Nenda kwa yaliyomo

Chawa-mbao

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Oniscidea)
Chawa-mbao
Chawa-mbao (Ligia oceanica)
Chawa-mbao (Ligia oceanica)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye mwili wa pingili na miguu ya kuunga wasio na ugwe wa mgongo)
Nusufaila: Crustacea (Gegereka: Arithropodi walio na kiunzi-nje chenye kaboneti ya kalisi)
Ngeli: Malacostraca
Oda ya juu: Peracarida
Oda: Isopoda
Latreille, 1817
Nusuoda: Oniscidea
Latreille, 1802
Ngazi za chini

Oda za chini 2, sectio 4:

Chawa-mbao (kutoka Kiing. woodlouse) ni arithropodi wa nusuoda Oniscidea katika oda Isopoda ya nusufaila Crustacea ambao wana miguu 14. Ingawa watu wengi wanafikiri kwamba chawa-mbao ni wadudu, kwa kweli ni gegereka. Ilhali gegereka wengi sana huishi majini (bahari na maji baridi), chawa-mbao, warukaji-mchanga (oda Amphipoda) na spishi fulani za kaa (oda Decapoda) hupatikana nchini kavu. Spishi za makundi mawili ya kwanza zinapendelea mahali panyevunyevu, mara nyingi karibu na maji. Spishi nyingi za chawa-mbao zinaweza kujiviringa katika umbo la tufe na kwa hivyo huitwa wadudu-donge.

Chawa-mbao ni wadogo kulingana na gegereka wanaojulikana sana. Wengi wana urefu wa karibu na sm 1 lakini wanaweza kuwa na urefu wowote kati ya sm 0.3 na 3. Kwa kawaida mwili wao ni bapa juu-chini (mpana kuliko kimo chao). Rangi yao inaweza kutofautiana kutoka kijivu hadi nyeupe au kahawia na wakati mwingine kuna madoa mekundu au zambarau.

Chawa-mbao wana kiunzi-nje chenye khitini kilicho na pingili 13 na jozi 7 za miguu ya kuunga. Kama Isopoda wote, wanakosa gamba dhahiri (carapace) lakini hilo hupunguzwa kwa "ngao ya kichwa" inayofunika kichwa tu. Hii inamaanisha kuwa miundo kama matamvua, ambayo inalindwa chini ya gamba katika makundi mengine yaliyo na nasaba nao, hupatikana kwenye viungo maalum vya fumbatio (angalia chini). Mgongo wa mdudu hufunikwa kwa safu ya mabamba yanayoungana na kulaliana ambayo hutoa kinga na pia kutoa mnepo.

Maumbile ya mwili yana kichwa, kidari (pereo) chenye pingili nane (pereoniti) na fumbatio (pleo) yenye pingili sita (pleoniti). Kichwa huungana na pingili ya kwanza ya kidari zikiunda kefalo. Kuna jozi moja ya vipapasio bila matagaa na jozi moja ya vibaki vya vipapasio, ambavyo vimekua vizima katika Isopoda wanaoishi majini. Macho ni ambatani na hayana kikonyo na sehemu za kinywa ni pamoja na jozi ya maksilipedi na jozi ya mandibuli (mataya) zenye palpi (viungo vyenye pingili vilivyo na kazi ya hisia).

Kila moja ya pingili saba huru za kidari hubeba jozi ya pereopodi (miguu). Katika spishi nyingi sana hizi hutumika kwa kusogea na ukubwa, mofolojia na mwelekeo zao ni sawa sana, ambayo inapatia oda hii jina lake la "Isopoda", kutoka kwa Kiyanuni “miguu sawa”. Katika spishi chache jozi ya mbele hutoholewa kuwa gnathopodi zilizo na pingili za mwisho kama magando yashikayo. Pereopodi hazitumiki kupumua kama ilivyo katika oda nyingine kadhaa, lakini koxa (pingili za kwanza) huungana na tergiti (mabamba ya mgongo) ikiunda epimera (mabamba ya upande). Katika wapevu wa kike viungo kadhaa au vyote vina viambatisho vinavyojulikana kama oostegiti ambazo hukunjwa chini ya kidari na kuunda chumba cha kuatamia mayai. Katika madume gonopori (midomo ya uzazi) ziko kwenye uso wa chini wa pingili ya nane na katika majike ziko katika mahali sawa kwenye pingili ya sita.

