwa kwa kazi nzitonzito za mashambani au msituni.

Aina nyingi zatumiwa kwa usafiri kama farasi za kupanda. Aina za pekee zimefugwa kwa michezo, kwa mfano mashindano ya mbio, mchezo wa polo, au kuruka juu ya vizuizi.

Farasi wadogo wasiofikia urefu wa 1.48 m mbegani huitwa "poni"; asili yao ni mazingira baridi na ya mlimani penye uhaba wa chakula. Hao poni walifugwa kiasili kwa kazi za kubeba watu au mizigo na siku hizi wanafugwa mara nyingi kama farasi wa burudani kwa watoto hata nje ya maeneo yao ya asili. Maarufu ni kwa mfano poni wa Shetland.

Historia

[hariri | hariri chanzo]

Asili ya farasi wote ni aina za farasi mwitu wa porini. Wataalamu huamini ya kwamba ufugaji ulianza wakati wa milenia ya tatu KK katika Asia. Utafiti wa genetiki unadokeza kuwa chanzo cha ufugaji wa farasi mwitu kilitokea mahali mbalimbali, si mahali pamoja tu.

Mnamo mwaka 2000 KK matumizi ya farasi yameshasambaa kwenye sehemu kubwa ya mabara ya Asia na Ulaya.

Makabila na mataifa waliotumia farasi walikuwa na faida katika shughuli za usafiri na vita. Baadaye iligunduliwa pia kwamba farasi anaweza kusaidia kwenye shughuli za kilimo kama kuvuta plau.

Farasi waliwezesha watu kuvuka haraka maeneo makubwa ya savana za Asia. Makabila ya wahamiaji walitumia farasi.

Wanyama hawa walibadilisha pia uso wa vita. Picha kwenye majengo ya Babeli, Mesopotamia na Misri ya Kale zinaonyesha jinsi gani magari yaliyovutwa na farasi yalivyobeba wanajeshi wawili au watatu. Magari haya yalihofiwa sana. Baadaye maendeleo ya teknolojia ya viti ya farasi yalisababisha kutokea kwa wanajeshi wa kupanda walioweza kushambulia kwa vikosi vikubwa.

Mahitaji ya vita yalisababisha pia ufugaji wa aina nzito sana za farasi walioweza kumbeba askari aliyevaa kinga ya feleji mwilini pamoja na silaha zake.

Farasi walikuwa usafiri mkuu wa wanajeshi hadi karne ya 19. Kutokea kwa reli kuliwezesha usafiri wa haraka wa askari wengi katika nchi za Ulaya na Amerika ya Kaskazini. Hata hivyo katika maeneo mengi ya dunia ni farasi waliobeba watu na mizigo ya jeshi.

Kilimo cha Ulaya kilitegemea hasa farasi tangu zama za kati na kugunduliwa kwa mbinu za kufunga plau kwenye mabega ya mnyama bila ya kukaza shingo lake. Kugunduliwa kwa teknolojia hii kulisababisha kupanda kwa mazao Ulaya na kuongezeka kwa watu.

Makala hii kuhusu mnyama fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Farasi kama uainishaji wake wa kibiolojia, maisha au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.