Al-Ghazali

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Abu Hamid Muhamad ibn Muhamad al Ghazali
Al Ghazali
Alizaliwa mnamo 1058 BK (450 AH)
Alikufa mnamo 1111 BK (505 AH)
Nchi Uajemi (Milki ya Waselchuki)
Kazi yake Mwanafalsafa, mwanatheolojia, mwanasheria wa Kiislamu

Abū Ḥāmid Muḥammad ibn Muḥammad al-Ghazālī (1058-1111) (Kiarabu:ابو حامد محمد ابن محمد الغزالی) kwa kifupi Al Ghazali, alikuwa mwalimu mashuhuri wa dini, falsafa na sheria ya Kiislamu. Anahesabiwa kati ya walimu wa dini muhimu zaidi katika historia ya Uislamu.

Maisha yake[hariri | hariri chanzo]

Alizaliwa mjini Tus katika jimbo la Khorasan la Uajemi. Pamoja na mdogo wake Ahmad alilelewa kama watoto yatima. Kijana alifundishwa sharia ya kiislamu akaendelea kuwa mwanafunzi wa mwanasheria wa Shafii ʿAbd-al-Malek Jovayni mjini Nishapur aliposoma pamoja na mwalimu Msufi. Baada ya kifo cha walimu wake alipata ajira kwenye ikulu ya waziri Nezam-al-Molk aliyewahudumia watawala Waselchuki . Waziri alimfanya profesa wa sharia huko Baghdad alipofundisha kufuatana na madhhab ya Shafii.

Mnamo mwaka 1095 Al Ghazali alishambuliwa na mashaka makali kutokana na masomo yake katika falsafa ya Kiislamu akaacha nafasi yake ya ualimu. Alikatishwa tamaa pia kutokana na rushwa kati ya walimu wa chuo chake. Wakati ule ilikuwa vigumu kutoka katika utumishi wa mtawala kwa hiyo aliomba rukhsa kuhiji Makka.

Miaka 11 iliyofuata hadi mwaka 1106 hakuna habari za hakika kuhusu shughuli zake. Katika kitabu alichoandika juu ya maisha yake mwenyewe Al Ghazali anasimulia jinsi gani alivyoguswa na nuru kutoka Allah iliyomrudisha hakika ya imani. Katika kitabu hiki anataja kipindi cha kufundisha kwenye madrasa huko Dameski, baadaye safari ya kutembelea kaburi la Abrahamu huko Hebron mnamo 1096. Hapa alitoa kiapo kutopokea pesa ya serikali tena, kamwe kumhudumia mtawala yeyote na kutoshiriki katika mashindano ya majadiliano ya kitaalamu tena.

Baada miaka hii ya kuzunguka kwa namna ya Wasufi alianza kufundisha tena kama profesa wa sharia huko Nishapur kwa miaka kadhaa. Baadaye alirudi kwake nyumbani mjini Tus alipokuwa na maisha kimya na kufundisha kibinafsai kama walimu Wasufi.

Mafundisho[hariri | hariri chanzo]

Al Ghazali alifahamu vizuri sana mapokeo ya falsafa kuanzia Wagiriki wa Kale na ya theolojia ya Kiislamu.

Kujisomea falsafa ilikuwa ikamleta katika kipindi cha mashaka. Katika kipindi cha maisha yake kama Msufi alirudi kwa imani akaandika kitabu cha kueleza mipaka ya falsafa. Alikataza falsafa kama njia ya kufikia ukweli. Akapinga watangulizi wake kama Avicenna na Alfarabi akisema hao waliharibu inami ya Kiislamu kwa kutumia mno matokeo ya Aristoteli na Platon. Alisisitiza ya kwamba mantiki haiwezi kumweleza Mungu aliye mkubwa kuliko akili ya kibinadamu.

Alipinga pia wenzake waliofundisha ulimwengu kuwa milele akitetea dhana ya uumbaji.

Maandiko yake kuhusu Usufi yalikuwa muhimu kwa kuleta kiwango cha upatanishao kati ya theolojia ya Kiislamu na harakati ya Wasufi. Alionyesha jinsi gani mazoezi ya Wasufi yanaweza kulinganishwa na kanuni za sharia akieleza desturi zao kwa undani. Kwa njia hii aliweza kupunza uadui ya ulema dhidi ya Wasufi.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu: