Carl Gotthilf Büttner

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Carl G. Büttner na mhadhiri wa Kiswahili Suleiman ben Said huko Berlin mnamo 1890/91.

Carl Gotthilf Büttner (Königsberg, 24 Desemba 1848 - Berlin, 14 Desemba 1893) alikuwa mchungaji wa Kiprotestanti, mmisionari na mtaalamu wa lugha kutoka Ujerumani.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Carl Gotthilf Büttner alisoma theolojia kwenye Chuo Kikuu cha Königsberg kisha akajiunga na Rheinische Missionsgesellschaft huko Barmen alipopata mafunzo ya umisionari. Kuanzia mwaka 1873 hadi 1880 alikuwa mmisionari kati ya Wanama na Wadamara katika maeneo yaliyokuwa baadaye koloni la Afrika Kusini Magharibi ya Kijerumani (leo: Namibia). Uwezo mkubwa wa Büttner ulikuwa zaidi katika taaluma za lugha.

Alitafsiri Agano Jipya katika lugha ya Waherero akatunga vitabu kuhusu lugha ya Kiherero. Mnamo 1880 alirudi Ujerumani, ambapo alikuwa mchungaji katika mji mdogo wa Wormditt huko Prussia Mashariki.

Kutokana na maarifa yake ya pekee ya nchi na lugha ya Namibia, alitumwa na serikali ya Ujerumani kama mwakilishi wa serikali kwenda tena huko mnamo 1885 kwa maagizo ya kuhitimisha mikataba ya urafiki na ulinzi na watawala wenyeji. Safari hiyo ilianza tarehe 23 Aprili 1885 kutoka Southampton (Uingereza) kufika 22 Septemba 1885 huko Okahandja, alimpeleka katika nchi ya Wanama, Wabaster na Waherero.

Aliporudi alipokewa na chansela Otto von Bismarck akapewa Tuzo la Tai Nyekundu (Roter Adlerorden), daraja la nne.

Baada ya kurudi, Büttner alichukua nafasi ya katibu (Inspektor) wa Shirika la Misioni kwa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani (Deutsch-Ostafrikanische Missionsgesellschaft) iliyoanzishwa mwaka 1886 baada ya kuanzishwa kwa koloni la Kampuni ya Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki katika sehemu za Tanganyika. [1] Lakini baada ya kukosoa vikali jinsi Kampuni ilivyowatenda wenyeji, Buettner alifukuzwa madarakani mnamo 1889.

Baadaye Büttner alifanya kazi kama mwalimu wa Kiswahili katika Semina ya Lugha za Mashariki huko Berlin alipotunga vitabu kadhaa juu ya lugha ya Kiswahili. Chuo Kikuu cha Königsberg kilimpa udaktari wa heshima mnamo 1888 kwa kazi yake ya kitaaluma.

Heshima na Tuzo[hariri | hariri chanzo]

  • Roter Adlerorden 4. Klasse (1886)
  • Daktari wa heshima kutoka Chuo Kikuu cha Königsberg (1888)

Vitabu na maandiko yake[hariri | hariri chanzo]

  • "A South African Arcadia" in Popular Science Monthly, 22 (March 1883)
  • "Domestic Arts in Damaraland" in Popular Science Monthly, 26 (November 1884)
  • "Medical Practice in Damaraland" in Popular Science Monthly, 28 (February 1886)
  • Kolonialpolitik und Christentum betrachtet mit Hinblick auf die deutschen Unternehmungen in Südwestafrika (Siasa ya kikoloni na Ukristo, zikitazamwa kwenye mfano wa jitihada za Kijerumani katika Afrika ya Kusini-Magharibi), 1885
  • Worterbüch der Suahelisprache: Suaheli-Deutsch und Deutsch-Suaheli (Kamusi ya lugha ya Kiswahili, Kisahili-Kijerumani na Kijerumani Kiswahili), 1890
  • Suaheli-Schriftstücke in arabischer Schrift: mit lateinischer Schrift umschrieben übersetzt und erklärt, W. Spemann, 1892 (Hati za Kiswahili kwa maandishi ya Kiarabu, kutolewa pia kwa maandishi ya Kilatini na kutafsiriwa)
  • Lieder und Geschichten der Suaheli (Nyimbo na hadithi za Waswahili), 1894

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Teltower Kreisblatt vom 19. Dezember 1893, S. 2.