Pingili moja au zaidi za fumbatio, kuanzia na pigili ya sita, zimeungana na telsoni (sehemu ya mwisho) kuunda pleotelsoni ngumu. Kila moja ya pingili tano za kwanza za fumbatio hubeba jozi ya pleopodi zenye matagaa mawili, miundo kama mabamba ambayo hufanya kazi ya kubadilisha gesi, na pingili ya mwisho inabeba jozi ya uropodi (viungo vya nyuma) zenye matagaa mawili. Katika madume jozi ya pili ya pleopodi hutoholewa ili kutumika katika uhamishaji wa manii. Endopodi (matagaa ya ndani ya pleopodi) hutoholewa kuwa miundo yenye kutikula (vifuniko vya nje vya kinamo) nyembamba inaoweza kupenyeka na ambayo inawezesha kubadilisha kwa gesi. Hizi huitwa mapafu ya pleopodi.

Chawa-mbao wana kiunzi-nje ambacho lazima kuambuliwa hatua kwa hatua wanapokua. Uambuaji hufanyika katika hatua mbili: nusu ya nyuma hupotea kwanza ikifuatiwa siku mbili au tatu baadaye na kipande cha mbele. Njia hiyo ya kuambua ni tofauti na ile ya arithropodi wengi sana ambao huambua kutikuli yao kwa mchakato mmoja.

Chawa-mbao wa kike huweka mayai yaliyotungishwa katika mfuko wa kuatamia kwenye upande wa chini wa mwili wake. Lava wanaoibuka hukua ndani ya mfuko huo, ambapo hupewa maji, oksijeni na lishe. Wanapitia maambuaji kadhaa na ule wa mwisho hutoa lava afananaye na mpevu mdogo anayeitwa manka (manca). Kwa hivyo mama anaonekana "kuzaa" watoto wake. Pengine manka hupokea huduma zaidi ya mamao. Wanaambua mara kadhaa zaidi hadi kuwa wapevu. Majike wa spishi fulani wanaweza kuzaa pia bila kutungishwa.

Licha ya kuwa gegereka kama kaa na kamba inasemekana kwamba chawa-mbao wana ladha mbaya kama "mkojo mkali".

Spishi zilizochaguliwa za Afrika ya Mashariki

[hariri | hariri chanzo]
  • Aethiopopactes chenzemae
  • Aethiopopactes marmoratus
  • Benechinus armatus
  • Ctenorillo buddelundi
  • Ctenorillo kenyensis
  • Diploexochus jeanneli
  • Eubelum breviantennum
  • Eubelum instrenuum
  • Gelsana abnormis
  • Hiallum affine
  • Hiallum richardsoni
  • Ignamba brevis
  • Ignamba microps
  • Kenyoniscus paradoxus
  • Ligia malleata
  • Ligia pigmentata
  • Mesarmadillo flavescens
  • Mesarmadillo giganteus
  • Microcercus armadilloides
  • Microcercus pseudanomalus
  • Myrmecethelum camponotorum
  • Oropactes frontelobatus
  • Oropactes maculatus
  • Periscyphis brunneus
  • Periscyphis montanus
  • Periscyphis pallidus
  • Periscyphis ruficauda
  • Periscyphops minimus
  • Periscyphops nigricans
  • Phalaba brevis
  • Phalaba dorkai
  • Pseudoaethiopopactes kohleri
  • Pseudodiploexochus lobatus
  • Pseudodiploexochus pilosus
  • Pyrgoniscus emarginatus
  • Pyrgoniscus lanceolatus
  • Rufuta arganoi
  • Rufuta carusoi
  • Stegosauroniscus horridus
  • Synarmadillo pygmaeus
  • Synarmadillo villosus
  • Synarmadilloides pila
  • Thermocellio kenyensis
  • Thermocellio kilimanjarensis
  • Tritracheodillo spatulatus
  • Tylos africanus
  • Venezillo bituberculatus
  • Venezillo glomus
  • Uramba marginalis
  • Uramba triangulifera
Makala hii kuhusu "Chawa-mbao" inatumia neno (au maneno) ambalo si kawaida na matumizi yake ni jaribio la kutafsiri neno (au maneno) la asili woodlouse kutoka lugha ya Kiingereza. Neno (au maneno) la jaribio ni chawa-mbao.
Wasomaji wanaombwa kuchangia mawazo yao kwenye ukurasa wa majadiliano ya makala.

Kamusi za Kiswahili ama zinatofautiana kuhusu matumizi ya neno hili au hazieleweki au hazina neno kwa jambo linalojadiliwa.