Nyasa (ziwa)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Ziwa la Nyassa)
Jump to navigation Jump to search
Mstari mwekundu unaonyesha mpaka usiokubaliwa kati ya Tanzania na Malawi. Tanzania inadai mstari mwekundu kuwa sahihi, lakini Malawi inadai ziwa lote hadi mwambao wa Tanzania. Mpaka kati ya Msumbiji na Malawi hauna matata.

Ziwa Nyasa (katika Malawi: Lake Malawi; katika Msumbiji: Niassa) ni kati ya maziwa makubwa ya Afrika ya Mashariki likiwa na nafasi ya tatu baada ya Viktoria Nyanza na Ziwa Tanganyika.

Lina urefu wa km 560 na upana wa km 50-80. Vilindi vyake vinaelekea hadi mita 704 chini ya uwiano wa maji yake.

Ziwa Nyasa linapatikana kati ya nchi za Malawi, Msumbiji na Tanzania.

Kusini mwa ziwa unatoka Mto Shire unaopeleka maji kwenye Mto Zambezi na hatimaye Bahari Hindi.

Kijiolojia ziwa ni sehemu ya Bonde la Ufa la Afrika ya Mashariki.

Ziwa Nyasa linajulikana kuwa na aina nyingi za samaki (zaidi ya 1500). Aina chache tu zinavuliwa kama chakula, lakini aina mbalimbali zinakamatwa na kuuzwa nje ya Afrika kwa wapenzi wa samaki wa rangi.

Eneo la Ziwa

Eneo la ziwa ni km² 29,600. Sehemu kubwa ni eneo la Malawi, ila robo ya kusini-mashariki ni eneo la Msumbiji, na robo ya kaskazini-mashariki ni eneo la Tanzania.

Kuna ugomvi kati ya Malawi na Tanzania kuhusu mipaka. Malawi imedai ya kwamba maji yote hadi ufukoni upande wa Tanzania ni sehemu ya eneo lake la kitaifa. Tanzania imedai ya kwamba mpaka uwe katikati kufuatana na desturi za kimataifa.

Sababu ya mzozo ni utaratibu wa kikoloni. Wakati wa kuundwa kwa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani serikali za Uingereza na Ujerumani zilipatana kuhusu mipaka ya eneo la Kijerumani kwa kutaja mpaka ulifuata ufuko wa Ziwa Nyasa.[1]

Baada ya mwaka 1919 Uingereza ilitawala Tanganyika pamoja na Malawi (Nyassaland), hivyo hakukuwa na shida.

Kumbe, baada ya uhuru Malawi ilitaka kutumia historia hii kama haki yake ya kitaifa. Polisi yake ilijaribu kutawala wavuvi na feri za Tanzania ziwani. Mzozo huu ulisababisha risasi kufyatuliwa.

Hadi leo hakuna mapatano rasmi lakini nchi zote mbili zinaendelea bila kutumia nguvu. Hali halisi Malawi imeheshimu dai la Tanzania, haijasumbua tena wavuvi wala feri za jirani ndani ya robo ya kaskazini-mashariki ya ziwa.

Mzozo ulifufuka tena tangu mwaka 2012 baada ya Malawi kutoa vibali vya upelelezi wa gesi na mafuta chini ya ziwa, tendo linalopingwa na Tanzania.[2]

Marejeo

  1. "In East Africa, Germany's sphere of influence is demarcated thus: ... To the south by the line that starts on the coast of the northern border of Mozambique Province and follows the course of the Rovuma River to the point where the Messinge flows into the Rovuma. From here the line runs westward on the parallel of latitude to the shore of Lake Nyasa. Turning north, it continues along the eastern, northern, and western shores of the lake until it reaches the northern bank of the mouth of the Songwe River. " (Anglo-German Treaty (Heligoland-Zanzibar Treaty) (July 1, 1890), article I,2, tovuti ya http://germanhistorydocs.ghi-dc.org, mradi wa German Historical Institute Washington, DC, iliangaliwa Machi 2019
  2. Malawi: Old Border Dispute With Tanzania Over Lake Malawi Flares Up Again
Africa satellite plane.jpg Makala hii kuhusu maeneo ya Afrika bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Nyasa (ziwa) kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.