Boma la Kale, Dar es Salaam

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Boma la Kale ni jengo la kihistoria mjini Dar es Salaam. Pamoja na Atiman House iko kati ya majengo mawili yaliyobaki na vyanzo wa mji huu tangu nayakati zilizotangulia ukoloni wa Kijerumani[1].

Nyumba ya wageni kabla ya ukoloni[hariri | hariri chanzo]

Nyumba hiyo ilijengwa mwaka 1866 wakati Sultani Sayyid Majid bin Said aliamua kuanzisha makao mapya barani baada ya kuchoka maisha ya kule Zanzibar akaita jumba jipya "Dar es Salaam" yaani "jumba la amani, utulivu". Jumba la Sultani lilijengwa pamoja na majengo mengine na Boma la Kale la leo lilikuwa nyumba ya kupokelea wageni wa Sultani.

Jinsi ilivyokuwa kawaida katika ujenzi wa nyumba za Waswahili wenye uwezo, kuta zilijengwa kwa kutumia mawe ya matumbawe; kwa ghorofa dari ilitengenezwa kwa kufunga nafasi kati ya kuta kwa magogo ya mikoko yenye ubao ambao huliwi na wadudu. Kwa hiyo urefu wa mikoko iliyopatikana iliamulia upana wa vyumba, ambao ni takriban mita 3.

Kuimarishwa wakati wa Vita ya Abushiri[hariri | hariri chanzo]

Baada ya kifo cha Sayyid Majid, alifuatwa na Sayyid Barghash ambaye hakupenda kuendelea na mradi wa makao mapya, hivyo majengo yalikaa tu.

Mwaka 1888 sultani mpya Sayyid Khalifa aliamua kukodisha mamlaka juu ya pwani ya Tanganyika kwa Kampuni ya Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki. Kampuni ilinunua majengo ya sultani ya Dar es Salaam pamoja na Boma la Kale na kuyatumia kama ofisi na makazi.

Mwaka uliofuata wenyeji wa pwani walipinga majarabio ya kampuni hii kuchukua mamlaka ya kiutawala mikononi mwake. Katika Vita ya Abushiri vituo vya Wajerumani vilishambuliwa mahali pengi kuanzia Septemba 1888. Baada ya kupokea habari hizi kwenye kituo cha Dar es Salaam nyumba hii iliunganishwa kwa ukuta pamoja na jengo jirani na hivyo kuimarishwa kuwa ngome. Kuanzia mwezi Desemba 1888 kulikuwa na mashambulio dhidi ya Dar es Salaam.[2]. Katika boma hili Wajerumani waliweza kujitetea kwa msaada wa wanamaji kutoka manowari SMS Möwe hadi kufika kwa jeshi la kikoloni la Schutztruppe kwenye Mei 1889.

Matumizi ya kiofisi wakati wa ukoloni[hariri | hariri chanzo]

Utawala wa Kampuni ya Kijerumani uliporomoka katika vita ya Abushiri na sasa serikali ya Berlin iliingia kati na kuchukua utawala moja kwa moja mikononi mwake. Makao makuu yalihamishwa kutoka Bagamoyo pasipo bandari kwa meli kubwa kwenda Dar es Salaam penye bandari nzuri. Boma la Kale liliendelea kutumiwa kama kituo cha forodha na baadaye kama gereza lenye wafungwa Waafrika hadi 200.[3]

Wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia Dar es Salaam ilivamiwa na jeshi la Uingereza kwenye mwaka 1916. Tanganyika iliendelea kuwa chini ya Uingereza na Dar es Salaam kuwa mji mkuu. Boma la Kale lilikuwa kituo cha polisi hadi uhuru wa nchi tarehe 9 Desemba 1961.

Urithi wa Kitaifa wa Tanzania[hariri | hariri chanzo]

Baada ya uhuru polisi ilihamia majengo mapya. Boma la Kale lilitumiwa kwa ofisi mbalimbali za serikali. Mnamo 1980 kulikuwa na mipango ya kobomoa nyumba lakini wananchi wengi wa mji walitetea jengo hilo la kihistoria. Mwaka 1995 liliandikishwa katika orodha ya kumbukumbu ya urithi wa kitaifa.

Tangu mwaka 2014 taasisi ya Dar es Salaam Centre for Architectural Heritage (DARCH) iliweza kupatana na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuhusu mipango ya ukarabati na matumizi ya Boma la Kale. Hivyo tangu mwaka 2017 Boma la Kale ni kituo cha kiutamaduni chenye programu na maonyesho kuhusu historia na urithi wa Dar es Salaam, mazingira, uchumi na mshikamano wa kijamii wake.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Sutton, J.E.G. (1970). "Dar es Salaam: a sketch of a hundred years". Tanzania Notes and Records (71): 4–5
  2. H.F. von Behr, Kriegsbilder aus dem Araberaufstand in Deutsch-Ostafrika, Leipzig 1891, uk 99 (online hapa kwenye archive.org)
  3. Bericht über die Bekämpfung der Malaria unter den Eingeborenen in Dar es Salaam, Medizinal-Berichte über die deutschen Schutzgebiete für das Jahr 1904/05, uk. 26 (online hapa)

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]