Money Mondays

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Money Mondays
Money Mondays Cover
Studio album ya Vanessa Mdee
Imetolewa 15 Januari, 2018[1]
Imerekodiwa 2015, 2016-2017
Aina R&B, muziki wa dunia, ragga dancehall, Bongo Flava
Lebo Mdee Music
Mtayarishaji Vanessa Mdee (Mtayarisha Mkuu)
Nahreel
Ekelly
S2keezy
Tahpha
Bob Manecky
Breezy
Elloriks Music
Lufa
Single za kutoka katika albamu ya Money Mondays
 1. "Cash Madame"
  Imetolewa: 5 Disemba, 2016
 2. "Kisela"
  Imetolewa: 8 Agosti, 2017
 3. "Bounce"
  Imetolewa: 14 Novemba 2017
 4. "Wet"
  Imetolewa: 4 Aprili 2018
 5. "Bambino"
  Imetolewa: 29 Novemba 2018


"Money Monday" ni jina la albamu ya kwanza kutoka kwa msanii wa muziki wa kizazi kipya kutoka nchini Tanzania, Vanessa Mdee. Albamu imetoka rasmi tarehe 15 Januari, 2018, japo utangazaji wake ulianza tangu Novemba na mnamo tarehe 29 Disemba 2017 aliita vyombo vya habari kwa ajili ya utambulisho na uzinduzi huku akisindikizwa na Mohombi kutoka Sweden.[2] Januari 20, 2018 alikutana na mashabiki wake pale Mlimani City na kuwauzia albamu hii huku akitia saini katika kava za albamu. Baadaye Jux akaja na kununua albamu 25 kuahidi kuzigawa kwa watu wake wa karibu.[3] Albamu ina jumla ya nyimbo 18, huku 2 zikiwa kama nyimbo za ziada. Albamu imetayarishwa na watayarishaji mbalimbali lakini kazi kubwa ya kuiboresha ilifanywa na Chizan Brain kupitia B. Records. Nyimbo zilizotolewa kama singo ni pamoja na Cash Madame, Kisela na Bounce. Nyimbo zilizowekwa kama za ziada ni pamoja na No Body But Me aliyoimba na KO na Juu aliyoimba na Jux.[4] Wasanii walioshirikishwa kutoka katika albamu ni pamoja na Mohombi kutoka Sweden, Konshens kutoka Jamaica, Cassper Nyovest na K.O wote kutoka Afrika Kusini. Wengineo ni kina Joh Makini, Mr P, Reekado Banks, G Nako, Tahpha, Tammy Flavor, Maua Sama na Jux. Kwa upande wa utayarishaji albamu kuna mkono wa Nahreel, Kelly, S2Keezy, Tahpha, Bob Manecky, Breezy na Lufah.

Historia[hariri | hariri chanzo]

Nyuma ya kava la Money Mondays

Mazungumzo juu ya albamu yalianza miaka mingi. Lakini tarehe19 Aprili, 2015, Vanessa alifunguka kiasi kuhusu jina la albamu na nia ya kuita hivyo katika kipindi cha "The Playlist" cha Times FM - katika mahojiano yake na Lil Ommy. Nessa alisema kwa vile wanamwita Vee Money, na alitaka kutengeneza albamu ambayo itaelezea pilika zake za muziki tangu alikotoka hadi sasa. Hasa ukitazamia Monday ni siku ya kwanza katika wiki za kazi, na kila mtu huenda mihangaikoni kujitafutia riziki.[5] Yeye hasa aliona kila Jumatatu, yaani, Monday, ni fursa mpya katika kubadilisha maisha yako. Halkadhalika imetumika kama sitiari ya kutokata tamaa, kwani ikiwa umekosa Jumatatu iliyopita, basi Jumatatu hii ile fursa unaweza kujaribu tena na tena. Nessa, anaona safari yake ya kimuziki inaanza rasmi baada ya kutoa albamu. Katika mahoajiano hayo, alitaja baadhi ya nyimbo zitakazo kuwepo katika albamu. Nyimbo hizo ni pamoja na Closer, No Body But Me, Come Over, Siri na Hawajui. Lakini baada ya kutoka albamu nyimbo zilizotajwa hazikuwepo zote, bali moja tu "No Body But Me". Nayo iliwekwa kama wimbo wa ziada ikiwa imeongozana na "Juu" ambayo kaimba na mpenzi wake Juma Jux.

Ili kutimiza jina la albamu, karibia nyimbo nyingi za Nessa zimetolewa siku ya Jumatatu, yaani, Monday. Nyimbo hizo ni pamoja na Kisela, Hawajui, na albamu imetolewa tarehe 15 Januari, 2018 nayo ni Jumatatu. Vilevile mapato atakayopata kupitia wimbo wa "Pumzi ya Mwisho" atagawana nusu kwa nusu na familia ya Mbaraka Mwinshehe. Nessa kabla ya kutoa albamu, aliiendea familia ya marehemu Mbaraka Mwinshehe na kuomba ridhaa ya kutumia sehemu ya kionjo cha nyimbo hiyo. Gawio kwa familia hiyo ni kwa manunuzi ya kidijitali, yaani uuzwaji kwa njia ya mtandaoni.[6]

Orodha ya nyimbo[hariri | hariri chanzo]

Hii ni orodha ya nyimbo zinazopatikana katika albamu ya "Money Mondays".

Na. Jina la wimbo Mtayarishaji Maelezo
1 Intro
2 Kisela Ekelly Kamshirikisha Mr. P wa P Square.
3 Unfollow S2keezy
4 Floating On a Wave Nahreel
5 Don’t You know Nahreel Akiwa na Tahpha
6 African Hustle (Interlude)
7 Cash Madame Ekelly
8 Pumzi ya Mwisho S2keezy Kamshirikisha Cassper Nyovest na Joh Makini
9 Wet Nahreel akiwa na G Nako
10 Scratch My Back Elloriks Music Radio na Weasel
11 Shadee (Interlude)
12 Bounce Breezy Maua Sama na Tommy Flavour
13 Kwangu Njoo Breezy Akiwa na Mohombi
14 The Way You Are Bob Manecky
15 Bomb Nahreel akiwa na Konshens
16 Bambino Ekelly Akiwa na Reekado Banks
17 No Body But Me Nahreel Akiwa na KO
18 18. Juu Lufa Akiwa na Jux

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]