Nenda kwa yaliyomo

Yataka Moyo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
"Yataka Moyo"
"Yataka Moyo" kava
Wimbo wa Professor Jay

kutoka katika albamu ya Machozi Jasho na Damu

Umetolewa 2001
Umerekodiwa 2001
Aina ya wimbo Hip hop
Urefu 4:21
Studio Bongo Records
Mtunzi Professor Jay
Mtayarishaji P. Funk
Machozi Jasho na Damu orodha ya nyimbo
  1. A1 - Ndio Mzee
  2. A2 - Jay Jr. Interlude
  3. A3 - Jina Langu
  4. A4 - Bongo Dar Interlude
  5. A5 - Bongo Dar es Salaam
  6. A6 - Yataka Moyo
  7. A7 - Nawakilisha
  8. B1 - Intro
  9. B2 - Machozi Jasho Na Damu
  10. B3 - Piga Makofi
  11. B4 - Niamini
  12. B5 - Salamu Bibi Na Babu
  13. B5 - Tathimini Interlude
  14. B6 - Tathimini
  15. B7 - Na Bado
  16. B8 - Outro

"Yataka Moyo" ni jina la wimbo wa sita upande A kutoka katika tepu ya albamu ya Machozi Jasho na Damu ya msanii wa muziki wa hip hop kutoka nchini Tanzania, Professor Jay. Wimbo umetayarishwa na P. Funk ndani ya Bongo Records.

Kwa ujumla wake Jay anazungumzia mafanikio ya sanaa na wasanii. Katika muziki wa Tanzania imeonekana kawaida sana kwa wasanii na wanamuziki kutokuwa na kipato kinachoeleweka. Mifumo isiyosaidizi kwa tasnia nzima ya muziki wa Tanzania.

Ubeti wa kwanza

[hariri | hariri chanzo]

Jay anazungumzia wasanii wa zamani jinsi walivyoteseka katika kuuleta muziki wa Tanzania katika ramani inayoeleweka. Tena wengi wao wanakufa maskini huku kazi zao zikitumiwa na taasisi za serikali na watu binafsi bila faida kwa msanii. Wanaomba hakimiliki ya kazi za sanaa zao lakini majibu bado magumu. Katika wimbo anataja watu wengi maarufu tangu muziki wa rap ulivyoanza, hadi makuzi ya muziki wa dansi.

Anakemea tabia ya serikali kutaka wasanii wadumishe mila zao katika sanaa huku mazingira mabovu ya kutunza hadhi na kazi za wasanii ni hafifu. Katika ubeti wa kwanza anamtaja Marijan Rajabu kama mfano wa mkuu jinsi sanaa ya Bongo isivyolipa. Marijan alihangaika na muziki na kuvumilikia mikikimikiki, lakini kafa maskini kabisa. "Marijan Rajabu, tulimwita jabari la mziki,
Alifanya maajabu, alivumilia mikikimikiki,
Kinachonipa ghadhabu, bwana sanaa ya Bongo halipi,
Tofauti na chati yake ndugu yetu amekufa na dhiki.

Anauliza sasa inakuwaje? Hii inasababishwa na viongozi kuwa na tamaa na kutoridhika na vipato vyao. Hapa alimaanisha ya kwamba kila juhudi za kudai hakimiliki kwa wasanii viongozi wanapewa hongo na wadau wanaojiita wasambazaji wa muziki. Kundi hili la wasambazaji ndilo hasa linafonufaika na muziki kuliko hata wasanii wenyewe. Kumekuwa na malalamiko mengi dhidi ya udanganyifu wa nakala za kanda zinatolewa na msambazaji. Msambazaji anamsainisha nakala labda 5,000 lakini hali halisi msambazaji anachapisha nakala hata mara kumi yake na kuzisambaza nje ya mji ili tu msanii asione kazi yake jinsi inavyoibwa.

Jay anatoa wazo la kuunda "Umoja wa Wasanii" kama njia madhubuti ya kudhibiti walanguzi na matapeli wa usambazaji. Hivyo ndivyo anavyomaliza na ubeti wa kwanza.

Ubeti wa pili

[hariri | hariri chanzo]

Hapa anaanza na Nico Zengekala (mwanamuziki kutoka Mombasa, Kenya aliyeingia Tanzania mwaka 1982) na kutamba kwa wimbo wa "Solemba" alioimba na bendi ya Juwata Jazz Band. Anamwambia awape salamu huko kuzimu huku Bongo bado wanafanya zindiko, yaani, hali si hali, chenga tu. Mambo kama zamani udhulumati unaendelea bila majibu yanayoeleweka.

Kisha anataja wasanii wengine maarufu nchini Tanzania, hasa wale wa miaka ya 1980 na 1990 - kama vile: Hard Blasters Crew, Sikinde, Remmy Ongala, Alca Paino, Underground Souls ya kina Imam Abbas, Gangwe Mobb, IK Kimara (IK ni kirefu cha Immeditation Kingdom - tazama "Taff B. kwa maelezo zaidi), Ottu Jazz Band, Ugly Faces. Jay analalamikia kutoungwa mkono kwa wasanii na soko limekuwa bovu kabisa. Walio wengi hawana pesa na wakizipata hawafanyii cha maana zaidi ya kunywa bia na kufanya ngono. Hasa kutokana na kipato chenyewe cha muziki kuwa hafifu kuliko mahitaji halisi. Isitoshe hata masoko ya nje serikali imekaa kimya na hao wanaojiita mapromota wengi wamekuwa matapeli na si vinginevyo.

Ubeti wa tatu

[hariri | hariri chanzo]
Kipande cha mwisho cha Yataka Moyo na kiitikio chake.

Ubeti huu, anazungumzia jinsi wasanii wa Bongo walio wengi hawajui maisha yao ya sasa, bado wanaishi katika maisha ya UJIMA. Jay anataka msanii apate japo hela ya kujikimu kimaisha na si lazima apate pesa za kununua gari zuri. Walau kipato chao kiendane na juhudi wanazofanya. Kwa wakati ule, suala la msanii kuvuma maredioni lakini mfukoni hana kitu lilikuwa jambo la kawaida. Nia ya dhati hasa ni kuifanya sanaa ya Bongo iwe ajira ilimradi kupunguza wimbi vibaka na watu wasio na kazi. Sanaa iwe sehemu ya ajira rasmi ambayo serikali inaitambua.

Kama kawaida mbele kidogo anataja watu mashuhuri waliofanikisha sanaa ya Bongo katika nyanja mbalimbali kuanzia, urembo, muziki, maigizo, uchoraji na mengine mengi. Waliotajwa ni pamoja na marehemu Mzee Jongo, Irene Ngowi, Miikka Mwamba, Solo Thang, Mr. Paul, Caz T, Taff B., Mzee Onyango, Masoud Kipanya, Oscar Makoye, African Stars, Tatu Nane, Vijana Jazz Band, Mr. II, KU Crew, Fid Q, Soggy Doggy, Mad Brain, Xplastaz, Juma Nature, Manzese Crew, SOS B, Killa B, Steve B, Master T, P. Funk, Master Jay, Ludigo, DJ JD, Bonny Luv, John Mahundi na Mack D. Katika ubeti huu Jay anasisitiza wasanii wote waungane, iwe wa muziki wa dansi au namna gani. Anaona mshikamano ni jambo jema litakaloondoa matatizo yao katika sanaa. Kutosana na kuwekeana mizengwe si jambo jema.

Viungo vya Nje

[hariri | hariri chanzo]