Nanyindwa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search

Nanyindwa ni kijiji ambacho kipo kilomita kama kumi hivi kutoka Masasi mjini ukielekea kusini, kaskazini mwa mkoa wa Mtwara, Tanzania.

Katika kijiji hiki kuna mitaa miwili, Kilimani na Zaire na kimepakana na vijiji vya Lilala, Nangose, na Nraushi.

Wenyeji wake ni Wamakua japokuwa siku hizi kuna Wamakonde wachache. Wenyeji wa kijiji hiki walikuwa na mamwenye (machifu), Namunlia, Mwenye Nakavina.

Wanakijiji ni wakulima wa mahindi, mtama, ufuta na mihogo. Zao la biashara ni moja tu, lile la korosho.

Baadhi ya wanakijiji hula panya au samaki mchanga.

Umaarufu wa kijiji hiki unatokana na kuwa na kanisa la kwanza la Anglikana ambalo lilijengwa mwaka 1912. Kasisi wa kwanza mzalendo alikuwa akiitwa Padri Enrico Akuchigombo ambaye alifariki mwaka 1969 katika wilaya ya Tunduru.

Mwaka 2012 mabaki yake yalirejeshwa Nanyindwa na kuzikwa upya kando kidogo na kanisa hilo kongwe ambalo hata hivyo mwaka huo lilikarabatiwa na Mkuvia Maita ambaye ni mzaliwa na mkazi wa kijiji hicho; awali alikuwa akifanya kazi Ofisi ya Rais lakini akawa mchimbaji wa madini.

Kanisa hilo lilifanyiwa ibada ya kutabaruku na Askofu Mkuu wa Anglikana Tanzania, Dk Valentone Mokiwa 14 Septemba 2012 ambapo maaskofu wanne walihudhuria. Tarehe hiyo kanisa hilo lilikuwa likitimiza miaka 100 na sherehe kubwa hiyo ilichangiwa na watu mbalimbali akiwemo Cate Kamba,

Kijiji hiki kina shule ya msingi na zahanati. Shule hiyo iliwahi kutoa watu maarufu kama vile aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya kilimo, C.Y. Mpupua, daktari wa kwanza mweusi wilaya ya Nachingwea, Mzee Mpupua au Bwana Makiko.

Kijiji hiki ni maarufu kwa kutoa walimu wengi sana ambao walifundisha sehemu mbalimbali za wilaya ya Masasi, kama Carlo Mpupua, Richard Kandaya, Kamenya, Jacob Chitukoro aliyewahi kuwa msaidizi wa Katibu Mkuu wa CCM, Rashid Kawawa alikuwa katibu mnyeka, Julius Savava, Luca Munlia, Walace Chitukuro, Brigita Francis, Owen Lami na Charles Lami ambao walikuwa mapacha wakaacha kufundisha na kushangaza wengi, Mwalimu Pepetua, Mwl Kambulaje, Mwl Stephano Jumbe, Mwl Francis Nchihiya na wengine wengi.

Kijiji kimewahi kutoa waandishi wa habari mahiri wawili, Elvan Stambuli na Gabriel Kandaya na mtangazaji maarufu wa Radio Tanzania, George Mpupua pia alikuwa mwanamuziki akiimbia bendi za Mwenge Jazz (Paselepa), Uda Jazz, n.k.

Lakini pia kijiji hiki kilitoa mapadre wengi kama vile Padri Msamati, Padri Carlo na kadhalika na mashemasi kama vile shemasi George Rashid, Shemasi Munlia na kadhalika.

Kijiji kina mabomba ya maji na siku hizi kina umeme.

Flag-map of Tanzania.svg Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Mtwara bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Nanyindwa kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno.